Kikao cha tathmini na mipango ya familia
Wiki hii mimi na familia yangu tulikuwa na kikao cha ‘halmashauri kuu’ ya mwaka. Kikao chenyewe kililenga kujitathmini sisi kama familia na kujiwekea malengo ya pamoja kwa mwaka 2023. Kikao hiki kinatarajiwa kufuatiwa na kikao cha 'Kamati Kuu.' Maandalizi ya kikao hiki cha 'banguabongo' yalifanyika kwa kupeana dondoo za kufanyia kazi agenda za kikao. Hatimaye siku ikawadia. Jioni ya Jumapili ya Desemba 25, 2022. Tukiwa eneo tulivu mbali nyumbani, baada ya mwenyekiti wa kikao kueleza kwa nini tumekutana, shughuli yenyewe ikaanza. Agenda ya kwanza ilisomwa na mtoto wetu wa kwanza, “Kitu gani ulichofanya mwaka huu kinakufanya ujisikie fahari?” Tukatakiwa kuandika kwenye vikaratasi vidogo tulivyokuwa tumegawiwa tayari. “Tumieni vikaratasi vya kijani. Mambo matano makubwa yaliyokufanya ukajisikia fahari kwa mwaka huu.” Baada ya kila mmoja kuorodhesha mambo yake matano yaliyomwendea vyema mwaka huu, mtoto wa pili akakusanya vikaratasi vyenye majibu na kuvibandika kwenye u...