Umuhimu wa Kujenga Tabia ya Kujitolea
Kujitolea ni kutoa sehemu ya muda wako, ujuzi na maarifa uliyonayo
na wakati mwingine nguvu zako kufanya kazi ya watu wengine bila kupata malipo ya
moja kwa moja. Kazi unayoifanya kwa kujitolea mara nyingi ungeweza kuifanya kwa
kudai ujira lakini unaamua kuifanya bure. Mathalani, mwajiriwa anayetamani kuleta mabadiliko nje ya ajira yake, anapotumia ujuzi wake kufanya kazi za jamii bila kudai malipo, anakuwa amejitolea. Tuangalie kwa mhutasari kwa nini ni
muhimu kujenga tabia ya kujitolea.
PICHA: jimmyscambridge.net |
Kusaidia kutatua
matatizo ya jamii
Maisha ni zaidi ya fedha. Mtazamo huu unaweza kuzua mjadala mrefu kutokana na tofauti za kimatazamo, lakini upo ukweli kwamba fedha si kila
kitu. Hatuishi kwa lengo la kujikusanyia fedha kujiletea faida binafsi na iishie hapo
ingawa ni kweli tunahitaji fedha.
Kujitolea, kwa mantiki hii, ni kuelewa kuwa si lazima ubadilishane ujuzi na muda wako kwa vipande vya fedha. Wakati mwingine waweza kutoa ujuzi, maarifa na nguvu
zako kwa lengo tu la kujisikia furaha ya kutoa mchango wako katika kuboresha maisha ya wengine
ambao katika hali ya kawaida wasingeweza kunufaika na ujuzi huo bila kukulipa.
Mhitimu wa chuo cha ualimu, kwa mfano, wakati akisubiri
ajira ya ualimu anaweza kuamua kuomba kujitolea kufundisha katika shule ya kata
iliyoko kijijini kwake bila malipo anayostahili. Kwa kujitolea huko, kijana huyu anajisikia kutoa
mchango muhimu katika kukabiliana na tatizo sugu la ukosefu wa walimu kijijini kwake badala
ya kusubiri wengine watafute majibu ya tatizo hili.
Kujifunza ujuzi bila
gharama
Si kila ujuzi tunaouhitaji makazini tunaupata vyuoni. Mara
nyingi vyuo hutufunza maarifa ya jumla yanayoweza yasioane kabisa na
matakwa ya soko la ajira. Hii ni kwa sababu si rahisi vyuo kufanya utafiti wa mara kwa mara kubaini mahitaji
ya soko la ajira kwa minajili ya kurekebisha mitaala yao.
Kadhalika, ni vigumu kwa mfumo wa elimu kukidhi
mahitaji mahususi ya kila mhitimu na kila mwajiri. Kwa sababu hiyo, vyuo hujikuta vikifundisha maarifa ya jumla ambayo katika hali halisi yanaweza yasikidhi mahitaji ya waajiri.
Katika mazingira haya, kujitolea hutusaidia kujifunza ujuzi mahususi
tunaouhitaji ili kuajirika kirahisi bila kulazimika
kuulipia kwa fedha isipokuwa kwa kutumia nguvu na muda wetu. Kwa mfano, mhitimu wa teknolojia
ya mawasiliano anaweza kujitolea kufanya kazi katika kampuni ya mawasiliano na hivyo
kujifunza mambo mengi ambayo huenda hakujifunza akiwa chuoni. Kwa kutoa muda na nguvu
zake bila kutarajia malipo, mhitimu huyu hupata faida ya kujiongezea nafasi ya
kuajirika pale nafasi za kazi zinapojitokeza.
Kujitafutia uzoefu
unaohitajika
Waajiri wengi huweka sharti la waombaji kuonesha uzoefu wa kazi wanayoiomba kama ushahidi wa uwezo wa kumudu kazi husika. Hiki, kwa hakika, ni
kikwazo kwa waombaji wengi hasa wanaotoka vyuoni moja kwa moja kwa sababu ni kweli huwa hawajawahi kuajiriwa na hivyo hawana uzoefu. Pamoja na ugumu wa sharti hili la uzoefu, bado litaendelea kuwa sehemu muhimu ya matangazo ya ajira.
Kuwasaidia wasioweza kukulipa kunakupa furaha PICHA: |
Kujitolea kwaweza kuwa sehemu ya suluhisho la sharti hili.
Unapojitolea bila malipo, unajitengenezea uzoefu utakaouhitaji na mwajiri bila
kulazimika kuajiriwa. Kujenga tabia ya kujitolea ni kuchukua hatua za makusudi kupambana na sharti hili.
Kwa kutokutambua umuhimu wa kujitolea, wahitimu wengi
wamekuwa walitumia muda mwingi kulalamikia sharti la uzoefu wakati katika hali
halisi hawafanyi chochote kukabiliana na changamoto hiyo. Wanabaki kusoma
magazeti na kuulizia nafasi za kazi ambazo hata wanapoomba wanajikuta hawakidhi vigezo vya uzoefu.
Ni vyema kutambua kuwa waajiri huvutiwa na mwombaji kazi aliyetayari kujitolea. Mwombaji mwenye historia ya kujitolea muda na ujuzi wake kuwanufaisha wengine anakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kushindana na wenzake wasiojitolea. Kujitolea kwaweza kuwa namna ya kuongeza uwezekano wa kuajirika.
Kujiongezea mtandao
wa kiajira
Katika siku za leo, mtandao wa kiajira ni hitaji muhimu.
Mtu anayefahamiana na watu wengi kwenye maeneo mbalimbali ya kikazi anajiongezea
fursa ya kuunganishwa na taarifa za kiajira. Siku hizi wanasema watu ni mtaji.
Aina ya mitandao ya kiajira tunayoijenga, mara nyingi
hutegemea tunafahamiana na watu wa aina
gani. kwa hiyo si kazi nyepesi, kwa mfano, kijana anayetoka kwenye familia za tabaka la
chini kijijini kufahamiana na watu wengi mjini wanaoweza kumpa taarifa za kiajira anazozihitaji. Ili kupata taarifa hizo muhimu kijana huyu hujikuta akitumia
nguvu nyingi sana zisizolingana na matokeo.
Kujitolea kwaweza kumsaidia mtafuta ajira wa aina hii kujiongeza
kimtandao. Unapokuwa tayari kufanya kazi za kujitolea kwa bidii na maarifa katika
maeneo mbalimbali, mathalani, unakutana na watu wa kada na wenye uzoefu tofauti. Ingawa ni kweli hupati
kipato unachokihitaji (sana) kwa wakati huo, lakini bado unakuwa na fursa ya
kujitengenezea mtandao muhimu wa watu wanaoweza kukufaa katika safari yako ya
kutafuta ajira.
Changamoto za
kujitolea
Pamoja na faida za kujenga utamaduni wa kujitolea, zipo
changamoto kadhaa. Kwa mfano, zipo taasisi za kinyonyaji zinaopenda kutumia nguvu
za watu bure kwa mwamvuli wa kujenga utamaduni wa kujitolea. Taasisi hizi hutumia shida za watu wasio na ajira kutafuta nguvu kazi itakayowawezesha kufikia malengo yao bila gharama kubwa ya kifedha (cheap labour). Ni vizuri kutambua 'unyonyaji' wa taasisi zenye tabia hii na kufanya
maamuzi sahihi yatakayokunufaisha na wewe kiujuzi na kiuzoefu. Tuliwahi kuaswa na kiongozi
mmoja kuwa wakati mwingine ni lazima kukubali kupoteza kidogo ili kupata.
Kadhalika, upo mtazamo hasi dhidi ya kujitolea. Wapo
wanaofikiri kujitolea ni kutokuwa na kazi ya kufanya. Katika mazingira yaliyojaa umasikini, ni vigumu watu kuelewa inakuwaje mtu anaweza 'kupoteza muda wake' kujitolea badala ya kuchapa kazi zinazomwingizia kipato. Wengine wanafikiri kufanya kazi bila
malipo ni kujidhalilisha utu wako.
Hata hivyo, tunaweza kuchukua hatua za kukabiliana na
changamoto hizi kulingana na mazingira yetu yalivyo ili tuweze kufikia malengo
yetu kwa wepesi. Kwa mfano, yako maeneo mengi tunayoweza kujitolea bila kukabiliana na vizuizi vingi. Kuna shule zisizo na walimu katika kila pembe ya nchi yetu, zipo taasisi nyingi zisizojiendesha kibiashara zinazojaribu kusaidia kutatua matatizo mbalimbali katika jamii yetu. Tunaweza kutumia taasisi hizi kama kianzio muhimu cha kujenga ari ya kujitolea.
Waajiri nao, kwa upande wao wanahitaji kubadilisha mitazamo
yao na kuweka mazingira yanayoruhusu wenye nia ya kujitolea kupata fursa hiyo. Kwa kufanya hivyo, wanatoa mchango wa kujenga daraja zuri linaunganisha maarifa ya darasani na hali halisi na hivyo kujenga ujuzi ambao wao wenyewe wanalalamika kuwa wahitimu hawanao.
Tuone fahari kujitolea
Ni muhimu kwa jamii yetu kujenga tabia ya kujitolea. Tujitolee
kuwasaidia wengine. Tujitolee muda na raslimali tulizo nazo kutatua changamoto zinazoikabili jamii yetu. Upo ukweli
wa kiutafiti kwamba unapowafanya wengine wawe na furaha, unakuwa na furaha
zaidi. Unapochangia kutatua changamoto za wengine, unajiwekea akiba ya mbeleni. Tuache hulka za kimaskini kwamba kila unalolifanya lazima likuingizie fedha. Hatuwezi kubadilisha mambo mengi kwa ujira.
Soma gazeti la Mtanzania kila Alhamisi kwa mada kama hizi kwenye safu ya Saikolojia.
Safi sana sir Bwaya!! Mungu akuongoze na kukupa nguvu katika kuelimisha umma!! I appreciate you!!!
JibuFutaSafi sana sir Bwaya!! Mungu akuongoze na kukupa nguvu katika kuelimisha umma!! I appreciate you!!!
JibuFutanakubari
JibuFuta