Kulikoni mambo ya dini



Ule mjadala hatujauhitimisha. Kama unayo maoni unaweza kuyaacha pale.

Kwa sasa ningependa kudurusu baadhi ya mambo yaliyojitokeza kwenye mjadala ule ambao ulipata maoni ya wasomaji mbalimbali. Ikumbukwe kwamba blogu zina maana hasa yanapokuwepo maoni ya wanaosoma na sio kuendeleza tu yale ya aliyeandika.

Jambo la kwanza lililojitokeza katika majibizano ya wasomaji wawili walioficha majina yao, ni kuhusu historia ya Uislamu. Kwamba mmoja anadhani Uislamu ulianza tangu kuumbwa kwa Dunia, na mwingine anadhani Uislamu haukuwepo hata miaka 2000 iliyopita.


Nijuavyo mimi, kabla ya miaka 2000 iliyopita, haukuwepo Ukristo wala Uislamu. Hizi zote ni dini za juzi juzi. Dini iliyokuwepo enzi hizo katika nchi hizo tunazoiita takatifu ilikuwa ni Judaism. Dini isiyo na uhusiano wa moja kwa moja na Uslamu wala Ukristo.

Ibrahimu anayetajwa na msomaji mojawapo kuwa na mila ya dini mojawapo, alikuwa na mila na utamaduni wa Kiyahudi mwenye dini ya Uyuda (Judaism).

Maana ya historia hii ni nini?

Dini zote hizi za kigeni zina mwanzo wake baada ya miaka 2000 iliyopita. Zina waanzilishi wake. Na kila moja inayo falsafa zake, ambazo kimsingi hazijulikani kwa waumini wengi siku hizi. Ni bahati mbay sana kwamba waumini wa dini hizi wako gizani na wanahitaji guvu za ziada kufungua macho yao.

Itaendelea...

Maoni

  1. Ngoja nikuite Bwaya sio Christian sababu umejidai kuwa neutral ingawa chembe chembe za udini zinakuumiza moyoni. Vyema kwanza nikukosoe katika kujenga hoja yako umesema mimi nadhani...! Mimi SIDHANI kama uislam ulianza tangu mwanzo wa dunia ILA NAELEWA na NAAMINI hivyo (siokudhani tu)!
    Nije kwenye mada yako, ingawa huja sema historia yako hiyo umeitoa wapi (source), na hujatwambia unaiamini kwa kiasi gani, huenda pia nikutoka kwa mafundisho ya kikristo, kwa hiyo bado unahubiri ukristo, na si mafundisho ya historia halisi. Ingawa ni vigumu kukufanya uamini nnachotaka kukufahamisha, sababu historia yangu mimi naipata kwenye KITABU kitukufu cha Allah (qur-an) ambacho wewe hukiamini, Lakini ni rahisi kukueleza. Acha ni kueleze;
    Kwa mafundisho sahihi ya uislam, yanaeleza uislam ni dini iliyoanza tangu binaadamu wa kwanza ambae ni Adam, huyu kwetu ndio mtume, ikaendelea kwa mitume wengi kwa nyakati tifauti na sehemu tofauti kama vile idrisa, Nuhu, yussuf, haroun, mussa, is-haka, yakoub, na wengine mpaka ikafika kwa Issa na wa Mwisho ni Muhammad (SAW), historia inasema mitume hawa wako zaidi ya 1000, ingawa kwenye quraani wametajwa 25 tu.
    Labda kwanini naamini uislam ulianza tangu kwa Adam´? Kwa sababu lengo la kuumbwa kwa wanaadamu ni kuja kumtukuza mungu (kufanya ibada), basi lazima hawa binaadamu wawe na mfumo wa kufanya hizo ibada, lazima wawe na njia, na njia hiyo lazima iwe inatoka kwa huyo aliyewaumba, na kwa sababu lengo lao ni moja ingawa wana kuja kwa nyakati na sehemu tofauti lazima njia yao iwe ni moja! Hivyo basi kwa Allah anasema HAKIKA DINI (njia) YA HAKI kwake ni UISLAM, kwa hiyo kama Adam aliumbwa lazima alipewa njia hii ya haki (uislam) ili atekeleze LENGO la kuumbwa kwake kwa usahihi!

    Kama ukiikata "source" ninayoamini kupata hostoria hiyo, jee kwanini mimi niamini source yako ulopata histora hiyo uloandika hapo kwenye blog yako????

    Hitimisho: Mambo ya historia yanaongozwa na imani, inaweza kuwa ya kidini (uislam au ukristo) au imani kwa mtu anaekuelezea (source) sababu hatukuepo, no proof! Ni imani tu, na imani yako huwezi lazimisha iwe ndo usahihi kwa kila mtu, itakuwa sahihi kwa wenye imani ya aina yako tu. Usijaribu kamwe kutoa "conlussion" kwenye mambo ya kuamini ambayo huweza kuhakikisha, sio kwa simulizi tu!

    JibuFuta
  2. Ni wazi hakuna aliyekuwepo miaka maelfu iliyopita. Hakuna alo na hakika na historia. Lakini bado historia ni mwalimu mkweli.
    Naungana na Bwaya juu ya uawali wa dini ya kiyahudi.
    Hizi zingine zinazoivuruga dunia wala si dini za tangu kuumbwa kwa ulimwengu.
    Lakini mi naweza kusema kwa yakini, hakuna anayeweza kutembea kifua mbele akidai yake nd'o dini sahihi.
    Tatizo la ndugu yangu Nautiakasi ni kulazimisha kuwa uislam ndo dini 'yenyewe'
    Mi nadhani kila mtu anayo imani yake. Kinachofurahisha uislam na ukristo hazikuwa dini zetu waafrika.
    Babu zetu hawakuwa katika dini hizo.
    Kuja kwa wageni toka mashariki ya kati na ulaya ndiko kulikoleta dini hizi katika afrika.
    Mababu zetu walilazimika kupokea dini mpya. Walozileta walizieneza kwa madhumuni yao kiuchumi na wala si kingine. Dini zote mbili hazikuwatenda vema waafrika hawa.
    Tumezaliwa kwenye familia zilizorithi dini hizi pasipo kufahamu walioziingiza katika koo zetu walilazimika kwa mazingira yapi.
    Tukitazama historia, tunapata ufahamu kuwa dini zote mbili zilitufanya waafrika kuwa watumwa.
    Kimsingi hatuna haja kugombana, hizi dini wala si zetu waafrika.
    Labda niseme hivyo!

    JibuFuta
  3. Ngoja niendelee kukuza uelewa kupitia majadiliano haya. Ahsante kaka Bwaya kwa kuleta changamoto.

    JibuFuta
  4. Nautiakasi, twende taratibu tusijadili mambo mengi kwa wakati mmoja.

    Hatuzungumzii usahihi wa dini hivi sasa. Tunazungumzia historia ya dini za sasa.

    Katika falsafa, huwezi kujadiliana kwa dhati ukijitengenezea uzio wa uelewa. Sifa za mtu atakayekujifunza ni pamoja na kuwa tayari kubadili mawazo yake ikiwa itakuwa lazima.

    Haya. Kuhusu vyanzo vya historia.

    Historia isiyopendelea dini fulani ndiyo tunayoitaka.

    Utakuwa shabiki wa dini yako kama utaendelea kujiaminisha kuwa Uislamu ulikuwapo enzi na enzi. Aliyeuleta Uislam anajulikana. Kurani kitabu chenye maelekezo kwa waislam kimeandikwa lini? Unajua? Ndugu yangu kabla ya Uislam waarabu waliishi kwa mila na desturi zao kama kawaida ambazo WANAENDELEA NAZO LEO.

    Ukristo hali kadhalika ulianza alipozaliwa Yesu. Kabla yake Ukristo haukuwepo! Wayahudi walikuwa na dini zao, mila na desturi zao.

    Tupunguze ushabiki tujadili uhalisi.

    JibuFuta
  5. Naona hapa darasa hili linaleta changamoto kweli. Ahsante kaka Bwaya kwani wengi tutajifunza mawili matatu:-)

    JibuFuta
  6. Yasinta, karibu kwa maoni yako pia. Kujifunza ni kujadiliana.

    JibuFuta
  7. Nautiakasi21/7/09 8:37 PM

    Bwaya kaka bwaya upo uwezekano huwa hufikirii unachoandika, unataka tutafute vyanzo visivyopendelea dini yoyote, kwa mafundisho ya ukristo wanakubali bila ubishi kwa dini yao haikuanza mwanzo wa dunia, wakati huo huo kwa mafundisho ya uislam (sahihi) tunakubali pasi shaka kwamba uislam ulianza tangu mwanzo wa dunia! Ndo hakuna chanzo utakacho kinukuu kisiwe kina pendelea dini yoyote! Umenipata hapo??? Sasa muhimu ni kwa namna gani unakiamini chanzo hicho. Mimi naiamini Qur-an kuwa ndo chanzo cha changu cha kujifunza historia hii ya dini hizi.
    Pili utofautishe UARABU na UISLAM, narudia tena uarabu SI uislam..! Pili lazima uwele kwamba kwa mafundisho ya uislam, mungu ameweka uislam kuwa ni njia au utaratibu wa maisha wa mwanaadamu, Lakini hii haizuii baadhi ya watu kujitaftia njia (utaratibu)nyengine za maisha, kama hizo dini za uyahudi, ukristo n.k! Hivyo basi historia inatwambia kwa kila kipindi cha nabii (kuanzia adamu) walizuka watu na utaratibu wao usio huu uislam. Kwa hiyo nikweli tena uko sahihi sana, kabla ya kutumwa Mtume Muhammad (SAW)kuja kufundisha njia sahihi ya kuishi (uislam) hao waarabu walikuwa na njia zao (uyahudi na ukristo pia ulikuepo), na ndo maana mungu alimtuma Muhammad kuja KUHUISHA uislam SI KUANZISHA uislam! (angalia mantiki hiyo)sababu uislam ulianza zamaniiiiiiiiii!

    Mkristo kama bado unashaka na dini yako, ni jambo jema sasa yakupasa kuitafuta dini utakayoamini na usiwe na shaka..! Acha hoja dhaifu eti waafrika walikuwa na dini zao, ujio wa watu wa ulaya na middle east ndo walileta dini mpya!!! Jee umesahau mafundisho yako kwamba Yesu mwenye alisema hakuja kwa watakatifu bali kwa ajili ya wenye dhambi??? Hivi si upuuzi kujaza chai kwenye kikombe kilicho jaa tayari! Jee huoni kwamba kutokana na kutokuwa katika njia sahihi ndo mungu aliwaleta hao kuja kutufunza dini sahihi? Na haya ndo mafundisho ya uislam, Muhhamad alikuja kwa dunia nzima, kuna mitume walitumwa kwa ajili ya watu wa sehemu flani tu!
    Kwa wale wasio amini uwepo wa Mungu, Bible inasema kumjuwa Mungu ni chanzo cha hekima (nna shaka na hekima zenu)

    JibuFuta
  8. Nautiakasi,

    Ni lazima uwe na mashaka na hekima za wengine kwa sababu huwezi kutegemea kuona rangi ya njano wakati umevaa miwani ya bluu.

    Chanzo cha taarifa unachokitumia kiko biased. Huwezi kutegemea habari nyingine zaidi ya hizo ulizonazo.

    Jifunze zaidi ya mipaka ya dini yako tutaelewana.

    JibuFuta
  9. sipendi kuwa kama wale wanaoshikilia upande mmoja wa mambo. labda swali langu ni je! uisilamu nini na ukkristo ninini na mwisilami ninani pia mkristo ninani? tafuteni maana ya maneno haya kwanza harafu mlete ubishi wenu wa kiakili!

    nautiakasi,

    hivi wewe unaamini kkuwa koran ilitoka mbinguni? itakuwaje leo kama ikishushwa nyingine au unauhakika gani kama haikuwahi kushushwa? je ni kitabu gani tunapaswa kukifuata? hivi tunavyochapwa viboko kuvikariri au kingine muhimu ambacho hatukioni kwani kimo ndani mwetu?

    wapi muhimu kama sio ndani mwetu? kwa nini tusi- 'tahajudi' (meditate) na kuuona ukweli mkubwa zaidi badala ya vijitabu hivi????

    JibuFuta
  10. Tatizo hapa watu wanauliza si wapate kujua bali wapate kukujua, ikiwa mtu anapewa hoja kutoka kwenye chanzo anachokiamini yeye na hoja hiyo iko wazi tu, bado haikubaliani nayo, inaonyesha itakuwa vigumu kuelewana na kuafikiana katika mawazo ambayo yana ukweli ndani yake. Matatizo watu hawaisomi hii Kuran, nadhani watu hawaifahamu maana ya neno kuran,maana ya Kuran ni chenye kusomwa, naomba wadau wawe wanaisoma hii Kuran ili waifahamu, wasikiogope kwani hakina madhara yoyote bali huwa kinaleta utulivu wa moyo. Watu wanasema Kuran haitoki mbinguni(kwa Allah)? Ndani ya Kuran imesema ikiwa hii Kuran haitoki kwa Allah basi watu wangelikuta ndani ya hii Kuran kuna ikhtilafu nyingi, ndani ya kitabu hiki kuna elimu tofauti, imezumzia kuhusu elimu ya embryology, zoology, geology na kadhalika hivi leo wanasayansi wanathibitisha mambo haya ambayo ni vigumu kwa mtu wa miaka 1400 iliyopita kuyajua ikiwa hajafunuliwa na Mjuzi aliye Mkuu(Allah). Watu wanadai kuwa dini hizi zimewafanya waafrika watumwa, naomba tuasahihishane kama tumekosea, utumwa ulikuwapo sehemu zote za ulimwengu, mayahudi walifanywa watumwa na wamisri, wairish walikuwa watumwa wa waingereza na hata hapa Afrika waafrika walifanyana watumwa baadhi yao, tulisoma kwenye historia baadhi ya makabila yakipigana wale mateka huwa watumwa,inasemekana kuwa kuna baadhi ya machifu ndiyo waliokuwa wakiwauza waafrika wenzao kwa hao wakoloni. Tufahamu ya kuwa hao wakoloni waliokuja walikuwa na sababu za kiuchumi lakini walikuwa watu wengine ambao kusudio lao la ujaji wa Afrika ni kutangaza dini. Kila mtu ana imani yake, lakini kwa imani ya kiislamu inaamini kuwa mtume Muhammad (S.A.W) amekuja kurekebisha yale yaliyoharibiwa, kwanini kauelezea unaswara katika Kuran? Kwani waarabu walikuwa manaswara? Walikuwa na imani zao za kuabudu masanamu, ikiwa atamzungumzia Issa (A.S) na mama yake (Mariam), habari hizi kaambiwa na nani? kama siyo ufunuo, kwanini asizungumzie habari ya baba yake au mama yake au wake zake au watoto wake ndani ya Kuran? Je hatulitambui hilo? Ukweli ni kuwa Yesu wakati ule watu hawakumfahamu mpaka kaondoka, ndiyo maana alisema akija huyo(comforter) atawaelezea yaliyo haki, na Muhammad(S.A.W) ndiye aliyekuja kuyaeleza haswa ujumbe wa Yesu. Sisi tunaambiwa tuwe wakristo,je Yesu alilitamka hili neno Kristo? au kwa lugha yake lina tamkwaje? Maana tumesoma kuwa neno (Christ) linatokana na neno la kigiriki (Kristos)na maana yake ni mpakwa mafuta, kwa kuwa wafalme wakitawadhishwa ufalme huwa wanapakwa mafuta na watu watakatifu pia hupakwa mafuta hiyo ilikuwa ndiyo ada yao, sasa Yesu akisema kuweni wakristo, hamaanishi tuwe watakatifu? Na mtakatifu ni yule aliyejitakasa na kunyenyekea kwa Mola Muumba, je huyo si yule aliyejisalimisha kwa Mungu ambaye ndiye MUISLAMU? Leo tunaona kuwa Roma ndiyo makao makuu ya ukristo na si Bethlehem ambako Yesu kazaliwa na hao waroma ndiyo waliokuwa maadui wakubwa wa waisraeli, na kwanini bado waisraeli wana dini yao ya kiyahudi na wasiwe wakristo na wao waokoke? Na ilhali Yesu alikuwa miongoni mwao aliyezungumza lugha yao na kuna athari zake mpaka hii leo huko wanapoishi? Naomba ndugu wadau tutafute neno halisi alilolitamka Yesu ili liwe ndiyo rejea hoja kwetu, kwani kuna watu waliomfanya Yesu kuwa ni mungu, sasa kama alikuwa mungu aliyekuja kwa maumbile ya kibinadamu kwa hakika alikuwa akizungumza lugha ambayo watu walimfahamu, na inasemekana alikuwa akizungumza kiamarik, ikiwa mungu atashindwa kihifadhi maneno yake mwenyewe aliyoyasema kwa lugha aliyoitamka basi ni nani mwingine atakyeweza? Hii Biblia tunayoisoma kwanza iliandikwa katika lugha ya kigiriki, baadaye ikatafsiriwa katika kiingereza na sasa imefasiriwa katika lugha mbalimbali ikiwemo kiswahili, je hatuoni kama kutakuwa na upungufu wa maana kutoka katika vitabu asilia? Kwasababu tafsiri si neno halisi, hatukatai tafsiri zisiwepo, bali lile neno halisi liwepo ndiyo liwe rejea kwa vizazi vijavyo. Samahanini lakini ndiyo kuliko na mambo ya dini hayo.

    JibuFuta
  11. Naomba kutoa maoni yangu kujibu hoja za upotoshaji zilizoletwa na msomaji wako. Kwanza kama yeye alivyojitambulisha kwa hoja zake kuwa ni Mwislamu, mimi ni Mkristo. Nitajibu hoja zake moja baada ya nyingine ili aelewe kama atakuwa tayari.
    1. Walioendesha biashara ya utumwa walikuwa Waarabu wa kiislamu. Hawa walikuja Afrika mashariki kufanya biashara mbaya kabisa ya utumwa na kueneza dini yao. Watumwa walisombwa kutoka Afrika kwenda Uarabuni mahali panaposadikika kuwa chanzo cha Uislamu. Ushahidi: Mahali ambako biashara hii ilifanyika, ndiko Uislamu ukikojikita mpaka leo. Angalia Zanzibar, maeneo ya pwani ya Afrika Mashariki nk. Dini ya Kislamu inaonekana kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na Biashara hii mbaya ya utumwa.
    2. Hoja yake ya kukanusha kwamba dini zilileta utumwa ni dhaifu. Utumwa ni dhana pana inayoenda mbali zaidi ya utumwa wa kuuzana na kupigana bei. Utumwa unaohusishwa na dini ni ule wa akili kama hizi za kutetea dini za walioendesha biashara ya utumwa.
    3. Hoja kwamba mtume mohamadi eti ndiye msaidizi alisemwa na Yesu haiwezi kuwa zaidi ya kichekesho. Yesu kwanza alieleweka. Alikaa miaka mitatu, akitengeneza wafuasi ambao yeye aliwaita mitume. Aliwafundisha na kuwaonyesha nini walipaswa kufanya. Tatizo lilikuwa utendaji wa yale aliyowafundisha. Alijua hawataweza kuyafanya. Ndio maana wakati anaondoka, akawaambia wale wanafunzi, nitawaletea msaidizi, ndiye Roho Mtakatifu atakayewasaidia kuyashika niliyowafundisha (ambayo alifahamu wazi hawataweza kuyashika pasipo msaada wa zaidi). Roho Mtakatifu yupo hivi leo. Kila Mkristo anayo haki ya kuwa naye na akasaidiwa kumpendeza Mungu. Hata hivyo wapo wakristo wengi ambao hawana Roho Huyu kuwasaidia kumpendeza Mungu. Hawa wanabaki kuwa mashabiki wa dini wenye kufanya dhambi kama kawaida japo wanaweza kuenda kanisani. Hiyo ndiyo maana yake!Yesu akatika mafundisho yake alisema yeye ndiye Alfa na Omega. Yaani ndiye mwanzo na mwisho, hakuna kabla yake, na hata baada yake hayupo.
    4. Kusema eti Mohamedi amekuja kuueleza hasa ujumbe wa Yesu ni udanganyifu usio na mantiki. Kama nilivyosema, Yesu alikuwa na mafundisho yake ya msingi ambayo Mohamedi hana habari nayo. Mfano alisema mwenyewe kuwa yeye ni mwana wa Mungu aliyetumwa kuwakomboa wanadamu na dhambi. Ukombozi huu kutoka kwenye nguvu za giza, hauji kwa kushika orodha ndefu ya sheria za wayahudi. Ukombozi huu ungefanyika kwa namna ya Roho. Ndio maana alikufa msalabani kwa ajili ya dhambi za wanadamu. Hili si sehemu ya Uislamu wa Mohamadi. Hivyo kusema mohamadi alikuja kuueleza ujumbe wa Yesu ni mbinu tu za kutaka kuonekana ni dini kongwe kuliko zingine wakati inaeleweka kwamba ilianza karne ya 6 ikiwa na mafundisho tofauti na yale ya Yesu.

    (maneno ni mengi, nimeyaendeleza hapa chini...)

    JibuFuta
  12. 5. Hoja ya Ukristo na Kristo iko hivi: Yesu mwenyewe alilisema hili vizuri kuwa yeye ndiye alikuwa yule Masihi aliyekuwa akisubiriwa na Wayahudi kwa sababu alikuwa ametabiriwa katika Agano la Kale (kitabu kilichokuwa kikiaminiwa na Wayahudi). Wao wakamkataa na kumwua kwa hila ili tu mafundisho ya dini yao yaliyokuwa yakisisitiza sheria ambazo hazikuwa na uhusiano wowote na roho zao. Wakaamua kubaki na dini ya Mababu zao (Ibrahimu, Isaka na Yakobo). Na mpaka leo wayahudi wanamsubiri Masihi wao. Wafuasi wa mafundisho ya Yesu ndio hasa waliitwa Wakristo. Kwa maana nyingine, huwezi kuwa Mkristo kama HUFUATI alichofundisha Bwana Yesu. Kutumia ujanja wa maneno kuhalalisha uhusiano wa Uislamu na Ukristo ni fallacy. Hapa naweza kukubaliana na wanaosema kuwa Uyuda ulikuwepo kabla ya Ukristo. Lakini leo wapo hata kama ni wachache, waliokubali kumpokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa Maisha yao. Ninao marafiki wa Kiyahudi walio wakristo. Lakini nakubali kwamba wengi waliamua kushikilia mila na tamaduni zao wakaachana na mafundisho mapya ya Bwana Yesu. Huu ni ushahidi kwamba Ukristo si utamaduni wa mahali Fulani kwa sababu ulihitilafiana hata na utamaduni wa kule uliokanzia.
    6. Kingine, huyu bwana anasema eti Roma ndiyo makao makuu ya Ukristo! Hili haliwezi kusemwa na mtu mwenye ufahamu wa dhati wa anachokisema labda kama anabangaiza hoja za kueteta upande wake. Ndugu zangu Roma kama kweli ni makao makuu basi ni ya Ukatoliki na sio ukristo. Ukristo hauna makao makuu. Historia ya hawa Wakatoliki ni ndefu na sina muda wa kuieleza hapa ila itoshe kusema kwamba Warumi katika kipindi fulani waliitumia imani ya kikristo kwa maslahi yao ya Kisiasa. Mapapa wao kuna kipindi walikuwa watesaji wakubwa wa wafuasi wa kweli wa Ukristo. Sitakuwa nimekosea nikisema kuwa Ukatoliki na Ukristo ni vitu tofauti japo vinaonekana kuwa na uhusiano wa aina fulani. Unapozungumzia Ukatoliki usidhani moja kwa moja unazungumzia Ukristo. Ukatoliki ni mchanganyiko wa mambo mengi (siasa, utamaduni, dini nk)
    7. Kutafuta maneno halisi aliyoyatamka Yesu si lazima ingawa ni vizuri. Mimi kama mwanafunzi wa Biblia ninaweza kujifunza lugha za awali ambazo zilitumika kuandikia Biblia. Lakini kwa sababu silazimiki kukariri maneno yake, bali kuelewa na kuishi kama alivyosema, sifungwi na mahangaiko hayo! Kutafuta lugha hizo hakusaidii kumwelewa Yesu kama anavyoshauri huyu ndugu. Biblia imetafsiriwa katika lugha mbalimbali ili kueneza ujumbe wa Yesu kwa watu wa mataifa mbalimbali bila kuwalazimu kuwa watumwa wa utamaduni wa watu (lugha). Ndio maana leo hii Ukristo umeenea katika sehemu mbalimbali duniani. Hili ni tofauti na Uislamu ambao unalazimisha waumini wao kukariri maneno kwa lugha ya Kiarabu ambacho masikini hawawezi kukizungumza wakiwa nje ya misikiti. Sishangai kwa sababu Uislamu unasisitiza kukariri maneno kwa orodha ndefu ya sheria za kutekeleza, suala ambalo halisaidii roho zao. Unapodai eti kutafuta maneno kwa lugha ya asili ndiyo suluhisho, sasa wewe una hakika gani kuwa aliyeandika Kurani kwa kiarabu enzi hizo aliandika kwa usahihi unaotatikana? Au unadhani Kurani iliporomoka tu kutoka hewani ikiwa imeandikwa na asiyejulikana?

    JibuFuta
  13. Nimalizie kwa hoja ambayo inatembea kudai kuwa Adam na Hawa walikuwa Waislamu. Dini zote za mashariki ya kati zinaanzia kwa Adam na Hawa. Na kihistoria, masimulizi haya basi, yalikuwa ya Wayahudi ambao waliamini kuwa Ukoo wao, umetokana na Adamu na Hawa. Mlolongo kutokea hapo, umeenda mpaka kwa Ibrahimu ambaye Biblia inamtaja kama baba wa imani. Biblia sehemu ya Agano la Kale inaonyesha historia ya kabila au niseme nchi ambayo Mungu aliitumia kutufikisha kwa Bwana Yesu. Wayahudi wanamwani Ibrahimu kama Nabii wa dini yao na babu yao kwa damu kupitia kwa Isaka mwanae wa pekee. (Kuna hata wakristo wenye ufahamu finyu wanaodai eti Ibrahimu ni baba yao wa kiimani wakati wao hawana uhusiano wowote wa kidamu na Ibrahimu.) Biblia inaeleza wazi kwamba Ibrahimu alichelewa kuzaa akamwingilia mfanyakazi wake wa ndani (Hajir) na kumzaa mwana wa haramu Ishmael ambaye ndiye chanzo cha Waarabu. Hapo ndiko historia ya waarabu inakounganikia na kuachana na historia ya Waisrael. Wasomaji muelewe kwamba hapa tunazungumzia historia ya Waarabu na Waisrael (Wayahudi) na sio Uislamu na Ukristo. Sasa waarabu kupitia Ishmael na mama yake Hajir ndio waliokuja kumzaa Mohamedi maelfu ya miaka baadae na akaanza harakati za kutangaza dini yake ambayo haikuwepo kabla yake. Maelezo yanayotumika kulazimishia Uislamu kuanzia kwa Adam na Hawa ni ya kuunga unga na kucheza na maneno kuliko ukweli wa mambo.
    Ukweli ni kwamba kitabu cha Kurani na Biblia vinaonekana kuwa na maelezo yanayofanana hasa ya kihistoria kwa sababu kihistoria Waarabu na Wayahudi ni ndugu hata kama hawapatani kwa sasa. Na bahati mbaya dini ya Kiislamu inaitumia historia hiyo kujaribu kubinafsisha haki ya kuanzia mwanzo wa dunia. Ni bahati mbaya kwamba hawa hawa Waarabu na Wayahudi ndio chanzo cha imani kuu duniani.
    Mwisho Allah, jina la mungu wa Waarabu hana uhusiano na mungu wa Waisrael. Kumbuka kwamba dunia hii ina miungu mingi sana. Hata sisi waafrika tulikuwa na miungu yetu. Ni makosa kudhani eti haya ni majina tofauti ya Mungu mmoja. Hapana. Ikibidi nitalieleza hili kwa kirefu wakati mwingine. Kama hivyo ndivyo basi, huwezi kudai eti Allah ndiye alikuwa anawaagiza Adam na Hawa wakati ule wa mwanzo, na ukajiaminisha kwmaba unachosema ndio kweli kwa kutumia maneno eti unyenyekevu. Niishie hapa kwa leo.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia