Inaanza na wewe...
TUMEKUWA maarufu kwa kuwalaumu watu wa mabara mengine kwa umasikini wetu. Tunatumia muda mwingi kuorodhesha visingizio. Kwamba ni ukoloni ndio umeyatenda yote haya, huo ndio umekuwa wimbo wa kurithisha vizazi na vizazi. Sitetei wakoloni. Lakini hebu na tufikiri. Kama matatizo yetu yanauhusiano na ukoloni huo, mbona, miaka hamsini baada ya kile kinachoitwa uhuru, hali imebaki pale pale? Kama kweli umasikini wetu una harufu ya ukoloni, mbona leo hii, tunausomba ukwasi tulionao kuupeleka ughaibuni? Halafu baadae tunaufuata huko huko kwa jina la misaada ya hisani? Linaelezekaje hili? Miaka hamsini ya kujitawala, bado waafrika weusi hawataki lugha zao. Wanafundishana mambo ya hao wanaowalaani kwa lugha za hao hao! Wanaongea wao kwa wao kwa lugha za kuazima! Ndugu zangu, sababu ya umasikini wetu ni akili zetu.