Upweke wa kutokublogu

BAADA ya kimya cha muda mrefu kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu, namshukuru Mungu wa Israeli nimerejea tena. Sijaja na kipya. Ila nimekuja kusoma mengi ya mtandaoni. Ukweli ni kwamba mtandao ni moja ya burudani zangu muhimu sana kama ilivyo mpira kwa wenzangu fulani. Kwa wenzangu na mimi tusiopenda kujua hata matokeo ya mechi za Uefa, wapi zaidi ya kwenye blogu?

Nilikosa kusoma posti na maoni ya wanablogu. Nimekuwa kwenye kipindi cha upweke fulani hivi nisioweza kuueleza.

Kila siku nijakosa kujiuliza: hivi Baba Mtakatifu Simon kasemaje leo? Da! Watu kama akina Mubelwa, Subira, John Mwaipopo, Yasinta, Maprofesa Mbele (bora hata ninakisoma kitabu chake kwa kukirudia na kukirudia) Matondo, akina Evarist, Kamala, Mbilinyi, Dada Vukani, Kisima, Lundu Nyasa (msee jibu lako nakuja nalo), akina Shabani Kaluse (pole na shule), wazee wa Strictly gospel (hee yale majadiliano nitayarudia mapema sana), na wengine wengi ambao nimebaki nao kichwani mwangu.

Nilikosa kusoma mawazo motomoto kwenye blogu zetu ambayo kimsingi hunifanya nitafakari, nicheke, na hata mara nyingine kuhuzunika.

Nimerudi tena kuwasoma watu wangu. Na karibuni tujadiliane.

Maoni

 1. Maoni haya yameondolewa na mwandishi.

  JibuFuta
 2. Karibu tena ulingoni. Siamini kwamba huko ulikokuwa kulitawaliwa na ukale tu. Au uliufumbia macho upya usionekane? Ni lazima tu utakuwa umekuja na jipya. Tunalisubiri!

  JibuFuta
 3. Hata kutokuja na jipya wakati twasubiria jipya ni upya wa mawazo kwa sisi tulioamini kuwa ukitoka lazima uje na jipya.
  Kwa hiyo asante kwa "jipya" hilo.
  Na sasa tunasubiri hayo ya kale yaliyoboreshwa kwa fikra za sasa ili kujua namna ya kusonga.
  Karibu saaana Kaka.
  Karibu tusonge

  JibuFuta
 4. karibu tena. bila shaka utazidi kutupa mengi ili tuweze kujielewa vema.

  JibuFuta
 5. Asanteni nyote. Tuko pamoja!

  JibuFuta
 6. Ndugu Bwaya, karibu tena. Nategemea umerejea ukiwa unajisikia vizuri na utulivu wa mawazo.

  Nakusikia unavyosema unasoma kitabu changu namna hiyo, nami namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kukiandika kama nilivyokiandika.

  Nanakuja Tanzania kuendesha warsha kadhaa mwaka huu, mojawapo ikiwa Arusha, tarehe 3 Julai, na masuala yaliyomo kitabuni yatazungumziwa katika warsha.

  JibuFuta
 7. Profesa Mbele, kitabu chako kimenifunza masuala mengi ya msingi. Na kadri ninavyoendelea kukisoma najifunza mengi zaidi.

  Najivunia kukipata kitabu hicho.

  Japo sijajua hadhira yako katika warsha hizo, lakini natumai kuwa utakuwa ni mfululizo wa warsha moto moto.

  JibuFuta
 8. Ndugu Bwaya

  Shukrani tena kwa ujumbe wako. Dunia ni kuelimishana, nami hupenda sana kuwa na watu wa aina yako, ambao ni watafutaji elimu.

  Wamarekani wanakitumia sana kitabu hiki wanapojiandaa kuja kwetu kwa shughuli mbali mbali. Wanajua kuwa kufahamu tabia, fikra, taratibu, na mienendo ya mataifa au jamii tofauti na zetu ni muhimu kwa mafanikio tunaposhughulika nao.

  Watanzania bado tuko usingizini. Tunadhani tunaweza kukurupuka tu na kwenda nchi ya mbali kufanya biashara, au shughuli nyingine yoyote bila kujielimisha kuhusu tofauti za tamaduni kama ninavyoelezea katika maandishi yangu. Nina hakika kuwa hatutaweza kushindana na hao wenzetu.

  Huu ndio msingi wa warsha zangu, ambazo naziendesha huku Marekani, na tangu mwaka juzi niziendesha pia huko Tanzania.

  Yeyote anakaribishwa kuhudhuria. Warsha zilizopita wamehudhuria wa-Tanzania walioko katika sekta ya utalii, ofisi za mashirika serikali, vyuo, sekta binafsi, na kadhalika. Huwa naziendesha kwa ki-Ingereza, kwani wanakuwepo watu wa mataifa mbali mbali.

  Kwa bahati nzuri, wa-Tanzania kadhaa wanaanza kutambua faida za hayo ninayoongelea. Kwa mfano, madereva wa kampuni ya utalii ya J.M Tours, iliyoko Arusha, ambayo inamilikiwa na mama mmoja mzungu, wanakienzi kitabu hiki, kwa vile kimewapa mwanga kuhusu tabia na mambo ya wateja wao, hasa wa-Marekani. Kila ninapokutana na madereva hao, wananichangamsha kwa jinsi wanavyoelezea yaliyomo katika kitabu hiki na jinsi wanavyoyatumia kazini. Vile vile, pale Mto wa Mbu kuna vijana wanaoshughulika na mradi wa utalii ambao nao wamegundua manufaa ya kitabu hiki katika shughuli zao. Kwa taarifa zaidi bofya hapa.

  Kwa kuhitimisha, narudia kusema kuwa jambo la msingi ni kuendelea kutafuta elimu. Kwa kusomasoma blogu yako, naona kabisa kuwa wewe uko mstari wa mbele katika suala hilo.

  JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mbinu za Kumfundisha Mtoto Kusoma Akiwa Nyumbani

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Fumbo mfumbie mwerevu

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)