Mnalipwa kwa kushabikia upuuzi?

TULIWAHI kujadili wakati fulani tafsiri hasa ya msomi na usomi. Mimi bado ninaamini nchi yetu ina uhaba mkubwa wa watu wenye hadhi hiyo nyeti. Wengi wetu ni wasomaji kwa maana ya kuwa na uwezo kujua vitabu vimeandikwa nini na kwa kweli ninaamini ‘wasomi’ tulioanao hawatusaidii.

Tunafahamu kabisa kwamba uchakachuaji/kughushi ni sehemu muhimu ya mfumo wa elimu yetu. Ndivyo tulivyojengwa. Ndio maana hata sikushangazwa na tafiti za hivi karibuni zilizokuwa na nia ya kubashiri nani na/au chama gani kinakubalika zaidi. Wewe fikiria kama, na si mara moja, mwanafunzi anaweza kabisa kuandaa ripoti ya kisayansi mezani (bila hata kutafuta data maabara) na ikatua mikononi mwa mwalimu wake naye aipitishe; ni nini cha ajabu kwenye tafiti hizi?

Umekuwepo mjadala wa kuhoji uhalali wa kuwatumia sampuli ya watu 2000 ili kujua maoni ya watu milioni arobaini. Watu wanadai how comes? Pengine ni vyema kukumbushana kuwa ni kweli inawezekana kabisa maoni ya watu elfu mbili yakajirudia rudia ama kujenga pattern fulani ambayo inaweza kutusaidia kujua hata wale wengine waliobaki watatuambia nini kama tungekuw ana nafais ya kuwauliza. Hiyo ni ikiwa tu watu hao elfu mbili walipatikana kwa mujibu wa kanuni halali za kisayansi.

Pamoja na ukweli huo, bado hiyo haiondoi hulka ya waswahili tuliojaliwa kutumia nadharia katika kuandaa taarifa mezani pasipo kulazimika kwenda kwenye eneo husika la utafiti. Huo ni mfano mmoja wa kututhibitishia kuwa elimu yetu ni haramu.
Hebu tutazame na mfano mwingine. Waandishi wa vyombo vya habari vya hapa nchini.
Sasa hivi kabla hata kujasoma gazeti, tayari unakuwa unajua nini utakutana nacho ndani kulingana na jina la gazeti husika. Magazeti hayana kazi nyingine isipokuwa ushabiki tu wa kisiasa. Yameibuka magazeti ambayo kwa kweli unahitaji tu kuwa na uwezo wa kusoma na kuandika kubaini wazi kwamba yanachokifanya hata yenyewe yanajicheka. Ni kama yaongozwa na job discription ya “shabikia bosi na marafiki zake, haribu mpinzani wa bosi kwa gharama yoyote ile!”

Sasa mtu unajiuliza, kama suala ni kupigia debe fulani, kwa nini usitwange debe kwa staha na hoja zinazoeleweka!? Kupiga debe ni mpaka uzue mambo?

Ni magazeti haya haya tena yanayoongozwa na wahariri wenye vyeti vyenye majina makubwa, yanayotumia sehemu kubwa ya kurasa zao kupamba vinavyonuka, vikata kuuone uvundo kuwa ni harufu nzuri ya kupendeza. Hofu kubwa inakuja pale unapokuta hata magazeti ya umma (yanayoendeshwa kwa kodi za wananchi) nayo yameingia kwenye mkumbo huu. Kwa kweli tunahitaji kujua “usomi katika vyumba vya habari unamaanisha nini?”

Kwa nini wasomi wanatumika kwa matakwa ya wafanya biasiasa? Au ndo tukubaliane kwamba elimu hutuandaa kuwa watumwa?

Ndio maana haishangazi kwamba magazeti haya yamedharaulika na hayauziki zaidi ya mtaa wa Sinza Kijiweni. Yamebaki kuendeshwa kibishi kwa sababu tu wenye maslahi yao wanajua kabisa kuwa wanayahitaji ama kwa kujibia kashfa zao za kila siku au kuendeshea propaganda chafu dhidi ya wapinzani wao!

Si magazeti tu, bali hata televisheni. Vipo vituo vya televisheni vinavyosikitisha sana na kwa kweli vinawaaibisha waandishi waadilifu. Unapokuwa na kituo cha televisheni ambacho shughuli kubwa ni kutoa muda mwingi katika kutangaza propaganda za watu wanaowashabikia, hata kama ni kweli wanatoa fedha, ujue tumejongea karibu kabisa na kifo cha maadili!

Mfano. Juzi zilitokea vurugu Maswa. Sote tulistuka kusikia watanzania wenzetu wameanza kutoana ngeu na hata kumwaga damu. Kilichosikitisha na kuogofya zaidi ni namna tukio hilo lilivyoripotiwa na vyombo vya habari. Kituo kimoja cha televisheni (cha huko mikoani) kinachoongoza kwa kurusha vipindi vya kumtangaza mgombea mmoja, bila hata haya kikatangaza “…wanachama wa CHADEMA wameua mwanachama wa CCM huko Maswa …(na kwamba) Katibu Mkuu wa CCM (akiwa huko huko Maswa) amesihi wanaCCM kutokulipiza kisasi…”

Habari hiyo haikueleza ukweli wote wa nini hasa kilitokea. Nani alikuwa wapi, na nani akaanzisha vurugu, hatimaye nini kikatokea. Hawa jamaa wakaachana na hayo yote kwa makusudi (ikiwa ni pamoja na mgombea wa ubunge wa CCM kumkata mtama OCD kwa sababu tu kamwachia huru mpinzani wake)na kukimbilia kutangaza kinachoonekana kuendana na job description yao!

Nadhani inaeleweka kabisa kwamba tunaendekeza ubabishaji kwenye mambo yetu mengi. Lakini hawa waandishi wa habari waliolewa ushabiki wakiendelea na vitendo hivi visivyokubalika, tusishangae vurugu zikilipuka (na usishangae hawa hawa ndio wakawa wa kwanza kurusha lawama). Mlipuko wa vurugu hizi utatokana na upuuzi huu wa waandishi wa habari kushabikia matendo vya hovyo ya baadhi ya wanasiasa majambazi kwa sababu tu wanalipwa kufanya hivyo! Na ni ajabu eti serikali haionekani kuona! Au ni kweli kwamba inapendezwa na upuuzi huu?

Shukrani kwa vyombo vya habari ambavyo kwa kweli havijakubali kulamba makenye ya watawala. Hawa wameamua kujali jukumu lao halisi la kuwahabarisha wananchi ukweli bila kujali wanakosa shilingi ngapi kujigeuza kuwa mashabiki wa upuuzi.
Na ka kweli ingetegemewa kwamba serikali ivisifu vyombo vya habari vinavyofanya kazi zao kwa weledi na uadilifu.

Katika vyombo hivyo, mimi niyapongeze magazeti ya kampuni ya mwananchi (The Citizen na Mwananchi) ambayo kuna tivii moja imegoma kabisa kuyasoma asubuhi kwenye kipindi chake cha Kumekucha. Niwapongeze pia Raia Mwema kwa kuonyesha wazi kuwa hawakubaliani na uenda wazimu tunaoushuhudia hivi sasa.

Maoni

  1. Ni ukweli unachokisema, watu wamekuwa na ushabiki usiofanana hata na hadhi na elimu zao yaani ni ilimradi liende utamkuta mtu msomi tu(japo wasomi wetu ndo walee wa vitabu darasani) anashabikia kitu ambacho daaah ni aibu tupu. lakini tufanye nini?

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia

Uislamu ulianza lini?