Ni kweli kuwa viumbe wametokana na mabadiliko 'ya kubahatisha'?

Tulichagua kutumia kanuni za Marehemu Charles Darwin kwa sababu ndiye aliyejaribu kujihusisha kwa kiasi kikubwa na asili ya mabadiliko ya viumbe kwa mtazamo wa kisayansi. Na kwa kuwa lengo letu ni kuitizama sayansi kwa jicho la haki, tunaona na ni vyema “kuweka kumbukumbu sawa”.

Marehemu Darwin amejaribu kuonyesha kwamba viumbe vilitokea kwa bahati, vikapitia mabadiliko ya uasili wao kufanya asili nyingine iliosababisha kugeuka na kuwa viumbe vya aina nyingine kabisa.

Ili kufafanua anachosema Darwin na rafiki zake, tuchukulie mfano wa viumbe kama samaki. Samaki, kwa mujibu wa kanuni ya “natural selection”, walipitia mageuzi kadhaa yaliyosababisha tofauti katika kundi lao la samaki. Tofauti hizi ziliendelea kuwa kubwa kiasi cha kusababisha kutengenezeka kwa aina fulani ya samaki waliokuja kufanya kundi la viumbe tofauti kabisa na samaki wengine waliobaki.

[Kundi hili linafahamika kama amphibia lenye mifano ya viumbe kama mamba na vyura].

Maana yake ni kwamba katika samaki, walitokea samaki waliokataa asili yao na kufanya asili nyingine iliyosababisha kutokea kwa viumbe vingine. Utetezi wa mabadiliko haya yanayosemwa na akina Darwin, ni mazingira. Kwamba samaki hawa, kwa mfano, waliishi katika mazingira yanayotofautiana kiasi cha kugeuka kwa asili yao. Kwamba asili hugeuzwa na mazingira kwa maana ya samaki kubadili tabia zake ili kuendana na mabadiliko ya mazingira alimo, ni jambo ambalo linatupasa kufikiri kwa tahadhari.

Kwamba asili ya kiumbe ndiyo inayomsaidia kugeuka ili kukabidili mabadiliko katika mazingira yake na kwamba asili yake ilibadilika, ikimtenga na wenzake, ili kufanya kundi lingine linalojitegemea la viumbe jamii nyingine, hilo si jambo rahisi.

Jambo moja ni vizuri tukalisema. Tunapozungumzia asili, moja kwa moja tunazungumzia chembechembe za viasili katika kiumbe. Viasili hivi, ndio hasa vidhibiti vya maisha na mwenendo wa kiumbe.

Chembechembe za mwili hufanya kazi kwa namna ambayo, naweza kusema, ni tata (complex) kuliko hata utata (complexity) wa kiumbe chenyewe. Nina maana hii. Ufanyi kazi wake unaonekana kupangilika sana kiasi kwamba ni vigumu kukubali urahisishaji huu unaofanywa watu kama akina Marehemu Darwin na Wallace.

Ipo mifumo kamili katika chembechembe hizi. Na mifumo yenyewe ina viambata kwa maelfu ambavyo vikihitilifika kidogo tu utendaji kazi wake hujaribu kujirekesha kurudia hali ya kawaida, ama la, husitishwa kabisa.

Ni kwa sababu hiyo, huwezi kuzungumzia mageuzi ya chembechembe hizi kwa urahisishaji wa kizembe kama huu, eti kwa kigezo cha kukadiria mamilioni ya miaka kuhalalisha mabadiliko hayo.

Sababu yake ni kwamba uasili wa kiumbe unaonyesha dhana ya mpangilio sawia ambao ni mwendawazimu peke yake anaweza kudhani vilijiweka hivyo kwa bahati bahati tu, yaani vilitokea tokea tu. Huo ni ukweli wa kwanza.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Fumbo mfumbie mwerevu

Mtoto ni nani?

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1