Udhaifu wa sayansi (2)


NIMEKWISHA kueleza kuwa sayansi si njia bora sana ya kuelezea masuala nyeti. Wanaofikiri kwamba sayansi ndiyo hitimisho la ufahamu, ninathubutu kusema kuwa wanakosea sana.

Katika kuthibitisha madai haya, naomba kama nilivyoahidi, kukuletea mifano halisi.

Tuanze na mwanasayansi maarufu katika elimu ya mada na tabia zake, bwana August Kekule. Huyu bwana (hapa pembeni) aligundua kile kinachoitwa benzene. Benzene ina umbo hili hapa kwa chini kama huwahi kuisikia. Mdude huu ni muhimu sana ( samahani sina Kiswahili chake) katika organic chemistry.


Kekule ndiye aliyeugundua mdude huu wa ajabu ambao leo hii umeleta mabadiliko makubwa katika ufahamu wa mambo ya madawa na kadhalika. Itoshe kusema Benzene ni sehemu muhimu ya elimu ya viini mwili.


Mvumbuzi wa umbo hili, Bw. Kikule hakuficha ukweli kwamba hilo umbo la benzene alilipata kwenye NJOZI. Huruhusiwi kushangaa. Hakufanya jaribio maabara, hapana, bali aliliota katika ulimwengu wa ndoto! Kuna watu wanadhani nimetia chumvi ili kuiongeza nguvu hoja yangu. Subiri kidogo:


Ilikuwa ni mwaka 1898, alipokuwa akitoa mhadhara wa “kitaaluma” uliopewa jina la Kekule Memorial Lecture huko London. Hiyo ilikuwa ni baada ya umaarufu wake kupanda alipogundua benzene mwaka 1865. Kwa maneno yake mwenyewe, Kekule aliwaambia wasikilizaji wake ( hawa ni mabwanyenye wanaojiita eti Jamii ya Kikemia London) kama ifuatavyo na ninanukuu:


“…Nilikuwa nimekaa, nikiandika katika kitabu changu, lakini ikawa kama vile kazi haiendelei, mawazo yangu yalikuwa yamehama. Nikasogeza kiti changu katibu na moto, nkalala…Katika njozi nikaona madude kama atomi yanazunguka na kujinyonga nyonga kama nyoka vile…basi nikaamka; na nikautumia usiku wote uliobaki kumalizia bashiri hiyo (akimaanisha kuichora benzene kama alivyoiona ndotoni)…”


“Ndugu zangu tujifunze kuota” akaongeza Kikule. “Kwa kufanya hivyo, labda tunaupata ukweli…lakini tusije tukajikuta tunachapicha njozi kabla halijathibitishwa na ufahamu wa kawaida… ” Tafsiri isiyorasmi kutoka kitabu cha David E. Lewis, Organic Chemistry, a Modern Perspective, Uk 710.


Njozi za Kekule zilikuwa na nguvu ya aina yake. Na kwa hakika ndizo zilizosababisha “tafiti” (mimi nadhani ni njozi nyingine za mchana) za kupata umbo linalokubalika zaidi. Watu kama akina Claus (1867), Ladenburg (1869), L. Mayer (1884) na Thiele (1899) nao walijaribu kupendekeza maumbo yao, na baadae lile lililootwa na Kekule ndilo lililokubalika zaidi baada ya marekebisho madogo. Kwa maneno mengine, njozi zilishindanishwa, na iliyoshinda ikawa ni ile ya Kikule.



Si hivyo tu, sehemu kubwa ya Kemia, imejengwa kwenye “ulimwengu wa kufikirika zaidi na/au nadharia” kuliko uhalisi. Na ukiangalia kwa miwani kali utaona, kama nilivyokwisha kusema, kwamba sayansi inakuwa zoezi la kutafutia ushahidi wa maabara, mawazo ya kawaida, kwa jina zuri, eti utafiti.


Pamoja na kusema hivyo, naomba nisieleweke vibaya. Silengi kudai kuwa sayansi haina maana. Sikusudii unielewe kimarienge kuwa sayansi haina maarifa. La hasha. Ninaelewa kuwa sayansi imesaidia kubaini mambo ambayo hayakuwa yanabainika kabla. Yapo mengi. Ingawa sidhani kama ni sahihi kusema huo ni ugunduzi kwa maana halisi ya ugunduzi. Kwa hiyo kama ambavyo, uchawi wa Sumbawanga na Tanga unavyosaidia watu kwa maana hii na ile, sayansi nayo kwa maana hiyo hiyo, imesaidia-saidia.


Ndio. Imesaidia sana. Imesaidia kuwa kichaka cha mawazo ya binadamu wenzetu wanaojifanya wanafikiri zaidi yetu.


Najua fika hutakubaliana na mimi mpaka hapo. Huo ni ushahidi wa wazi wa nguvu ya wanasayansi.Tutaendelea.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia

Uislamu ulianza lini?