Mazingira Manne ya Kimalezi Yanayotengeneza Tabia za Watoto

Watafiti wa makuzi na malezi wanasema mtoto anahitaji mazingira yanayomchangamsha kihisia, kiakili, kimwili na kimahusiano. Anapochangamshwa vyema, tunaambiwa, mtoto hujisikia utulivu wa moyo unaomfanya awe karibu na wazazi na watu wengine wanaomzunguka. Anapokosa kuchangamshwa, mtoto hujenga uduwavu unaojenga tabia za kujilinda na uchungu wa kujiona anapuuzwa. Katika makala haya, tunaangazia mambo manne yanayoweza kumchangamsha mtoto kihisia na kimahusiano na hivyo kutengeneza tabia na mitazamo yake.
Kumwelewa anataka nini

Huu ni uwezo wa mzazi kujua mtoto anataka nini na kwa wakati gani. Kwa mfano mtoto anapolia yaweza kuwa njaa, maumivu, hasira, wasiwasi, kutafuta kusikilizwa na kadhalika. Mzazi anayeweza kuelewa vizuri ujumbe huo humfanya mtoto ajione mwenye sauti inayosikika.

Wakati mwingine ni vigumu kuelewa kwa nini watoto hupenda kucheza karibu muda wote. Ni hitaji lao.  Picha: APF

Kinyume chake ni kutokutambua na wakati mwingine kupuuza anachokihitaji mtoto. Ni pamoja na kuchukua hatua zinazokidhi mahitaji yetu ambayo kimsingi si yale ya mtoto mwenyewe. Mfano ni pale mtoto anapotaka kucheza na wenzake, lakini mzazi asionekane kujali hitaji hilo na kumwamuru akalale. Kumwelewa ni kumfanya mtoto akalale hali akiamini hitaji lake la kucheza linaeleweka na halijapuuzwa.

Kumkubali bila kujali alivyo

Mtoto anapozaliwa mambo mengi hubadilika katika familia. Kuna kubadilika kwa utaratibu wa kulala na kuamka, mwonekano na umbile la mwili (kwa mama), na hata tabia. Kukubali kubadilika shauri ya mtoto ni kupokea jukumu zito la malezi. Kadhalika, kumkubali mtoto bila kujali jinsia yake, ulemavu wake, rangi isiyo tarajiwa, hutuma ujumbe unaomjengea mtoto kujiamini.

Kinyume chake ni kumfanya mtoto ajisikie kukataliwa kwa sababu pengine hayuko katika hali iliyotarajiwa na wazazi au kuna sababu nyingine. Tunajua, kwa mfano, wapo wazazi tunaoacha kuwanyonyesha watoto mapema bila sababu za msingi isipokuwa labda kuogopa kupoteza umbile la usichana. Kitendo hiki chaweza kuchangia kuzorotesha hali ya mtoto kujiamini.

Kushirikiana naye

Tangu kuzaliwa, mtoto huhitaji kuwasiliana na kushirikiana na watu wanaomzunguka. Mfano, hutabasamu anapowaona watu akitafuta kushirikiana nao. Kumpa nafasi ya kuhusiana naye humfanya ajisikie kuthaminiwa. 

Kinyume chake ni kushindwa kushirikiana nae na kutokuelewa hitaji la uhuru wake kwa kumwingilia kupita kiasi. Hali hii humfanya ajisikie kubanwa na hujiona hana uwezo wa kufanya lolote bila ‘msaada’ wa mtu mwingine. Matokeo yake mtoto hunyong'onyea na kupoteza kujiamini.

Kuwa na muda wa kupatikana

Kupatikana ni kuwepo kwenye maisha ya mtoto kimwili na kihisia. Ni kuwa na muda wa kutosha na mtoto ili kufahamu yanayoendelea kwenye maisha yake. Kuahirisha 'mambo mengine muhimu' ili kuwa na muda na mtoto hujenga hali ya kuaminika.

Kinyume chake, ni kuweka mbele shughuli nyingine za kimaisha tunaziziona kuwa za maana zaidi na wakati mwingine kuwaachia wengine jukumu letu la malezi. Hali hii huweza kumfanya mtoto ajione hathaminiki na hujenga tabia za kujihami.

Matokeo ya mazingira hayo ni nini?

Manne hayo kwa pamoja yana athari kubwa mbili. Kwanza, yanaathiri namna mtoto anavyojiona yeye mwenyewe na pili, namna anavyowaona na kuhusiana na watu wengine wanaomzunguka. Mchanganyiko wa mazingira hayo manne ya kimalezi, kama tulivyoona hapo juu, yanaweza kuzaa tabia kuu nne kwa mtoto.


Barua pepe: bwaya@mwecau.ac.tz

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?