Lugha ni nyenzo muhimu sana tunayoihitaji katika maisha. Hatuwezi kufikiri vizuri, kuongea kwa ufasaha, kusikiliza, kueleza mambo tuliyokutana nayo na hata tunayoyatarajia siku zijazo bila kuhitaji lugha. Ni wazi tunalazimika kutumia maneno au ishara kuwasiliana na wanaotuzunguka. Mjadala wa namna gani mtoto hujifunza lugha ya mama una historia ndefu. Kwamba mtoto huzaliwa na asili ya lugha inayoongoza namna anavyojifunza lugha au ni mazingira anayokulia ndiyo yanayomwezesha kujifunza, ni vigumu kuhitimisha kwa hakika. Hata hivyo, kuna ukweli kwamba ili mtoto ajifunze lugha ipasavyo anahitaji kuwa na uwezo fulani anaozaliwa nao unaomwezesha kuelewa kanuni muhimu za lugha bila msaada mkubwa. Lakini pia mazingira, anayokulia mtoto, nayo yana nafasi kubwa ya kumwezesha kujifunza na kumudu lugha ya kwanza kirahisi.