Ukifikiri Upendo ni Vitu Utamkinai Anayekupenda

Juzi naongea na kijana mmoja, umri nakadiria kavuka miaka thelathini, ananiambia ameanza kuhisi kama vile hakuumbiwa mapenzi. Ukisikia mtu anatoa kauli nzito hivi ujue kuna jambo. Kudodosa, kumbe, kayapambania mapenzi na yamekaribia kumtoa roho. Kila anayempenda kwa dhati anaishia kumwacha hewani.  Haelewi afanye nini. 

“Hawa wanawake wanataka nini?” Kaniuliza. Tuliongea mengi. Naomba nikushirikishe, japo kwa muhtasari, maudhui ya mazungumzo yetu. 

 

Picha: Tony Cordoza Getty Images

Tumeanza kuwa na kizazi cha vijana werevu, watafutaji, wenye uwezo mkubwa wa kutafuta pesa lakini wenye hisia kificho, wasiojali hisia na wasio na haja ya kina cha mahusiano.  Hiki ni kizazi, aghalabu, kilichozaliwa na kizazi cha wazazi wasomi, wenye maarifa zaidi na pesa zaidi kuliko kizazi kilichopita. Tunatumia muda mwingi kazini, kwenye biashara, na shughuli nyingine za kutafuta vitu. Ukiangalia kwa haraka unaona hiki ni kizazi chenye watu wenye kazi nzuri, biashara kubwa, majumba, magari na kila aina ya mali ambazo wazazi wetu waliopita hawakuwa navyo. 

 

Kwa bahati mbaya sana wingi huu wa vitu na pesa unakuja na gharama kubwa kwenye malezi. Hatuna muda wa kuhusiana na watoto. Hatuna muda wa kupenda —kupatikana kihisia, kuzungumza, kusikiliza, kuhusiana, kujali na kadhalika. Imeanza kuwa kawaida, mzazi kutoka asubuhi nyumbani watoto wakiwa wamelala na kurudi jioni wakiwa wamelala. Kadhalika, imeanza kuwa kawaida kwa familia kuishi miji tofauti kwa sababu za kikazi na biashara. 

 

Kwa vile hatuna muda wa kupatikana, tunatumia vitu kama nyenzo muhimu ya malezi. Katika kufunika hatia ya kutokupatikana, tunawahonga watoto shule nzuri zinazofaulisha. Tunawataka watie bidii kwenye masomo kama njia ya uhakika ya kujitengenezea maisha yao. Jambo zuri lakini linalokuja na gharama isiyoonekana. 

 

Tunawahonga watoto midoli wasiyoihitaji. Mtoto akilia, kwa mfano, tunampa kishikwambi atulie. Kwa hivyo nyumba zetu zina kila aina ya ving’amuzi vinavyotumia muda mwingi na watoto wetu. Katuni zinatumika kupotezea hitaji la mtoto kusikika na kuonekana. Tukishindwa kuzungumza na mtoto tunawasha runinga kumnyamazisha. Tukikosa muda wa kulea tunalipia chekechea ya bweni. Unaweza kuona ongezeko la wimbi la watoto wadogo ambao kimsingi bado wana utegemezi mkubwa kwa wazazi kupelekwa shule za bweni.

 

Kwa mazingira haya, mtoto anaanza kujifunza namna mpya ya kushughulikia mahitaji yake ya kihisia kwa ugumu na maumivu makubwa. Watoto wengi, mathalani, wamejifunza kuishi maisha ya upweke. Hawana mahusiano ya karibu na wazazi wao. Ukimwuliza mtoto leo anamwamini nani zaidi, nani anaweza kumwambia hofu zake, mambo yake binafsi, siri zake, unaweza kushangaa anayetajwa ni mtu mwingine nje ya familia aghalabu anayeonekana zaidi kwenye luninga.

 

Tunafahamu mzazi ndiye mwenye mchango mkubwa kujenga dhana ya kipi ni muhimu zaidi kwa mtoto. Kupitia matarajio anayoyaona kwa mzazi wake, mtoto anaafanya ‘ugunduzi’ muhimu kuhusu nini hasa ni muhimu kwa mzazi wake na maisha kwa ujumla. 

 

Kwa mfano, kila anapokutana na mzazi swali lisilokosekana ni ‘homework’ na ‘umekuwa wa wangapi?’ Ugomvi mkubwa ni kazi za shule na matokeo. Ukitaka kumfurahisha mzazi unalazimika kufaulu mengine yote ikiwemo maadili yanavumilika. Ukiwa mshenzi, mwongo, huna adabu lakini unaongoza darasa, unavumilika kwa mzazi. Mtoto anajua, hatua kwa hatua, kuwa kilicho muhimu zaidi kwa mzazi ni matokeo ya mitihani. 

 

Kazi kubwa inakuwa ni kusoma na kufaulu. Hatuna anayejali hisia na mahusiano. Kwa hakika ni kama muda na nguvu nyingi zinatumika kupuuza hisia. Upweke, kupuuza hisia, kucheza na hisia za watu, ubinafsi, kukweza vitu na wenye vitu inakuwa sehemu ya mahusiano. Mtazamo huu wa maisha unaunda mwelekeo mpya wa mahusiano na watu ili  mtoto aweze kumudu uhaba mkubwa wa upendo. Rejea aya ya kwanza kwa tafsiri ya upendo. Matokeo yake, tukifikia umri wa mahusiano, kama wa kijana niliyekutana naye, tunachoshwa haraka uhusiano unaotudai tupende. 

 

Tunataka kupendwa lakini hatuelewi upendo maana yake nini. Tunataka kuaminiwa lakini tunamchoka haraka anayetuamini. Hatujazoea kuaminiwa. Tunataka mtu aoneshe kujali lakini tunakinai haraka kujali kukimaanisha muda kwa ajili yetu. Tunatamani kueleweka lakini tunatishwa na muunganiko wa hisia. Tumezoeshwa vitu kutumika kama mbadala wa kuhafahamiana vizuri, kuunganika kihisia na shauku ya kuwa karibu na mtu.

 

Tunalea kizazi ambacho ukimnyima mtu muda wako ukampa pesa anaamini unampenda, hata kama utamuondoa kabisa kwenye ratiba zako. Ukimpa mtu muda wako, usikivu, ukawekeza kwenye mahusiano, lakini usiwe na pesa mtu anaona unamchosha. Ukimnyima muunganiko wa hisia, ukampa uhakika wa ufundi wa ngono anachagua ngono hata akikosa uhakika wa mahusiano ya kudumu. Jitihada zozote za kudumisha mahusiano bila ngono inaonekana ni mzaha na ndoto za abunuwasi.

 

Hatutaki kuwekeza tunataka kupita. Hatutaki kudumisha tunataka kusisimuka. Hatutaki kufahamiana tunataka kutumiana. Hatutaki kujipa muda tunataka kilicho tayari. Hatutaki gharama tunataka matokeo. Hatutaki kutafuta tunataka vya kupewa. Hatutaki kusubiri tunataka ghafla. Hatutaki uaminifu tunataka uhuru. Hatutaki usisi tunataka umimi. Hiki ndicho kizazi kinachoishi matokeo halisi ya utoto uliotekelezwa. Hiki ndicho kizazi kinachotafsiri vitu na mali kama upendo. Ukifikiri upendo ni vitu utamkinai anayekupenda.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Uislamu ulianza lini?

Haiba ni nini?

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3