Kujitambua ni Kushinda Ubinafsi, Kujali Mahitaji ya Wengine?

Tulianza kudodosa suala la kujielewa katika makala yaliyopita. Kama tulivyodokeza, kujielewa kunakwenda sambamba na kuelewa msukumo ulio nyuma ya yale tuyatendayo kila siku. Katika sehemu hii, tutaangalia kwa ufupi kwa nini kujitambua ni zaidi ya ule ‘ubinafsi’ unaoishi ndani yetu.


Kutokusikiliza matakwa ya wengine?

Suala la kujielewa lina mjadala mrefu na wenye kuchanganya. Kila jamii, utamaduni na hata mtu mmoja moja, hulitazama suala hili kwa jicho tofauti. Katika jamii zinazotukuza uhuru wa mtu binafsi, kwa mfano, ‘sisi’ ni yale tuliyonayo ndani yetu yanayotuwezesha kujitegemea na kujiona kama watu walio huru tuliotengwa na ‘utumwa’ wa matarajio na matakwa ya wengine.

Kwa maana hiyo, kujielewa ni kujipatia uwezo wa kuingia ndani mwetu, kujikagua na kuibua yale  tuliyonayo bila kuzingatia sana maoni ya wengine. Kuingia ndani mwetu maana yake ni kuchunguza malengo yetu binafsi –ambayo yanaweza kuwa kinyume kabisa na matarajio ya wengine– ili kuona namna tunavyoweza  kujiletea manufaa binafsi.

Kwa mtazamo huu, watu wengine wanabaki na mchango wa aina mbili kwetu; ni ama kutusaidia au kutuchelewesha kufikia malengo yetu. Wa kundi la kwanza, ni lazima wakubali kuheshimu ubinafsi wetu na hivyo tuwape nafasi ya kuendelea kuwa nao; wa kundi la  pili tunajitenga nao kwa sababu moja kubwa; nao wanahangaika na ubinafsi wao na hivyo hawaoni uthamani wa ubinafsi (u-sisi) tulionao.

Kuweka mbele malengo binafsi?

Tutumie mfano mmoja rahisi. Kijana anapoanza maisha hujikuta akiwa katikati ya majukumu mengi yenye mchanganyiko wa matarajio yake binafsi na ya jamii inayomzunguka. Kijana huyu mwenye mshahara mdogo hujikuta akilazimika kuchagua kipi kati ya kufikia malengo binafsi na kusaidia wategemezi wake kama ndugu, marafiki na jamii inayomzunguka.

Tukitumia maelezo hayo hapo juu, maana yake ni kwamba kama kijana huyu anajielewa, basi analazimika kuchagua kwenda mbele ‘kimaendeleo’ na kamwe asiendekeze matarajio ya wengine yanayoelekezwa kwake. Ndio kusema awe tayari kusitisha ukaribu na marafiki wasio msaidia, apunguze mawasiliano na ndugu zake masikini kule kijijini kwake ambao kimsingi ‘wanambughudhi kuchelewesha utilimifu wa ndoto zake’.  Hatua hizo za 'kujitenga na usumbufu wa jamii' ni za lazima ili kumpa fursa kijana huyo kuelekeza nguvu zake katika kufikia malengo yake mbali na matarajio ya wale wanaomtegemea.

Hiyo, hata hivyo, haina maana kwamba kijana huyu aachane na jamii wala asijilinganishe na wengine katika jamii. Hapana. Kijana huyu anatarajiwa kufuatana kwa karibu sana na makundi ya vijana ‘wenye mtazamao wa kimaendeleo’ wanaoweza kumpa hamasa ya kufikia malengo yake binafsi. Kwa kawaida, malengo ya kijana huyu ni yale ya kujilimbikizia mali na utajiri kuliko kuisaidia jamii masikini inayomzunguka. Kama ni elimu, lazima imsaidie kujimbikizia mali. Vinginevyo, elimu hiyo haina maana. 

Kadhalika, kujilinganisha na wengine ni muhimu. Kwa hiyo kadri anavyoendelea ‘kufanikiwa’ kijana huyu anapaswa kujiongezea imani na mshawasha wa kufikia matakwa yake binafsi kwa kuangalia namna anavyokwenda na kasi ya 'vijana wenzake wa kimaendeo' na namna anavyowazidi vijana 'wasio na mtazamo wa kimaendeleo'. Kimsingi, furaha yake inaongezeka kadri anavyowazidi wengine na kujiongeza kibinafsi. Kilicho muhimu ni malengo yake binafsi.

Vipi matarajio ya wengine?

Mtazamo wa pili wa kujitambua unakinzana kabisa na huo wa kwanza. Kujitambua maana yake ni kuelewa wengine wanatarajia nini kwetu. Katika jamii za kijamaa zinazothamini mshikamano wa kidugu, ni rahisi kuulewa mtazamo huu.

Furaha ya kuwasaidia wengine  Picha: Golf/Getty Images
Kujielewa hakuangaliwi kwa macho ya matakwa yetu binafsi pekee. 

Ndio kusema ‘sisi’ haitenganishiki na matarajio ya jamii inayotuzunguka au makundi tunayojipambanua nayo hata kama wakati mwingine hatukubaliani nayo. 

Kujitambua, kwa maana hiyo, ni kwenda nje ya matakwa yetu binafsi. 



Kujielewa ni kufaidiana na wengine, kutegemeana na wengine na wakati mwingine kujitazama na kujipima kwa kurejea uhusiano wetu na wengine.

Katika mazingira haya, swali kuu linalojibu ‘sisi ni nani’ linakuwa, ‘watu wengine wananionaje?’ Watu wa kundi langu, watu wa chama changu, watu wa kazini kwangu, watu wa imani yangu, familia yangu wanatarajia nini kwangu? Nina kipi cha kuwapa watu wanaonizunguka? Kwa hiyo tunaona hapa kujitambua ni ule utayari wa kwenda mbele ya matamanio, matakwa, malengo binafsi na kujipima kwa kutumia kwa namna tunavyoweza kuchangia ustawi wa wale wanaotuzunguka.

Kukubali kucheleweshwa?

Tukirejea mfano wa kijana tuliyemtaja awali, kijana yule atakuwa anajielewa ikiwa ataweza kujitazama kwa kusaili nafasi aliyonayo katika jamii. Kijana yule atakuwa anajielewa kama ataweza kuamua kufanyika msaada kwa wengine hata ikibidi kwa gharama ya kuchelewesha matakwa na matamanio yake binafsi. Kwamba (kijana yule) awe tayari kufikiria kile anachoweza kufanya ndani ya uwezo wake kuwasaidia ndugu zake masikini kule kijijini na wengine wanaomzunguka.

Kijana yule atakuwa anajitambua ikiwa ataweza kuchelewesha ndoto zake za kufanana na ‘vijana wa mjini’ ili awe jibu la changamoto za watu anaojua wanamhitaji. Hilo linawezekana ikiwa kijana yule atakuwa tayari kuendelea kufungamana na marafiki ‘wasiomsaidia’ kwa sababu tu anaelewa kuwa pengine marafiki hao nao wanamhitaji.

Mkanganyiko usio halisia?

Katika kuhitimisha, pengine ni vizuri tujikumbushe kuwa kujielewa haliwezi kuwa tukio la siku moja. Kujielewa ni safari ndefu kwa sababu, kama tulivyoona, zipo tofauti za kimtazamo zinazoweza kuathiri namna tunavyopima kujielewa kwetu. Pale tunapodhani tunajitambua, wakati mwingine, wengine hutuona kinyume.

Kadhalika, ni ukweli ulio bayana kuwa tunafanya mengi kwa msukumo tusiouelewa vyema. Wakati mwingine hatujui kwa nini tunatenda tuyatendayo. Kwa mfano, twaweza kuwa na tabia fulani tusizozipenda lakini twaendelea kuwa nazo. Je, tunaweza kujielewa na bado tusijue kwa nini tunayafanya yale tuyafanyayo? Je, huo hauwezi kuwa ushahidi wa kwa nini wakati mwingine hatujitambui hata pale tunapofikiri tunajitambua? Labda. Hiyo, hata hivyo, haimaanisha  hatuwezi kujitambua. 

Au ni kushinda 'u-mimi'?

Kwa kuwa tunapenda mahitimisho, nihitimishe kwa maoni binafsi. Swali la ‘sisi ni nani’ ni swali la kujielewa. Kujielewa ni mchanganyiko wa kufahamu sisi (tunaojiuliza swali hilo) tunataka nini, hali kadhalika, wengine wanaotuzunguka nao wanatarajia nini kwetu. Vile vile, kujielewa ni kujua na kuvikubali vile tulivyonavyo na kukubali wajibu wetu kama sehemu (muhimu) ya kujibu mahitaji ya wengine.

Kujielewa ni kuthamini wengine, kuwatanguliza wengine, kuwainua wengine bila kutarajia manufaa kutoka kwao isipokuwa furaha inayotokana na vile tunavyoweza kuwanufaisha wengine hata ikibidi kwa gharama yetu. Kujitambua ni kufahamu iliko furaha yetu. Furaha inayotokana na kuwanufaisha na kuwainua wengine kwa haki. Kujielewa ni kushinda u-mimi. Unakubaliana na mtazamo huu? Inawezekana?

Inaendelea

Makala haya yalichapishwa kwenye gazeti la Mtanzania. Kwa mijadala zaidi fuatilia safu ya Saikolojia katika gazeti la Mtanzania kila Alhamisi.


Barua pepe: bwaya@mwecau.ac.tz

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Mbinu za Kujenga Ujuzi wa Mwanafunzi