Soma maoni marefu ya Silas Jeremia

Msomaji aliyejitambulisha kama Silas Jeremia amenitumia waraka mrefu kupitia barua pepe leo. Aliniandikia SMS akiniarifu kuwa ameshindwa kuweka maoni yake kwenye blogu (Nadhani ni kwa sababu mchango wenyewe ulikuwa mrefu kuzidi kiasi cha meneno yanayoruhusiwa kuwa maoni kwenye blogger.) Nami nikamwelekeza kutumia barua pepe ambayo ni njia rahisi kwake. Kwa kuheshimu mchango wake, kama wasomaji wengine, nimeona ni vyema niu –paste mchango wake hapa kusudi upate hadhira inayohusika kwa majadiliano zaidi:


"
Naomba kutoa maoni yangu kujibu hoja za upotoshaji zilizoletwa na msomaji wako. Kwanza kama yeye alivyojitambulisha kwa hoja zake kuwa ni Mwislamu, mimi ni Mkristo. Nitajibu hoja zake moja baada ya nyingine ili aelewe kama atakuwa tayari.

1. Walioendesha biashara ya utumwa walikuwa Waarabu wa kiislamu. Hawa walikuja Afrika mashariki kufanya biashara mbaya kabisa ya utumwa na kueneza dini yao. Watumwa walisombwa kutoka Afrika kwenda Uarabuni mahali panaposadikika kuwa chanzo cha Uislamu. Ushahidi: Mahali ambako biashara hii ilifanyika, ndiko Uislamu ukikojikita mpaka leo. Angalia Zanzibar, maeneo ya pwani ya Afrika Mashariki nk. Dini ya Kislamu inaonekana kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na Biashara hii mbaya ya utumwa.

2. Hoja yake ya kukanusha kwamba dini zilileta utumwa ni dhaifu. Utumwa ni dhana pana inayoenda mbali zaidi ya utumwa wa kuuzana na kupigana bei. Utumwa unaohusishwa na dini ni ule wa akili kama hizi za kutetea dini za walioendesha biashara ya utumwa.

3. Hoja kwamba mtume mohamadi eti ndiye msaidizi alisemwa na Yesu haiwezi kuwa zaidi ya kichekesho. Yesu kwanza alieleweka. Alikaa miaka mitatu, akitengeneza wafuasi ambao yeye aliwaita mitume. Aliwafundisha na kuwaonyesha nini walipaswa kufanya. Tatizo lilikuwa utendaji wa yale aliyowafundisha. Alijua hawataweza kuyafanya. Ndio maana wakati anaondoka, akawaambia wale wanafunzi, nitawaletea msaidizi, ndiye Roho Mtakatifu atakayewasaidia kuyashika niliyowafundisha (ambayo alifahamu wazi hawataweza kuyashika pasipo msaada wa zaidi). Roho Mtakatifu yupo hivi leo. Kila Mkristo anayo haki ya kuwa naye na akasaidiwa kumpendeza Mungu. Hata hivyo wapo wakristo wengi ambao hawana Roho Huyu kuwasaidia kumpendeza Mungu. Hawa wanabaki kuwa mashabiki wa dini wenye kufanya dhambi kama kawaida japo wanaweza kuenda kanisani. Hiyo ndiyo maana yake!Yesu akatika mafundisho yake alisema yeye ndiye Alfa na Omega. Yaani ndiye mwanzo na mwisho, hakuna kabla yake, na hata baada yake hayupo.

4. Kusema eti Mohamedi amekuja kuueleza hasa ujumbe wa Yesu ni udanganyifu usio na mantiki. Kama nilivyosema, Yesu alikuwa na mafundisho yake ya msingi ambayo Mohamedi hana habari nayo. Mfano alisema mwenyewe kuwa yeye ni mwana wa Mungu aliyetumwa kuwakomboa wanadamu na dhambi. Ukombozi huu kutoka kwenye nguvu za giza, hauji kwa kushika orodha ndefu ya sheria za wayahudi. Ukombozi huu ungefanyika kwa namna ya Roho. Ndio maana alikufa msalabani kwa ajili ya dhambi za wanadamu. Hili si sehemu ya Uislamu wa Mohamadi. Hivyo kusema mohamadi alikuja kuueleza ujumbe wa Yesu ni mbinu tu za kutaka kuonekana ni dini kongwe kuliko zingine wakati inaeleweka kwamba ilianza karne ya 6 ikiwa na mafundisho tofauti na yale ya Yesu.

5. Hoja ya Ukristo na Kristo iko hivi: Yesu mwenyewe alilisema hili vizuri kuwa yeye ndiye alikuwa yule Masihi aliyekuwa akisubiriwa na Wayahudi kwa sababu alikuwa ametabiriwa katika Agano la Kale (kitabu kilichokuwa kikiaminiwa na Wayahudi). Wao wakamkataa na kumwua kwa hila ili tu mafundisho ya dini yao yaliyokuwa yakisisitiza sheria ambazo hazikuwa na uhusiano wowote na roho zao. Wakaamua kubaki na dini ya Mababu zao (Ibrahimu, Isaka na Yakobo). Na mpaka leo wayahudi wanamsubiri Masihi wao. Wafuasi wa mafundisho ya Yesu ndio hasa waliitwa Wakristo. Kwa maana nyingine, huwezi kuwa Mkristo kama HUFUATI alichofundisha Bwana Yesu. Kutumia ujanja wa maneno kuhalalisha uhusiano wa Uislamu na Ukristo ni fallacy. Hapa naweza kukubaliana na wanaosema kuwa Uyuda ulikuwepo kabla ya Ukristo. Lakini leo wapo hata kama ni wachache, waliokubali kumpokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa Maisha yao. Ninao marafiki wa Kiyahudi walio wakristo. Lakini nakubali kwamba wengi waliamua kushikilia mila na tamaduni zao wakaachana na mafundisho mapya ya Bwana Yesu. Huu ni ushahidi kwamba Ukristo si utamaduni wa mahali Fulani kwa sababu ulihitilafiana hata na utamaduni wa kule uliokanzia.

6. Kingine, huyu bwana anasema eti Roma ndiyo makao makuu ya Ukristo! Hili haliwezi kusemwa na mtu mwenye ufahamu wa dhati wa anachokisema labda kama anabangaiza hoja za kueteta upande wake. Ndugu zangu Roma kama kweli ni makao makuu basi ni ya Ukatoliki na sio ukristo. Ukristo hauna makao makuu. Historia ya hawa Wakatoliki ni ndefu na sina muda wa kuieleza hapa ila itoshe kusema kwamba Warumi katika kipindi fulani waliitumia imani ya kikristo kwa maslahi yao ya Kisiasa. Mapapa wao kuna kipindi walikuwa watesaji wakubwa wa wafuasi wa kweli wa Ukristo. Sitakuwa nimekosea nikisema kuwa Ukatoliki na Ukristo ni vitu tofauti japo vinaonekana kuwa na uhusiano wa aina fulani. Unapozungumzia Ukatoliki usidhani moja kwa moja unazungumzia Ukristo. Ukatoliki ni mchanganyiko wa mambo mengi (siasa, utamaduni, dini nk)

7. Kutafuta maneno halisi aliyoyatamka Yesu si lazima ingawa ni vizuri. Mimi kama mwanafunzi wa Biblia ninaweza kujifunza lugha za awali ambazo zilitumika kuandikia Biblia. Lakini kwa sababu silazimiki kukariri maneno yake, bali kuelewa na kuishi kama alivyosema, sifungwi na mahangaiko hayo! Kutafuta lugha hizo hakusaidii kumwelewa Yesu kama anavyoshauri huyu ndugu. Biblia imetafsiriwa katika lugha mbalimbali ili kueneza ujumbe wa Yesu kwa watu wa mataifa mbalimbali bila kuwalazimu kuwa watumwa wa utamaduni wa watu (lugha). Ndio maana leo hii Ukristo umeenea katika sehemu mbalimbali duniani. Hili ni tofauti na Uislamu ambao unalazimisha waumini wao kukariri maneno kwa lugha ya Kiarabu ambacho masikini hawawezi kukizungumza wakiwa nje ya misikiti. Sishangai kwa sababu Uislamu unasisitiza kukariri maneno kwa orodha ndefu ya sheria za kutekeleza, suala ambalo halisaidii roho zao.

Unapodai eti kutafuta maneno kwa lugha ya asili ndiyo suluhisho, sasa wewe una hakika gani kuwa aliyeandika Kurani kwa kiarabu enzi hizo aliandika kwa usahihi unaotatikana? Au unadhani Kurani iliporomoka tu kutoka hewani ikiwa imeandikwa na asiyejulikana?
Nimalizie kwa hoja ambayo inatembea kudai kuwa Adam na Hawa walikuwa Waislamu. Dini zote za mashariki ya kati zinaanzia kwa Adam na Hawa. Na kihistoria, masimulizi haya basi, yalikuwa ya Wayahudi ambao waliamini kuwa Ukoo wao, umetokana na Adamu na Hawa. Mlolongo kutokea hapo, umeenda mpaka kwa Ibrahimu ambaye Biblia inamtaja kama baba wa imani. Biblia sehemu ya Agano la Kale inaonyesha historia ya kabila au niseme nchi ambayo Mungu aliitumia kutufikisha kwa Bwana Yesu. Wayahudi wanamwani Ibrahimu kama Nabii wa dini yao na babu yao kwa damu kupitia kwa Isaka mwanae wa pekee. (Kuna hata wakristo wenye ufahamu finyu wanaodai eti Ibrahimu ni baba yao wa kiimani wakati wao hawana uhusiano wowote wa kidamu na Ibrahimu.)

Biblia inaeleza wazi kwamba Ibrahimu alichelewa kuzaa akamwingilia mfanyakazi wake wa ndani (Hajir) na kumzaa mwana wa haramu Ishmael ambaye ndiye chanzo cha Waarabu. Hapo ndiko historia ya waarabu inakounganikia na kuachana na historia ya Waisrael. Wasomaji muelewe kwamba hapa tunazungumzia historia ya Waarabu na Waisrael (Wayahudi) na sio Uislamu na Ukristo. Sasa waarabu kupitia Ishmael na mama yake Hajir ndio waliokuja kumzaa Mohamedi maelfu ya miaka baadae na akaanza harakati za kutangaza dini yake ambayo haikuwepo kabla yake. Maelezo yanayotumika kulazimishia Uislamu kuanzia kwa Adam na Hawa ni ya kuunga unga na kucheza na maneno kuliko ukweli wa mambo.

Ukweli ni kwamba kitabu cha Kurani na Biblia vinaonekana kuwa na maelezo yanayofanana hasa ya kihistoria kwa sababu kihistoria Waarabu na Wayahudi ni ndugu hata kama hawapatani kwa sasa. Na bahati mbaya dini ya Kiislamu inaitumia historia hiyo kujaribu kubinafsisha haki ya kuanzia mwanzo wa dunia. Ni bahati mbaya kwamba hawa hawa Waarabu na Wayahudi ndio chanzo cha imani kuu duniani.

Mwisho Allah, jina la mungu wa Waarabu hana uhusiano na mungu wa Waisrael. Kumbuka kwamba dunia hii ina miungu mingi sana. Hata sisi waafrika tulikuwa na miungu yetu. Ni makosa kudhani eti haya ni majina tofauti ya Mungu mmoja. Hapana. Ikibidi nitalieleza hili kwa kirefu wakati mwingine. Kama hivyo ndivyo basi, huwezi kudai eti Allah ndiye alikuwa anawaagiza Adam na Hawa wakati ule wa mwanzo, na ukajiaminisha kwmaba unachosema ndio kweli kwa kutumia maneno eti unyenyekevu. Niishie hapa kwa leo.

Ndugu Silas asante sana kwa kutumia muda wako kushiriki mjadala huu.

Maoni

  1. Awali, nakushukuru kaka Bwaya kwa kuuthamini mchango wa kaka Silas.
    Pili, nikushukuru kaka Silas kwa kuutumia muda wako kuchungua na kuwasilisha mezani majibu ya hoja hizo.
    Nami nimepata changamoto ya kutosha na ufahamu juu ya mambo kadhaa. Nami ngoja niendelea kutazama historia hii kwa marefu na mapana.
    Wikendi njema kwenu nyote.

    JibuFuta
  2. Asante sana kaka Fadhy, bila shaka nawe kama Silas utakuja na mchango ulioshiba. Nakutakia mwisho mwema wa Juma.

    JibuFuta
  3. Hapa kila mmoja anakuwa na uwezo wa kutoa maoni yake kulingana na imani yake inavyomtuma.


    Wanaozitetea imani hizi walizirithi tu,na wanaweka hoja zao kwa ku refer vitabu zikiwemo Biblia na Kurani.
    Utetezi wa aina hii binafsi siukubali kabisa kwani imani za watu zatawala zaidi bila kuangalia uhalisia na mwenendo mzima kuhusu dini.Hapa ufahamu au akili haimuongozi mtu bali ni kwa kadiri ya imani. Kwa maana hii pande mbili hizi zinazovutana hazitafikia muafaka.


    Hakuna hata mmoja anayeweza kuelezea mapungufu yoyote kuhusiana na dini na imani yake.Hili ndilo tatizo kubwa kabisa.Jamani tutafakari kuhusu imani zetu na tutumie ufahamu na akili zetu bila kujali historia na wigo wa kiimani tuliokwisha kujiwekea(wigo wa kutokuhoji kuhusu imani za kidini).

    JibuFuta
  4. Ndugu bwaya napenda kukushukuru kwa kuwa na hii blog ya watu kutoa maoni yao na hususan kwa katika maoni yanayohusu imani za watu, kuweza kujadiliana, lakini naona kuna upendeleo fulani ya kwamba ndugu Silas amejibu hoja bila ya watu kuelewa maswali yalioulizwa, kwa namna hii nadhani wanablog yako watakosa faida ya maana nzima ya blog. Silas umedai hoja zilizotolewa ni za upotoshaji sijaona hoja zako ndizo zilizo sahihi. Ningependa kujua wale wamarekani weusi kule Amerika walipelekwa na waarabu? Ikiwa utumwa unaohusishwa na dini ni ule wa akili wa kutetea walioleta biashara ya utumwa mbona wewe uautetea hiyo dini ya kilokole ambayo zilizoanzishwa huko marekani na ndiyo hao waliowafanya ndugu zetu wa kiafrika wasijue asili zao?
    Ikiwa huyo msaidizi ni roho mtakatifu, mbona alikuwapo huyo roho mtakatifu hata kabla ya Yesu kuzaliwa. Mafundisho ya Yesu hajakuja kwa kumuokoa mtu kiroho, kwa imani tu uamini eti uwe na imani ya kuwa Yesu kafa mslabani ili kuokoa dhambi za watu ndiyo uwe umeokoka, Yesu aliwafundisha wanafunzi wake njia ya kuokoka kwa kuwaambia wafuate amri 10 za Mungu, na akwafundisha kutawadha na akawafundisha kusali, sijaona wakristo wakifanya hayo. Sasa nyinyi mnapowaambia watu wamuamini Yesu kuwa kafa kwa ajili zao wameokoka na yale mafundisho mumemwachia nani? Ikiwa hoja ya Ukristo na Kristo kuwa Yesu ndiye Masihi aliyetabiriwa katika agano la kale? Je huko huyo masihi alitabiriwa kama Mungu au nabii? Mbona unataka kuwachanganya watu?Na unasema mayahudi hawakumkubali na kumuua, ikiwa wewe ni mtoto wa Mungu Muweza au ndiye Mungu Mkuu utakubali utezwe nguvu na maadui, ikiwa ni hivyo basi Mungu wenu hafai kufuatwa maana yake ikiwa Mungu kauliwa basi sembuse wafuasi?
    Ndugu Silas hao marafiki zako wa kiyahudi hawawezi kuwa wakristo labda uniambiye ni waisraeli wakristo.
    Leo unawakanusha Wakatoliki si wakristo, ahsante naomba unifahamishe wakristo sahihi ni wakina nani?
    Kuhusu lugha ya Yesu aliyo zungumza itakuwa muhimu watu waifahamu kwasababu ndiyo lugha aliyo zungumza Mungu kuleta ujumbe usitake kuitoa umuhimu, kwani kuna mambo yamezushwa na kanisa ambayo hayapo kwenye biblia, kama utatu mtakatifu, millenium haipo kwenye biblia nja kuna mambo mengi ambayo ni mafundisho ya kanisa ambayo wala kwenye biblia hayamo, ndiyo maana tukaomba tupate biblia iliyoandikwa kwa lugha aliyozungumza Mungu itusaidiye, sidhani kwamba Yesu alilitamko neno KRISTO? Naomba ndugu Silas unifahamishe ni nini maana ya neno Kristo kwa lugha kiswahili.
    Kuran injieleza yenyewe haina shaka ndani yake na hakuna muislamu mwenye shaka nayo labda nyie wenzetu ndiyo wenye shaka nayo na kama unadhani una shaka nayo nenda kwa wenye elimu ya Kuran ukawaeleze shaka yako.
    Unaisoma biblia lakini huitaki kuifahamu, kwa kuwa kuna chuki na uislamu kwa baadhi ya wenzetu wakristo, naomba unionyeshe andiko ambalo linasema Ibrahim alizini na Hajer na kumzaa Ismail, mnafikia hata kumtia dhambi mtume mkuu ni baba wa imani Ibrahim ili mpenyeze chuki yenu dhidi ya waarabu, mbona hamuzungumzii kwamba Ibrahim alimuoa Sara ni akijua ni dada yake wa baba mmoja kama biblia inavyosema? Kama unavyodai kuwa Allah ni Mungu wa waarabu na hana uhusiano na waisraeli, hiyo ni hoja yako binafsi ebu chukua biblia ya kiarabu na uisome Humo Mungu katajwa kwa jina gani? Kwa imani ya kiislamu Mungu ni mmoja na ana majina 99 miongoni mwa hayo ni Allah, naomba tuwaulize waisraeli hata kama wanablog humu je wao Mungu wao anitwa nani? Naomba usitoe hoja isiyokuwa na uasili wowote alimradi uwachekeshe watu, nyinyi walokole ndiyo wa kwanza kusema Allah ni Mungu wa waarabu. Na kama utakuwa una hoja ya kuonyesha tofauti ya miungu ilete, kwani nyinyi ndiyo mliozoea kuwafanya watu kuwa miungu. Leo Watu wanakuja kutuambia wao ni mitume na wana roho mtakatifu lakini matendo yao yanasikitisha sijui ukweli huu unathibitishwa vipi? Lakini haya yote ni majadilano, naomba samahani kama nitakuwa nimeziumiza hisia za watu haya ni mambo ambayo ndugu Silas aliya tolea hoja na kusema ni upotoshaji, ahsanteni.

    JibuFuta
  5. Nikushukuru ndugu uliyejibu hoja za Bw. Silas. Bila shaka maswali uliyoyaibua, yatatendewa haki na wasomaji akiwemo Silas. Nisamehewe kwa kasoro zozote zanazojitokeza na kuwaletea usumbufu wasomaji wangu.

    Wakati napitia mjadala, nilihisi alikuwa akijibu hoja za wasomaji wasiotaja majina yao. Pengine wakati mwingine atabainisha hoja kabla hajazijibu.

    asanteni

    JibuFuta
  6. Nikushukuru ndugu uliyejibu hoja za Bw. Silas. Bila shaka maswali uliyoyaibua, yatatendewa haki na wasomaji akiwemo Silas. Nisamehewe kwa kasoro zozote zanazojitokeza na kuwaletea usumbufu wasomaji wangu.

    Wakati napitia mjadala, nilihisi alikuwa akijibu hoja za wasomaji wasiotaja majina yao. Pengine wakati mwingine atabainisha hoja kabla hajazijibu.

    asanteni

    JibuFuta
  7. Nawashukuru wote kuna kashule nimepata hapa!

    JibuFuta
  8. JE! MUNGU NA YESU NI MMOJA?
    Makanisa ya Kikristo yanafunza ya kuwa Yesu Kristo si kama kuwa ni Mwana wa Mungu tu, bali hakika ni Mungu khasa. Baba, Mwana na Roho Mtakatifu ni mmoja. Watatu katika mmoja, na mmoja katika watatu. Wote ni wa milele, wote ni sawa. Yesu ni Mungu, na Mungu ni Yesu. Hiyo ni imani ya Kikristo, ambayo inaaminiwa na karibu Wakristo wote. Hebu tuifunue Biblia tutazame inasema nini katika jambo hili?
    Mt Paulo katika barua yake ya kwanza kuwapelekea Wakorintho aliandika:

    Naam, na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi.
    1 Wakorintho 15.15

    Juu ya kuwa Paulo anaambiwa ya kuwa akiamini kuwa Masihi (yaani Kristo) na Mwenyezi Mungu ni kitu kimoja hapa anasema: "Tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo." Ikiwa Mungu kamfufua Kristo, hawawezi kuwa wote wawili hao ni mtu mmoja. Mmoja alikuwa ni mtenda, mfufuaji, na wa pili alikuwa ni mtendwa, mfufuliwa. Kama Kristo ni Mungu mwenye uwezo wa kufufua basi maelekeo ni kusema: "Kristo kajifufua", sio kafufuliwa. Mwenye kufufuliwa ni mfu asiyejiweza kitu.
    Katika kitabu cha Matendo ya Mitume inasimuliwa kuwa Mt Stefano alisema aliyoyaona yaliyo mbinguni. Alisema:

    Tazama! naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu.
    Matendo 7.56

    Mwana wa Adamu ndiye Yesu, na kwa jina hilo ndio mwenyewe akipenda kujiita, sio Mwana wa Mungu. Hapo basi huko mbinguni Stefano anasema anamwona Yesu kakaa mkono wa kulia wa Mungu. Mwenye kukaa mkono wa kulia wa fulani hawezi kuwa ndiye yule yule fulani. Hayo ni maelezo ya mbinguni. Ni wazi basi kwa ushahidi wa Biblia kuwa Yesu hakuwa Mungu mbinguni kama alivyokuwa si Mungu duniani.
    Yesu alipokimbilia kwenye Mlima wa Zaituni na huku akisakwa na Mayahudi alijitenga na wanafunzi wake. Huko faraghani aliomba hivi:

    Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.
    Luka 22.42-43

    Hapa tunaona mambo matatu muhimu:

    Yesu anamwomba Mungu. Yesu anamwabudu Mungu. Wawili hao ni mbali mbali, na vyeo vyao ni mbali mbali. Yesu ni mtumwa mnyonge mwenye kuomba na kuabudu. Na Mungu ni Mwenyezi Mungu mwenye uwezo wote na mwenye kustahiki kuabudiwa pekee, hata na Yesu, mwenye kutakiwa msaada pekee, hata na Yesu.
    Mapenzi ya Mungu ni mbali na yale ya Yesu. Yesu hataki kuuliwa, ananyenyekea na kuomba kwa Bwana wake: "uniondolee kikombe hiki" cha mauti. Yesu hana azma hata chembe ya kufa msalabani, kifo cha mhalifu, kifo cha laana kama maadui zake Mayahudi walivyoazimia kumpatilisha nacho. Lakini anakiri kuwa ni mapenzi ya Mungu sio yake yeye yatendeke. Yeye hana hila wala nguvu za kuzuia kudra ya Mwenyezi Mungu.
    Yesu, Mwana wa Adamu, anakata tamaa. Imani inampunguka. Kavunjika moyo. Ikabidi "Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu."
    Jee, yaelekea kuwa Yesu ndiye Mungu? Yaelekea kuwa yeye na Mungu kuwa ni sawa? Kama upo wasiwasi wo wote wa kujibu hayo, mwenyewe Yesu anajibu kama anavyo hadithiwa na Yohana kuwa kasema:

    Baba ni mkuu kuliko mimi.
    Yohana 14.28

    Na mwishoni naye yupo mslabani:

    Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha?
    Mathayo 27.46

    Yafaa hapa tujiulize: Yesu akimlilia Mungu gani hapo msalabani ikiwa naye mwenyewe ni Mungu? Au nini alikusudia aliposema: "Mungu wangu naye ni Mungu wenu"? Maneno hayo kama yanaonyesha cho chote basi yanaonyesha unyenyekevu wa Yesu mbele ya Mungu wake. La kustaajabisha ni kule kukata tamaa kwake na kuvunjika moyo. Huwaje mtu wa imani, licha ya nabii na mwana pekee wa Mungu, akate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Ama kuwa Mungu akate tamaa na Mungu, na kumyayatikia: "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha", ni jambo ambalo halimkiniki kuwa.
    Kwa uthibitisho ulio wazi Biblia inatwambia kuwa Yesu si Mungu, wala Mungu si Yesu.

    JibuFuta
  9. ningeomba niulize Maswali.

    1. Hivi kwanini kila dini au dhehebu yote yanaungana na kulishambulia kanisa katoliki??
    2. Je ni kanisa katoliki pekee lenye weakness?

    Kumbukeni humu duniani sote ni watenda dhambi si mchungaji wala shekhe sote ni wadhambi.

    Lakin one day ukwel utajulikana.
    Japo kuwa linasemwa sana lakin kwa nguvu za mungu kanisa katolik bado lipo IMARA.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Pay $900? I quit blogging

Haiba ni nini?

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Heri ya mwezi mpya!