Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia

Ingawa ni kweli tunazaliwa na sehemu ya tabia tulizonazo, upo ukweli wa kiutafiti unaothibitisha kwamba mazingira ya kimalezi yana nafasi kubwa katika kujenga tabia za mtu. Ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili, mathalani, unatawaliwa zaidi na uasili ambao kwa kiasi kubwa hatuna mamlaka nao. Hata hivyo, ukuaji wa kihisia na kimahusiano unatawaliwa zaidi na mazingira ya kimalezi ambayo tayari tuliyaona kwenye makala iliyopita.
Katika makala haya, tutaangalia makundi manne ya tabia za watoto ambazo kimsingi ni zao la aina ya malezi tunayowapa watoto wetu. Lengo si kujenga hatia kwa wazazi bali kutusaidia kuelewa namna gani tunaweza kufanya yaliyo katika uwezo wetu kuwasaidia watoto kuwa na tabia tunazotamani wawe nazo.

Mtoto mtulivu, mkarimu

Huyu ni mtoto anayewaamini wazazi na watu wanaomzunguka. Utulivu wake unasababishwa na kujiona yu katika mazingira salama na hivyo hana wasiwasi. Kutokuwa na wasiwasi kunamfanya asiwe mgomvi wala msumbufu na hivyo hana tabia kulia lia bila sababu. Kulia kwa watoto mara nyingi ni kuonesha kutokuridhika. Mtoto anapolia mara kwa mara bila sababu za msingi, maana yake hana utulivu wa nafsi. Huyu hana sababu ya kulia kwa sababu nafsi yake imetulia.

Kumpa fursa ya kukidhi mahitaji yake hujenga kujiamini. Picha: @bwaya
Kadhalika, mtoto wa kundi hili ni mkarimu kwa wenzake. Anapokuwa na kitu ni mwepesi kuwapa wengine. 

Ni kama anajisikia fahari kushirikiana alichonacho na wengine. Ni mtoto mwenye upendo wa dhahiri na hana ubinafsi.




Kadri anavyoendelea kukua, hujifunza kirahisi sana kutatua migogoro pasi na  njia za kibabe. Huyu ni aina ya mtoto anayeweza kuwaambia wenzake, ‘nitakusemea kwa baba/mama’ kwa sababu haoni sababu ya kupigana nao.

Tabia hii ya utulivu ni matokeo ya malezi yanayomwelewa, yanayomshirikisha, yanayomkubali na kumweka karibu. Kwa hiyo, anajisikia mtu aliyeshiba na hana njaa ya ‘kueleweka’, ‘kushirikishwa’ ‘kukubaliwa’ na ‘kupendwa’.

Ukiacha watoto wa kundi hili, lipo kundi la watoto wenye changamoto tofauti za nafsi waliogawanywa katika makundi madogo matatu; wale wanaojitenga na watu, waongeaji lakini wasiojiamini kwa siri na wale wakorofi.

Mtoto anayejiamini, lakini hujitenga na watu

Huyu ni mtoto anayejiamini lakini anayejiona bora kuliko wengine. Kwa maneno mengine, anaamini wengine hawatamfaa na wanaweza kumsumbua. Kimsingi hajisikii salama anapokuwa na wengine ndio sababu ana tabia ya kujilinda kwa kujitenga. 

Mara nyingi ni mkimya na hana maneno mengi ingawa anaweza kuwa na uwezo mzuri kiakili. Wapo watoto  wa kundi hili wanaoweza kuwa na namna fulani ya kiburi au hali ya kuwadharau wengine. Sababu kubwa ni kujiona kujengeka kwa ubinafsi fulani ndani yao.

Ni rahisi kumgundua mtoto wa kundi hili tangu akiwa mdogo kwa tabia ya kutokujali sana pale anapoachwa na mama yake au mlezi wake wa karibu. Ingawa wakati mwingine anaweza kulia kuonesha kutokutaka mama aondoke, lakini mama yake anaporudi, hastuki. Kutokusisimshwa na kurudi kwa mama ni namna ya kusema hana ukaribu na watu na ni mbinafsi anayejiangalia yeye kuliko wengine. 

Tabia hii ni matokeo ya malezi yanayoonekana kutokujali (yanayopuuza) hisia za mtoto ingawa yanamshirikisha na kuonesha kumwelewa. Ingawa wazazi wa watoto hawa wana ukaribu na watoto wao, changamoto yao ni kushindwa kuonesha kuelewa hisia za mtoto. Mtoto anaposhitaki kuonewa na wenzake kwa mfano, mzazi hujibu kirahisi rahisi au kupuuza kabisa maumivu ya mtoto. Hali hiyo hudumaza uwezo wa mtoto kuelewa hisia za wengine.

Mtoto mwongeaji lakini asiyejiamini

Huyu ni mtoto mwenye wasiwasi na vile anavyojiona ingawa anawaona wengine kuwa bora kuliko yeye. Kimsingi hajiamini sana na anajiona hawezi kufanya mengi bila ‘kuzungukwa’ na watu muhimu. Kwa sababu hiyo anapenda sana kujichanganya na watu kufidia hisia za upweke wa siri ndani yake. Tofauti ndogo ndogo za watoto wa kundi hili zipo. Wapo wale wapole hasa wanapokuwa katikati ya watu wasioonekana kuwaelewa vyema, lakini wapokutana na watu wanaowaelewa, ni wachangamfu na waongeaji kuliko kawaida. Upole na uongeaji ni namna ya kujihami na upungufu wanaojisikia ndani yao.

Kwa ujumla, mtoto wa kundi hili ameathirika na tabia ya wazazi watoro (wasiopatikana) kimwili. Mtoto huyu amelelewa katika mazingira ya wazazi wake kuwepo na kutokuwepo kwa wakati huo huo. Mfano rahisi ni wazazi wenye shughuli nyingi zinazowalazimu kuwa mbali na nyumbani au na familia zao muda mwingi lakini hata hivyo wenye kuwaonesha watoto wao upendo. 

Matokeo ya mchanganyiko wa wazazi kujali na kutokupatikana ni watoto kuamini wazazi wao hawawajali ipasavyo ingawa wanajua (wazazi) wanawapenda. Wanajikuta wakiamini wengine ndio waliobeba furaha yao na hivyo bila kuzungukwa na watu wenye uwezo wa kuleta furaha yao, hawawezi kuwa na furaha iliyo kamilifu.

Hutokea wakati mwingine shauri ya kujihisi hapati ushirikiano anaoutaka mtoto wa kundi hili hujenga hisia za kujistukia na kujenga kisasi cha utoto. Kwa hiyo huwa na hasira na hali ya kubeba vitu moyoni hasa wengine wanaposhindwa kutambua nafasi yao.


Mtoto mkorofi/mtundu

Huyu ni mtoto asiyejielewa. Ni mtoto aliyechanganyikiwa. Hujiona hana thamani na wengine wanaomzunguka hawana maana pia kama alivyo yeye. Ni mtoto anayejidharau na kudharau wengine. Hana hisia na haelewi hisia za wengine na ndio sababu huwa mgomvi na mtundu. Ugomvi ni namna yake ya kujitutumua kufidia uduni na ubinafsi uliokithiri anaohisi ndani.

Mtoto huyu ni kama anafurahia kuwaona wengine wakiumia kwa hiyo huwachokoza wengine na hata kuwatukana ilmuradi ajisikie na yeye yumo. Ni mchoyo hasa kama amekulia kwenye mazingira ya kukosa vitu vya msingi.

Kinachomfanya awe mgomvi ni malezi yasiyoheshimu hisia zake yenye uonevu. Mfano ni wazazi kuwa wagomvi mbele yake, wenye matusi na namna nyingine za kukosa staha. Kadhalika, wazazi wenye tabia ya kutumia nguvu katika malezi, mathalani, kuchapa kunakoashiria ugomvi kuliko kurekebisha tabia ya mtoto.  Vile vile wazazi wenye hasira na uchungu wa muda mrefu wana uwezekano wa kuwa na mtoto wa namna hii wasiopochukua hatua mapema. Vinginevyo, ni rahisi (wazazi hawa) kumtumia mtoto kama namna ya kupambana na maumivu na uchungu wao kwa kumwonesha mtoto ghadhabu.

Itaendelea

Makala haya yalichapishwa kwenye gazeti la Mtanzania. Kwa mijadala zaidi  ya Malezi fuatilia safu ya Uwanja wa Wazazi katika gazeti la Mtanzania kila Alhamisi.
Barua pepe: bwaya@mwecau.ac.tz


Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Mbinu za Kujenga Ujuzi wa Mwanafunzi