Kuanzisha na Kuimarisha Urafiki wa Karibu

Katika zama hizi za maendeleo ya kidijitali, ni rahisi sana kufahamiana na watu wengi ambao, hata hivyo, wanaweza wasiwe marafiki. Unaweza, kwa mfano, kuwa na ‘marafiki’ elfu tano kwenye mitandao ya kijamii, lakini usiwe na rafiki hata mmoja katika maisha halisi.

Marafiki wa kweli na wa karibu ni moja wapo ya mahitaji muhimu katika maisha. Tunaweza kuwa na sababu nyingi kuhalalisha kwa nini hatuna (haja na) marafiki wa karibu.  Hata hivyo, zipo nyakati  hufika tukajikuta katika maisha yenye kujaa upweke  na msongo wa mawazo kwa sababu hatukutumia muda wetu kutengeneza urafiki wa karibu na watu tunaofahamiana nao.


Rafiki ni nani?

Rafiki wa karibu ni mtu mnayehahamiana kwa karibu sana , mnayeminiana na kushirikiana mambo mengi binafsi kwa uwazi bila wasiwasi wa kugeukana. Mara nyingi huyu ni mtu asiye ndugu wa damu wala mwanafamilia, hufanyika sehemu ya maamuzi yetu, furaha yetu na hata katika hali ngumu tunazoweza kukutana nazo katika maisha. Ndio kusema, si kila mtu mnayefahamiana anaweza kuwa rafiki wa karibu. Tunaweza kufahamiana na watu wengi, lakini tukawa na marafiki chache wa karibu.

Marafiki tegemezi

Kwa ujumla, tunaweza kuwagawa  marafiki katika makundi mawili makubwa; marafiki tegemezi na marafiki wainuaji. Marafiki tegemezi ni wale tunaowazidi katika mengi na hivyo wanajifunza zaidi kwetu. Hawa ndio wale marafiki ambao wakati mwingine tunaweza kuwaona kama  wenye hali duni kiuchumi, ndoto zao nyingi hazijafikiwa na pengine wanatutegemea sana ili kufikia ndoto zao za kimaisha.

Katika mazingira ya ‘maendeleo ya kisasa’ yaliyotukuza ubinafsi, ni rahisi kuwaona marafiki hawa kama mizigo tunayohitaji kuitua pale inapowezekana. Tunawaona kama watu wanaovuta mashati kutuchelewesha kufanya mambo yetu. Hata hivyo, kadri tunavyozidi kujitambua, ndivyo tunavyoweza kuwachukulia hawa kama sehemu ya mafanikio yetu.

Marafiki wainuaji

Marafiki wainuaji ni wale wanaotuzidi kiroho, kuchumi, kiufahamu na kiuzoefu na hivyo tuna mengi ya kujifunza kwao kuliko wao wanavyojifunza kwetu. Hawa ndio wale watu maarufu katika jamii zetu kwa sababu ya mafanikio ya kazi wanazofanya.

Katika hali ya kawaida, ni rahisi sana kuvutiwa nao na kutaka kuwa nao karibu kwa sababu tunajua wametuzidi. Tunawatamani kutumia ujuzi wao, maarifa yao, uzoefu wao ili kufika kule tunakotaka kwenda.

Lakini kwa kutumia kanuni ya kuwatendea wengine vile tunavyopenda kutendewa, tunaweza kuona nafasi ya aina zote hizi za marafiki katika kufanya maisha yawe mduara wa kutegemeana. Tunawahitaji marafiki tegemezi ili tuwasaidie kufikia ndoto zao, na hali kadhalika, tunawahitaji marafiki wainuaji ili na sisi tupate mwangaza wa kufikia ndoto zetu.

Kwa hakika, urafiki wa karibu na watu hauwezi kutokea hivi hivi. Urafiki ni kama uwekezaji unaodai gharama kubwa hasa katika hatua za mwanzo kabla ya kufikiria kupata faida. Tuone baadhi ya gharama hizo tunazolazimika kuzilipa ili kujenga ukaribu na marafiki zetu.

Kuwekeza muda

Muda ni gharama ya kwanza kutuweka karibu na watu.  Tunalazimika kutoa muda wetu kuwatafuta na kuwasiliana na watu tunaotaka kujenga nao urafiki wa karibu pasipokusubiri wao watutafute.

Kwa kawaida watu hawavutiwi na marafiki tegemezi wanaotaka watafutwe. Watu wana kawaida ya kujipenda wenyewe zaidi. Tunaposubiri wengine wafanye jitihada za kututafuta, tunaweza kungoja sana kwa sababu na wao wanasubiri tuwatafute. 
Kupatikana ni jitihada moja wapo ya kujenga urafiki wa karibu. PICHA: Tylissa Hide
Kwa hiyo ikiwa tunataka kujenga uhusiano wa karibu na watu tunalazimika kuchukua hatua za makusudi na kufanya bidii ya kupatikana. Kupatikana ni pamoja na kuwa na muda wa kutoka pamoja, kufanya shughuli za kijamii pamoja, kutembeleana na mambo mengine yanayotufanya tuonane ana kwa ana.

Ni rahisi kuwatafuta watu pale tunakuwa na shida. Hata hivyo, kuwatafuta watu tunaowaita ‘marafiki’ wakati tunapowahitaji hujenga picha ya rafiki tegemezi na hivyo kuzorotesha ukaribu wa kirafiki. 

Kuaminika

Watu hawajengi uhusiano wa karibu na mtu wasiyemwamini. Wangependa kuwa na mtu wasiye na  wasiwasi naye. Ili kuaminika, tunalazimika kujenga tabia ya kuwa waaminifu kwa mambo yao. Uaminifu ni pamoja na kutunza ahadi zetu na kutovunja makubaliano na watu tunaowaita marafiki.

Kadhalika, kutunza siri za wengine ni jambo la lazima. Tunapotambulika kwa sifa ya kuongea na watu tunaokuwa nao badala ya kuongelea watu wasiokuwepo, tunajenga kuaminika. Kusema mambo ya watu wasiokuwepo, ni kujipunguzia imani bila kujua. Hii ni kwa sababu watu kwa kawaida hawapendi waseng’enyaji hata kama wanaweza kuvumilia kusikiliza mambo mabaya ya wengine. Wanajua yule anayewaambia mambo yao, huwaambia wengine mambo yao.

Uwezo wa kusikiliza

Binadamu anapenda kusikilizwa. Tukitaka kuishi na watu vizuri tunahitaji kuwapa nafasi ya kuwasikiliza kuliko tunavyotaka watusikilize sisi. Kusikiliza ni kuwa na uwezo wa kufuatilia kwa makini kile wanachojaribu kusema. Ni kujaribu kuelewa mtazamo wa anayezungumza badala ya kufikiria kile tunachodhani kilitakiwa kusemwa.

Kadhalika, kusikiliza ni kutokukatisha na kuingilia ingilia wengine wanapozungumza. Ni rahisi sana, kwa mfano, kumkatisha mtu pale tunapohisi anasema asichotakiwa kukisema ama tunapoamini amepotoka. Lakini tunapoweza kuvaa viatu vyao, tunaweza kabisa kuvumilia maoni yao hata kama wakati mwingine hatubaliani nayo.

Kukubali mapungufu ya wengine

Haiwezekani watu wakawa vile tunavyotaka wawe. Tunatofautiana kimtazamo, kiimani, na kiuelewa. Ni makosa kulazimisha mitazamo yetu, imani zetu na hata uelewa wetu na kuufanya uwe wa watu wote.  Tuna kawaida ya kutokupenda watu wanaojiona sahihi muda wote wenye tabia ya kukosoa wengine zaidi. Ni muhimu kuonesha kukubali mapungufu ya watu kwa upendo.

Hata hivyo, yapo mazingira ambayo twaweza kuwa na tofauti kubwa za kimisimamo na wengine. Mathalani, kuna masuala kama imani, itikadi na misimamo mingine muhimu ya kimaisha.  Tofauti kubwa wakati mwingine zinaweza kuathiri ukaribu wa dhati na wengine. Sababu ni kwamba watu wana tabia ya kuvutiwa na wale wanafanana nao.

Aidha, pamoja na kwamba zipo nyakati tunalazimika kutofautiana na wengine bado tunaweza kabisa kufanya hivyo kwa upendo bila kuwafanya wengine wajisikie kudharauliwa. Kukosoa kupita kiasi, kudhihaki na kukejeli wengine ni tabia zinazoweza kuzorotesha urafiki.

 Kushiriki furaha, huzuni zao

Tunahitaji kufurahi wenzetu wanapokuwa na furaha. Tunahitaji uwezo wa kuhesabu mafanikio ya rafiki zetu kama mafanikio yetu badala ya wivu na husuda pale tunapohisi kuzidiwa. 

Upo ukweli kwamba kadri unavyofurahia mafanikio ya wengine, ndivyo unavyokuwa na furaha. Lakini pia, watu hufurahi wanapoona tunafurahia mafanikio yao kwa dhati pasipo unafiki. Tukitaka kuwa na marafiki wa karibu, tunalazimika kuwa na tabia ya kufurahia mafanikio ya wengine.

Kadhalika, zipo nyakati ngumu katika maisha. Kuna matukio mazito hutokea yanayotufanya tuwahitaji wengine kutusaidia kubeba mizigo yetu. Mfano, kufiwa na watu wa karibu, kupoteza kazi, changamoto za kiuchumi na kijamii na mambo kama hayo.  Tunahitaji kuwa tayari kubeba mizigo ya wenzetu na kuifanya kama yetu. Waswahili walishasema mapema, akufaae wakati wa shida, ndiye rafiki wa kweli. Kuhesabu matatizo ya wengine kama matatizo yetu wenyewe, ni sehemu ya kujitambua.

Jitihada za kujenga urafiki wa karibu na watu zina gharama kubwa kama tulivyoona. Lakini faida zinazoambatana na urafiki wa karibu sana kiasi hicho zinaweza kabisa kuhalalisha gharama hizo za lazima. Wanasema, hakuna kizuri kisicho na gharama. Tunaweza kutoa visingizio vingi leo kuonesha kwa nini haiwezekani kufanya jitihada hizi, lakini ukweli ni kwamba maisha hayawezi kukamiliki bila urafiki wa karibu sana  na baadhi ya watu. Uwezo na jitihada za kujenga urafiki wa karibu na watu ni sehemu ya kujitambua.


Unaweza kufuatilia safu ya Saikolojia kwenye Gazeti la Mtanzania kila Alhamisi kwa mijadala kama hii.

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia

Uislamu ulianza lini?