Kwa Nini Wanawake Wenye Mafanikio Wanaogopwa?





UPO ukweli kuwa wanaume wengi wanawaogopa wanawake wenye mafanikio. Hawa ni wanawake wenye kiwango kikubwa cha elimu, fedha, umaarufu au hata madaraka katika jamii. Hoja ya wanaume wenye mawazo haya ni ugumu wa kuwaongoza wanawake wanaowazidi kama alivyonieleza Godfrey, mwalimu wa sekondari jijini Arusha:

“Mwanawake akipata kitu anakuwa jeuri sana. Hawezi kukusikiliza tena na atataka awe huru kufanya mambo yake bila kuingiliwa.” Kwa mujibu wa Godfrey, uwezo wa kifedha na mafanikio kwenye maeneo mengine ya maisha mara nyingi humfanya mwanamke asiwe na utayari wa kuwa chini ya utawala wa mwanaume. “Huwezi kuishi na mwanamke anayejiona yuko juu yako na ukabaki salama. Hatokuwa tayari kukupa nafasi ya kuwa na sauti kwenye nyumba.”

Hitaji kubwa la wanaume wengi ni mamlaka. Wanaume wanapoingia kwenye uhusiano na mwanamke wanakuwa na shauku ya kuwa na sauti inayosikika bayana kukidhi dhana ya kichwa cha familia. Ili sauti hii iweze kusikika bara bara uwezo wa kifedha, kielimu, kimadaraka na hata umaarufu unakuwa na nafasi yake.

Kwa maana hiyo inapotokea mwanamke ameshindwa kuwa chini ya mamlaka yake, mwanaume huanza kujisikia hayuko salama kama anavyoeleza Dickson, karani wa benki mjini Moshi:
“Niliwahi kuwa na dada mmoja mwenye Masters wakati huo mimi nafanya shughuli zangu ndogo ndogo za kiujasiriamali na elimu yangu ya Diploma. Kaka nilikoma kuringa. Mule ndani tulikuwa na bunge lisiloisha. Kila ninachosema, bi mkubwa lazima apinge. Masters ikawa inashindana na Diploma sikuweza kuvumilia.”

 Inavyoonekana kuna ukweli kuwa mwanamke anapokuwa na mafanikio anakuwa na nguvu saidi. Hii si kwa wanawake pekee. Hata wanaume nao wanapofanikiwa wanakuwa na nguvu zaidi katika jamii. Hadhi yao katika jamii inaongezeka na wanasikika zaidi kuliko watu wasio na mafanikio.

Lakini je, kwa nini mwanaume atishwe na sauti ya mwanamke? Je, haiwezekani mwanamke awe na sauti sawa na mwanaume na mambo yakaenda? Silas anajibu, “Lazima mwanamke awe chini ya mwanamke. Iko hivyo tangu kuumbwa kwa dunia. Ukijaribu kupora mamlaka ya mwanaume umepora uanaume wake.”

Kwa upande mwingine tatizo linaweza lisiwe mafanikio ya mwanamke bali kutokujiamini kwa wanaume kama anavyoeleza Irene: “Wanaume wengi hawajiamini. Wanajitutumua tu kwa mabavu na ukali lakini wamejaa wasiwasi. Kwa nini utishwe na mafanikio ya mwanamke kama unajiamini?” anauliza Irene ambaye ni mhasibu wa shirika la moja la umma na kuendelea, “Kwa nini utake kuwa juu ya mwanamke? Kwani ukiwa sawa na mwanamke unakosa uanaume wako? Haya ni mawazo yaliyopitwa na wakati.”

Kwa mujibu wa Irene, si wakati wote tatizo linakuwa ni mwanamke mwenye mafanikio. Wakati mwingine hizi huwa ni hisia tu ambazo zikiaminiwa hugeuka kuwa kweli. Inavyoonekana wanaume wengi wana nafsi zilizo na umaskini wa hadhi na hivyo wanatumia mahusiano yao na wanawake kushibisha njaa waliyonayo.

“Umewahi kujiuliza kwa nini wanaume wengi wanapenda kuoa wanawake wanaowazidi? Maprofesa wengi wanaoa darasa la saba. Mtu kusoma kote anaishia kuoa housegirl. Unafikiri ni kwa nini?” aliniuliza Balibate. Hoja yake ni kuwa wanaume huvutiwa na wanawake dhaifu ili waweze kuwatawala kwa urahisi.

“Mwanaume wa kawaida yuko radhi aoe mwanamke asiye na mbele wala nyuma tena bila kipato chochote ili iwe rahisi kumtawala. Nafikiri suala hili limekaa kimazoea zaidi kuliko kimaumbile. Tumelelewa tukiaminishwa uanaume ni jinsia bora zaidi kuliko kuwa mwanamke.”

Kama anavyoeleza Balibate, wanaume wengi huficha udhaifu wao kwa kuvutiwa na wanawake dhaifu. Jitihada za kujihami na fedheha ya kuonekana yeye ni mtu asiye na mamlaka humfanya aogope kuwa na mwanamke anayeweza kumzidi.

Tunachoweza kujifunza ni kuwa kuna ukweli kiasi fulani kuwa shida ipo. Wanawake wenye mafanikio huwa ni tishio kwa baadhi ya wanaume. Ipo haja kwa wanawake kuchukua hatua za kuondoa tishio hili. Wanawake wasiogope kufanya wajibu wao kama wanawake kwa kutambua mahitaji ya kisaikolojia ya wanaume. Mwanamke waepuke kutumia mafanikio yao kushindana na wanaume.

Lakini pia wanaume, kwa upande mwingine, wanahitaji kujitambua na kuelewa kuwa hawawezi kuwa imara zaidi kwa kutumia mbinu za kizamani. Siku hizi wanawake wengi wanakwenda shule. Nafasi yao kufanikiwa imekuwa kubwa sawa na wanaume. Wanaume wakubali kuwa wanawake nao wanaweza kuwa na mafanikio. Mawazo kuwa uimara wa wanaume utegemee udhaifu wa wanawake yamepitwa na wakati. Muhimu ni wote, mwanaume na mwanamke kujitambua na kutambua wajibu wao.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia

Uislamu ulianza lini?