Kujenga Tabia ya Kusoma kwa Watoto Wadogo
Kusoma
si tabia nyepesi kuijenga katika mazingira ambayo masimulizi na mazungumzo ni vyanzo vikuu vya maarifa kuliko maandishi. Tumelelewa katika utamaduni usiosisitiza
sana umuhimu wa kusoma. Lakini, hata hivyo, hatuwezi kukwepa kusoma katika ulimwengu
huu unaotulazimisha kuyasaka maarifa kwa njia ya maandishi.
Kadhalika,
mafanikio ya mtoto kitaaluma yana uhusiano wa moja kwa moja na utamaduni wa
kujisomea. Mtoto asiyependa kusoma anajiweka katika hatari ya kuwa na mafanikio
dhaifu kielemu kwa sababu, katika mfumo wa elimu, kusoma si uamuzi binafsi.
Kwa
hivyo, ikiwa tunatamani watoto wetu wafanikiwe kielimu sambamba na kujenga
utamaduni wa kujisomea bila kushurutishwa, tunao wajibu mkubwa wa kuwajengea
utamaduni huo tangu wangali wadogo. Katika makala haya tunaangalia mbinu nne rahisi zinazoweza kuwasaidia watoto wetu kupenda kusoma.
Kuweka
mazingira ya kujisomea
Mazingira
yanayohamasisha kujisomea ni pamoja na kuhakikisha vitabu vinapatikana
nyumbani. Tafiti zinaonesha kuwa watoto wanaokulia katika mazingira yenye vitabu, wana uwezekano wa kuvipenda kuliko wenzao waliokulia katika mazingira yasiyo rafiki kwa maandishi. Mtoto anapoona vitabu nyumbani tangu akiwa mdogo huamini vitabu ni
sehemu ya maisha yake ya kila siku.
Kwa
kutambua ukweli huo, mzazi anaweza kukusanya vitabu, magazeti, majarida na
machapisho mbalimbali na kuyatunza katika sehemu maalum inayoonekana kirahisi nyumbani.
Sambamba
na hilo, tunaweza pia kupunguza muda wa watoto kutazama televisheni. Ni vigumu
kudhibiti maudhui ya vipindi vya televisheni lakini tunaweza kudhibiti namna
chombo hicho kinavyotumika vyumbani. Kwa hiyo badala ya watoto kukaa muda
mwingi wakitazama yanayoendelea kwenye televisheni, tunaweza kuwa na utaratibu
maalum wa kutazama mambo yanayofahamika katika chombo hiki. Udhibiti wa
televisheni unapokwenda sambamba na upatikanaji wa vitabu vinavyomvutia mtoto,
ni rahisi kujenga mazoea mapya ya kupenda maandishi.
Kuwa
mfano kwa kusoma
Hatuwezi
kumfundisha mtoto tabia ambayo sisi wenyewe hatuna. Kama tunataka mtoto apende
kusoma, tunashauriwa sisi wenyewe tujifunze kupenda kusoma. Ni hivyo kwa
sababu, kwa kawaida, mtoto hujifunza kwa kile anachokiona mzazi akikifanya
kuliko anachokisema. Tunapoonekana tukisoma mara kwa mara, ni rahisi mtoto
kuiga mazoea hayo.
Ni
mara ngapi sisi wazazi tumeonekana nyumbani tukisoma hata kipande cha gazeti?
Mara ngapi watoto wametuona tukisoma biblia, kwa mfano? Sababu rahisi mara
nyingi ni kukosekana kwa muda. Inavyoonekana ni kwamba ingawa wazazi hatuna muda wa kusoma bado tuna matarajio makubwa kwa watoto wetu kuwa ni lazima wasome kwa bidii.
lakini hata kama hatuna kawaida ya kusoma, hatulazimiki kusoma vitabu tusivyovipenda kwa lengo tu la kuigiza utamaduni tusiouzoea.
Kuna magazeti, majarida na vitabu rahisi ambavyo kila mzazi anaweza kuvisoma awapo
nyumbani akitaka. Tabia zote zinajengwa. Tunaweza kuanza na magazeti na baadae
tukaanza kusoma vitabu mbalimbali bila kujisikia adhabu.
Kadhalika, vipo vitabu vya lazima kiimani, ambavyo kwa hakika hatuwezi kuwa waamini imara bila kujenga tabia ya kuvisoma. Ni jambo jema kwa mtoto kuona tukivisoma tuwapo nyumbani. Anapoona
sisi wenyewe tukisoma Biblia, ni rahisi na yeye kuiga.
Kumsomea hadithi
Mtoto hawezi kuthamini tu kile anachokiona bila kuona umaana wake katika maisha yake. Kuona mzazi anasoma kunaleta maana kama mtoto anaweza kuelewa thamani ya kinachosomwa. Ili kuleta maana ya vitabu, ni muhimu kujenga mazoea ya kumsomea mtoto yale anayoyapenda tangu akiwa mdogo.
Baba akiwasomea wanae hadithi. PICHA: verywell.com |
Kwa kawaida, watoto
wadogo wanapenda sana hadithi zenye visa mbalimbali vinavyowakuza uelewa wao.
Kwa hivyo, kuwasomea hadithi zinazowavutia kuliko kuwasimulia husaidia kutambua
thamani ya vitabu kimaudhui.
Kwa mfano, yapo
masimulizi mengi katika vitabu vitakatifu tunayoweza kutafuta vitabu vyake na
kuwasomea watoto wetu. Mazoea ya kuwasomea hadithi, hata kwa dakika chache wakati wanapojiandaa kulala kila siku, mbali na kusaidia kujenga ukaribu na mtoto, yanamfanya mtoto ajenge
shauku ya kujua kusoma mwenyewe ili aweze asome hadithi hizo yeye mwenyewe.
Anapokua na tabia hii, haitakuwa kazi ngumu kuwa msomaji mzuri wa vitabu atakapokuwa
mtu mzima.
Kumpa motisha anapojisomea
Kwa kufanya matatu tuliyoyaona, ni rahisi mtoto kuanza kuiga tabia ya kusoma. Mara anapoanza kuonesha kupenda vitabu, tunahitaji kumpa motisha ili kuiendeleza tabia hiyo. Kwa mfano, anapodai kusomewa hadithi jioni kwa mazoea yaliyoanza kujengeka, motisha ni kutimiza shauku hiyo kwa kumsomea pasipo kutoa visingizio vyovyote.
Ni kweli wakati mwingine
tunarudi nyumbani tukiwa wenye uchovu wa kazi nyingi za siku. Lakini kusomea
mtoto haihitaji dakika kumi. Watoto hasa wadogo hawawezi kuzingatia kitu kwa
muda mrefu. Hatuna sababu ya kutumia visingizio vya uchovu wa mambo mengi kama sababu ya kushindwa kuwasomea watoto.
Kadhalika, badala ya
kuwaletea watoto zawadi za pipi na vitu vingine vya kawaida, tunaweza pia
kuwaletea vitabu vya hadithi wanazozipenda na kuwasomea. Tunapofanya hivyo, tangu
wakiwa wadogo, tunawajengea hamasa ya kuwafanya wathamini vitabu kama
wanavyothamini zawadi nyingine. Mazoea haya yanajenga tabia imara ya mtoto
kupenda kujisomea.
Pamoja na changamoto za
kujenga tabia hii tangu utotoni, bado tunaweza kabisa kuwajenga watoto kuwa
wasomaji wazuri. Kilicho muhimu katika yote ni sisi wazazi kuona umuhimu wa
kujisomea kwa kuwa mfano wa usomaji wa vitabu tuwapo nyumbani.
Unaweza kusoma zaidi makala kama
hizi kwenye safu ya Uwanja wa Wazazi kwenye gazeti la Mtanzania kila Alhamisi.
Maoni
Chapisha Maoni