Kipimo cha Kujitambua ni Tunavyowatendea Tusiowajua, Wasioheshimika
Mjema
anaandika ripoti inayohitajiwa na mkuu wake wa kazi. Wakati muda wa kukabidhi
ripoti hiyo ukikaribia, anapigiwa simu na mtu asiyemfahamu. Mjema hajui ni nani
hasa anayemtafuta muda huo hivyo anaamua kupokea simu. Bahati mbaya aliyempigia
simu hasikiki vyema. Mjema anahisi labda ni tatizo la mtandao, anaamua kuikata
mara moja.
Baada
ya dakika moja, namba ile ile inampigia tena. Mjema anapokea simu. Kwa mara
nyingine anayeongea upande wa pili wa simu hasikiki vyema. Mjema anajisikia kusumbuliwa
na anakasirika. Anakata simu kwa hasira. Mara ya tatu, namba ile ile inaita
tena. Mjema anaudhika na kupandwa na hasira. Mara hii, anaipokea kwa hasira na
kuporomosha matusi ya nguoni mfululizo na kukata simu mara moja.
Baada
ya dakika tatu, Mjema anapokea ujumbe mfupi wa maandishi kutoka namba hiyo
hiyo. Mara hii mhusika anajitambulisha na kuomba msamaha kwa kumsumbua na
kukata simu. Mjema anagundua kumbe aliyekuwa anamsumbua muda wote huo alikuwa
ni Mkurugenzi wa kitengo anachofanyia kazi. Mjema anachanganyikiwa na kuhaha
asijue la kufanya. Huku akijutia kitendo cha kumtukana mkuu wake wa kazi (bila
kujua), anaamua kupiga simu haraka kuomba msamaha kwa kitendo chake hicho.
Kwa
nini Mjema anasikitika kumtukana mkuu wake wa kazi bila kujua? Je, kama Mjema
angegundua kuwa huyo aliyemtukana bila kujua alikuwa ni mtu asiye na hadhi
yoyote katika jamii na asiyeweza kuathiri maisha yake kwa namna yoyote,
angesikitika kwa kiwango hicho hicho? Kwa nini?
Kulazimika kuwa vile tusivyo?
Tukio
kama hili hutukuta wengi wetu katika maisha yetu ya kila siku. Tunapokuwa na watu
tunaowaheshimu, kama wazazi wetu, wapenzi wetu, viongozi wa dini, wakuu wa
kazi, tunajiweka katika sura inayoheshimika. Tunafanya jitihada za kuonekana
wanyenyekevu ili kupata heshima yao. Tunaogopa kudharauliwa na watu hao na
hivyo tunajitahidi kujiweka katika hali wanazozitarajia kwetu.
Wakati
mwingine tunafanya kinyume. Tunapokuwa na watu tunaodhani ni wa hadhi ya chini,
wasioheshimika, hatuoneshi heshima. Kwa mfano, tunapoongea na wahudumu wa
migahawa ya chakula ni rahisi kuonesha dharau ambazo kwa hakika tusingethubutu
kuzionesha kwa watu tunaowaheshimu. Tunafanya hivyo kwa sababu tunajua hata
wanapojisikia vibaya, hatupati hasara yoyote.
Kadhalika, tunapokwenda mahali tunapojua hatufahamiki tunabadili tabia zetu. Tunageuka kuwa watu wengine kabisa kiasi kwamba kama angetokea anayetufahamu angeshangaa. Kubadilika huku kwa ghafla ni kujaribu kuwa vile tulivyo katika uhalisia wetu kwa sababu kufahamika hutufanya tulazimike kuwa tusivyo.
Kujenga taswira inayotarajiwa?
Kuna ukweli kuwa mwanadamu
anayo kawaida ya kujenga taswira anayojua wengine wanaitarajia kwake. Tunaweza
kuwa na sura fulani tuwapo wenyewe lakini tunapokuwa katikati ya wengine tunavaa sura nyingine na kufanya
vinginevyo. Uwepo wa watu wengine hutulazimisha kubadili tabia zetu ili kukidhi
matarajio ya watu hao.
Marafiki hujua kujenga taswira zinazotarajiwa. PICHA: HONGQI ZHANG |
Wakati
mwingine tunavuka mipaka na kujikuta tunaigiza tabia zisizo halisi ili kuzidi uhalisia wetu. Tunalazimika kujibadilisha badilisha kama kinyonga kama
jitihada za kutengeneza hadhi bandia tunazozihitaji kwa wengine.
Hadhi,
hata hivyo, si jambo baya wakati wote. Kujenga taswira chanya kwa wengine
hutusaidia kujua namna bora ya kuenenda mbele za watu.
Mathalani, ni kawaida tunapojiandaa kwenda
kukutana na watu wengine tunajitazama kwenye kioo kuhakikisha tunaonekana
vyema. Tunakuwa makini kuhakikisha tunakuwa na taswira chanya hata ikibidi kwa
kufikiria namna gani tutatabasamu, tutakavyokaa na hata ikibidi badili kidogo mwonekano
wa nywele, tunavyoa ndevu na kadhalika. Hizo zote ni jitihada za kujenga taswira inayotarajiwa na wengine.
Aidha,
tunajitahidi kuvaa mavazi ya kupendeza kwa lengo la kukidhi hadhi tunazotaka
kuwa nazo katika jamii. Tunavaa tai, makoti, nguo za rangi na mitindo mbalimbali kuongeza kukubalika kwetu, jambo ambalo, kwa hakika, si baya linapofanyika kwa
nia njema. Ndio kusema kuyasoma mazingira ya kijamii yanataka nini ili tutende
yapasayo ni sehemu ya busara ya kawaida ya kibinadamu.
Ulaghai wa taswira chanya?
Lakini
kwa upande mwingine, kudhibiti namna watu wanavyotuona kama mbinu ya kuwafanya
waone uzuri tusiokuwanao yaweza kuwa tatizo. Kwa mfano, kuongea kwa staha na
mtu tunayemheshimu haiwezi kuchukuliwa kuwa ni tabia yetu halisi ikiwa tunaweza
kuonesha dharau kwa mtu tunayemwona kama asiyestahili heshima. Kuonesha staha
kwa tunayemheshimu inaweza kuchukuliwa kuwa mbinu tu ya kuipata heshima yake.
Wakati
mwingine tunaweza kushangaa iweje, kwa mfano, binti anayeongea kwa adabu na
nidhamu ya hali ya juu kwa kijana aliyeonesha nia ya kumchumbia akawa na dharau
zilizopitiliza kwa wahudumu wa mgahawa wa chakula. Ukweli ni kwamba tabia halisi ya binti
huyu ni dharau kwa sababu kwa mhudumu wa mgahawa halazimiki kujenga taswira fulani. Hivyo anapozungumza na mhudumu huyu huo ndio unakuwa uhalisia wake. Nidhamu anayoionesha kwa kijana yule mwenye matazamio
fulani kwake ni mbinu tu ya kujenga hadhi inatakayomwezesha kukubalika.
Tabia zinazokubalika huanzia ndani
Tunaweza
kusema kubadilika badilika kwa lengo la kuendana na mazingira ya kimahusiano yaweza
kuwa dalili ya kutokujikubali na hata kutokujitambua. Mtu anayejielewa na kujikubali
halazimiki kubadilika kilaghai kukidhi matarajio yasiyokuwepo. Kwa lugha
nyingine, tabia zake njema huanzia ndani na kujidhihirisha nje kwa namna ile
ile kwa watu wote bila kujali mazingira ya kimahusiano.
Ili
kupima tabia zetu halisi na kujitambua kwetu, ni muhimu kuangalia
tunavyowatendea watu wasioheshimika; tunavyoongea na watu tusiowafahamu; tunavyowajibu
makondakta wa daladala; tunavyowasemesha wahudumu wa mikahawa. Tukitaka kujua
tabia ya mtu, pa kuanzia ni kuangalia anavyowatendea watu wa chini yake na
wasiomsaidia. Kwa sababu kujitambua ni kuelewa binadamu wote wanastahili
heshima yetu ya dhati bila kujali nafasi na hadhi walizonazo. Unakubaliana na
hitimisho hili? Udhani inawezekana?
Kwa mijadala zaidi fuatilia safu ya Saikolojia katika gazeti la Mtanzania kila Alhamisi.
Barua pepe: bwaya@mwecau.ac.tz
Ndg Bwaya, kwanza nikupongeze kwa makala nzuri, bila shaka wengi watajifunza kupitia makala hii kama nilivyojifunza mimi.
JibuFutaBinafsi nina maoni ya ziada juu ya badiliko la tabia kwa watu mbali mbali kulingana na mazingira. Tabia tofauti kwa watu (mazingira) tofauti yaweza kusababishwa na mambo mengi. Jambo la kwanza ni kama ulivyolieleza kwa kina katika makala hii.
Jambo la pili ni kuwa inategemea na mahusiano baina ya muonyesha tabia na muonyeshwa tabia. Mfano, kama tumezoea kutaniana, basi kila tunapokutana tabia ya kutaniana haiwi mbali. Habari Njema ni kwamba, wawili hao kwa muda wote watakaokuwa pamoja wanajua ni wapi walitania na ni wapi walimaanisha walichokifanya ama kusema.
Lakini kama mahusiano yetu hayako katika mazingira ya kutaniana, utategemea mawasiliano ya mwelekeo huo. Hii ni kusema kwamba, mara nyingine tunaweza kutoa hukumu isiostahili juu ya tabia za watu kama "hukumu" yetu haikuzingatia muktadha wa mawasiliano yao.
Maranya O'Mayengo
Ndugu Maranya, asante sana kwa maoni yako makini. Naamini wasomaji wa blogu hii watajifunza kwa uliyoyaandika pia.
JibuFutaNi kweli kama unavyosema, hukumu ya kwa nini tunatenda tuyafanyayo inategemea sana na namna mwonesha tabia anavyohusiana na mwoneshwa. Msingi wa hoja ya makala haya ni kwamba tabia halisi ni zile tunazozionesha kwa wale tusiowachukulia kwa uzito katika maisha yetu na hivyo hatulazimiki kujenga taswira chanya kwao.
Nadhani utani wa kirafiki ni suala tofauti kidogo na linahitaji mjadala unaojitegemea. Hata hivyo, ni kweli kwamba huwa hatutaniani na kila mtu. Na tunapotaniana mara nyingi malengo yetu huwa si kujenga taswira fulani chanya kwa tunayetaniana naye. Kwa hiyo, ni vigumu maudhui ya makala haya kujibu suala hili ipasavyo.