Watoto Wanaopenda Kucheza Kuliko Kujifunza Katika Umri wa Miezi 0 – 36
Pamoja na kuwa kucheza ni hitaji la msingi katika kujifunza kwa mtoto, michezo ipaozidi wazazi wengi hupata wasiwasi. Michezo huweza kupoteza muda mwingi sana wa mtoto, muda ambao ungeweza kutumika kwa mambo mengine. Kwa kawaida mtoto anayependa sana michezo ni 'mtu wa watu' na kumtenga na watoto wenzake ni kama adhabu.
Katika makala haya tunajaribu kuangalia namna gani mzazi anahusika kutengeneza hali hii ya mtoto kupenda sana kucheza na kuzungukwa na watu kuliko anavyoweza kutamani kujifunza. Tutaona kwa nini tabia hii inatokana na kutokujiamini kwa watoto mwenyewe kiasi cha kujikuta akiwaamini wengine zaidi.
Kutokujiamini
humfanya awaamini wengine
Mtoto ‘mpenda michezo’ ni mtoto tunayeweza kusema ameweka michezo mbele. Muda wote anatamani kucheza na kujichanganya na watoto wenzake. Anaweza kutokuwa na mazingira ya kumwezesha kucheza lakini moyo wake unatamani kucheza muda wote. Kwa muhtasari kucheza ni muhimu sana kwa mtoto huyu kwa sababu ndani mwake mna utupu unaomfanya asitosheke kuwa mwenyewe-mwenyewe kama
wenzake wa kundi la pili. Imani yake iko kwa watu wengine anaodhani wanaweza
kumsaidia kufukia utupu huo.
Kinachomvuta kuwa na wengine si upendo alionao kwao bali ni shauku yake kubwa ya kutaka mno kuwapendeza na kuwaridhisha watu wengine, ambao kimsingi ndio tumaini la furaha yake. Hii ni kinyume kabisa na mtoto wa kundi la pili ambaye furaha yake haiko sana kwa watu bali kwa anachoweza kukifanya hata akiwa peke yake. Kwa lugha nyingine, furaha ya mtoto ‘mpenda michezo’ haianzii ndani, kama wenzake wa kundi la kwanza, bali huanzia nje kwa kuwaridhisha na kuwafurahisha wengine.
Kinachomvuta kuwa na wengine si upendo alionao kwao bali ni shauku yake kubwa ya kutaka mno kuwapendeza na kuwaridhisha watu wengine, ambao kimsingi ndio tumaini la furaha yake. Hii ni kinyume kabisa na mtoto wa kundi la pili ambaye furaha yake haiko sana kwa watu bali kwa anachoweza kukifanya hata akiwa peke yake. Kwa lugha nyingine, furaha ya mtoto ‘mpenda michezo’ haianzii ndani, kama wenzake wa kundi la kwanza, bali huanzia nje kwa kuwaridhisha na kuwafurahisha wengine.
Hali hii inatokana na malezi yaliyojaa upendo lakini kwa bahati mbaya hayatabiriki. Mtoto anakuwa hana hakika ni wakati gani hasa thamani yake kama
mtoto inaweza ‘kuonekana’ kwa mzazi wake. Kutokueleweka kwa ufasaha lini mzazi
huona thamani ya mtoto, hufanya upendo wa mzazi uonekane kama mchezo fulani wa
kubahatisha. Mzazi ‘apatapo’ nafasi baada
ya majukumu yake ya ‘muhimu’, ndipo humpa mtoto ‘dozi’ maalum kwa kumsikiliza, kushirikiana
naye na kadhalika na kumfanya mtoto kujisikia thamani yake halisi.
Bahati mbaya 'dozi' hiyo maalum haidumu kwa sababu muda mwingi mzazi hana habari na mtoto na matokeo yake hujisikia kupuuzwa,
kutokusikilizwa, kutokuelewa na kadhalika. Kwa hiyo katika macho ya mtoto, upendo wa mzazi unaonekana kama vile upo,
lakini haijulikani nini kifanywe ili kuulipia. Matokeo yake mtoto huhangaika kujaribu
kutafuta mbinu ya kumpata mzazi huyu asiyeeleweka ni lini hutoa upendo. Kazi hii ya kutafuta upendo badala ya kuupokea bila masharti hujenga ombwe kwenye moyo wa mtoto. Ombwe hili ndilo hasa hali ya kutokujiamini, na huzibwa na shauku iliyopitiliza ya kutaka kuwa kiini cha mazungumzo na mawazo ya wanaomzunguka kama tutakavyoona hivi punde.
Mbinu
za ‘kuonekana’ kwa mzazi wake
Mtoto wa kundi hili hajifichi. Kwa sababu hana hakika na usalama wake akiwa na mzazi ambaye kwa kiasi fulani anaaminika lakini hapatikani, hupenda sana ‘kumganda’ mzazi/mlezi kupita kiasi. Na anapohisi dalili za kuachwa, hali ya hewa hubadilika. Akiwa na miezi kadhaa tu, hapendi kabisa kuachwa. Ingawa na mtoto wa kundi la kwanza naye atalia kama huyu, tofauti yao ni kwamba itamchukua muda huyu kunyamaza. Kadhalika, mzazi atakaporudi, mtoto wa kundi hili humganda kwa kutaka ‘attention’ hali inayoweza kuhesabiwa kama kudeka na mzazi mwenye 'majukumu mengine muhimu'.
Kwa sababu mtoto ana hakika mzazi wake anampenda ingawa hajajaua afanye nini ili kuupata upendo huo, mtoto hujikuta akijitengenezea vijitabia vya kutafuta ‘attention’ ya mzazi. Kwa hiyo tangu miezi ya mwanzo anakuwa mtoto wa kulia lia bila sababu ya msingi. Mzazi anaweza kushangaa mtoto analia katika mazingira ambayo haonekani kuhitaji chochote. Kadri anavyoanza kuongea, unaweza kushangaa anavyokuwa fundi wa kulalamika, kupiga kelele zisizo na sababu, vituko-vituko. Lengo kubwa n iili tu ‘aonekane’ na apate usikivu wa wanaomzunguka, usikivu ambao haupati bila kufanya hivyo.
Kwa upande mwingine, hali hii
husababishwa na wazazi ambao wapo kimwili, lakini kihisia ni kama vile hawapo.
Ni wale wazazi ambao mpaka umfurahishe lazima uwe umefanya kazi ya ziada,
vinginevyo sarakasi zako zote za kutafuta kuonekana kwake hazitaonekana. Ni
kama hakuoni.
Wakati mwingine ni shauri ya malezi
ambayo hayajibu madai halisi ya mtoto bila kumlazimisha mtoto kufanya kasheshe
ya namna fulani hivi. Kwamba bila hiyo kasheshe kinachofanywa na mzazi ni kile
anachokitaka yeye mzazi na sicho kinachohitajika kwa mtoto. Kwa mfano, mtoto anapoomba
kupewa kitu fulani hakuna anayeonekana kusikia. Sana sana ataambulia kupata
mahubiri ya namna hicho kinachohitajika kisivyofaa. Lakini ajabu, mtoto huyo
akileta kasheshe la uhakika wakati mwingine hata mbele za watu, mzazi
analainika na kufanya kinachoombwa.
Hatimaye mtoto anagundua jambo muhimu.
Kwamba mzazi hujibu kwa haraka pale ‘kituko’ kinapofanyika iwe kwa kulia,
kupiga kelele, kurusha rusha mikono, kulalamika mbele za watu na kadhalika. Mbinu
kuu inakuwa ‘ukitaka baba/mama
akusikilize…leta kasheshe’. Kasheshe linaanza kusaidia kumsogeza mzazi karibu
na mtoto.
Anaanzaje
kujiona hapendwi
Kwa sababu mzazi mwenyewe haeleweki
na wakati mwingine ni vigumu kujua kipi hasa kikifanyika kitaleta matokeo, hufika
wakati hatimaye jaribio la ‘kumsoma’ mzazi huzaa matunda. Mtoto huanza kuonesha
hisia zaidi ya ‘kutumia akili’. Analia, kupata ‘usikivu’ wa mzazi. Anafanya
kituko, walio karibu wanaanza kumsikiliza. Akichekesha, anasikilizwa.
Akiwa kati ya miaka miwili na mitatu
kuna vijitabia huanza kuonekana. Kwa mfano, anaweza asilie-lie akiwa na wazazi
wake kwa sababu anajua hawatajihangaisha na madai yake. Lakini wakiwepo wageni au wawapo kwenye umati
wa watu, hujua hiyo ndiyo fursa ya kusikika. Hapo ndiko anakoweza kufanya ‘makasheshe’
ili wazazi ‘wahangaike’ nae. Kitendo cha wazazi kusumbuka kumnyamazisha kinampa
kuridhika kwamba anaweza kutaka kitu kwa mbinu fulani na kikafanyika. Hata
hivyo, huwepo mazingira ambayo, mtoto hushindwa kumsoma mzazi. Athari yake ni
kuanza kujiona kama mtu asiye na thamani na kupendwa.
Shauri ya kushindwa kabisa kumfanya
mzazi atende apendavyo, mtoto hujiona mtupu akiwa na wazazi na hata akiwa mwenyewe.
Suluhu ya kuibua thamani yake ni kugandana na watu ili kufidia huo utupu huo. Michezo
ndiyo namna nzuri na muafaka kwake kugandana na watu wengine.
Watoto 'wapenda michezo'. Picha: huffingtonpost.com |
Akiwa na umri wa kati ya miaka
miwili na mitatu, mtoto wa kundi hili tayari anataka kucheza sana, lakini
michezo yake ni ile ambayo inamfanya asikike zaidi kama kulia lia, kulalamika,
kusemea semea wenzake na sio michezo yenye ubunifu na udadisi. Kwa lugha
nyingine, huyu anacheza ili aonekane sio kujifunza. Na kwa sababu anatumia muda
mwingi sana kucheza kuliko kingine chochote, anapofikisha miaka mitatu, ni kazi
ngumu sana kumtenga na michezo hasa ile inayomfanya aonekane na wengine.
Kwa ujumla, hawa ni watoto ambao
watu kwao ni muhimu kuliko shughuli nyingine yoyote na wanaongozwa na hisia
(kulia, kulalamika, kutafuta huruma na
sifa) kuliko wanavyoshughulisha akili. Na shauri ya kuamini zaidi hisia na
kuwekeza kwa ‘watu’ hujikuta wakikosa muda wa kujifunza mambo mengi ya msingi
ambayo wenzao wa kundi la kwanza na la pili wanajifunza. Matokeo yake hawawi na
uwezo mzuri sana wa ‘kujua’, uwezo ambao jamii na wazazi wengi wanaouhitaji.
Hali hii huwaondolea ujasiri unaotoka ndani, na kuwafanya waendelee kujisogeza
zaidi kwa watu kwa njia zitakazowafanya wasikike kama ugomvi wa hapa na pale,
ucheshi wa kudhalilisha, na kadhalika.
Katika makala inayofuata tunazama
kundi la mwisho la watoto wagomvi na wajeuri.
Inaendelea
nice articel.. its can make me know about all.. thanks.. .. regards
JibuFutamebel jepara murah
can hopefully share...
Maoni haya yameondolewa na mwandishi.
JibuFuta