Amana ya ‘nguvu zangu’

Hivi majuzi, nilipata fursa ya kula pasaka nyumbani kwetu, Singida. Katika niliyoyafanya, ni pamoja na kukagua ‘maktaba’ ambayo mzee wangu alitutengenezea chumbani kwetu. Ni kijishelfu kidogo ambacho alikitumia enzi hizo kutuwekea vitabu kadhaa kila mara na kutuhimiza kuvisoma. Pamoja na vitabu, humo aliweka nakala za magazeti ya Rai ile ya zamani na mengineyo. Na kweli tuliyasoma, mimi na mdogo wangu.




Namshukuru baba yangu kwa hilo. Maana nakumbuka alinifanya nianze kugharamia nakala za magazeti tangu nikiwa kijana wa darasa la sita na saba. Niliweza kubana matumizi ili kumudu kununua gazeti hilo kila wiki. Ndio ulikuwa ulevi wangu.

Pia nimshukuru kwa sababu alinijengea ari ya kuiba vitabu kila nilikopita. Ujue kila mtu hukumbuka siku zile za ‘adolesensi’ kwa jinsi yake. Wengine kwa idadi ya wasichana aliowatongoza. Wengine kwa michezo ya ‘baba na mama’. Na kadhalika. Mimi huzikumbuka zaidi kwa wizi wa vitabu.

Sikuwa na uwezo wa kumudu kununua vitabu nilivyovipenda. Kwa hiyo suluhisho pekee la wakati huo wa ‘ujanani’ lilikuwa ni ‘kuvivusha’ vitabu hivyo kutoka kwenye shelfu za umma kwenda kwenye shelfu ya chumbani kwangu. Hata sikumbuki nilikuwa nawezaje kutoka na vitabu kwenye maktaba za mkoa na shule nilikosoma. Kilikuwa ni kipaji fulani hivi cha pekee.



Vitabu vingi vinaonekana kwenye shelfu hili ni matokeo ya ‘nguvu zangu mwenyewe’ zilizolenga katika kujenga mtaji wa usomaji wa kujitegemea na wa ujamaa wa kweli. Ujamaa kwa sababu sikuacha kuwapa rafiki zangu nao wajisomee japo wengi nao walitoroka navyo mpaka leo.

Kwa hiyo nilipolitazama shelfu lile la chumbani kwetu siku chache zilizopita, nilijikuta nikiikumbuka dhambi hiyo ya 'ujizi'. Picha hii ni ishara ya kukiri kwangu.

Na juzi nikiwa nyumbani nililikabidhi shelfu hilo kwa bwana mdogo wa mwisho aliyeridhi chumba hicho na ‘amana’ zilizomo. Bila shaka hajarithi dhambi ya sisi tuolikuwa wakazi wa chumba hicho miaka ya tisini mwishoni.

Maoni

  1. Kaka Bwaya leo umenikumbusha kukiri jambo moja. Katika maisha yangu ya adolescent nilishiriki jambo hilo kupindukia. Kulikuwa na vitabu vingi nilivyihitaji kuvisoma, lakini nisingeweza kumudu gharama. Hivyo nililazimika kuficha kitabu kwenye sweta ama koti ama kama ni kidogo kwenye buti langu la Timberland ilimradi nijipe uhakika wa kusoma kitabu. Sasa nami najivunia hamu ya kumiliki vitabu imenifanya kuwa mnunuzi mzuri wa vitabu na magazeti makini hadi sasa.

    JibuFuta
  2. kaka Bwaya kumbe babako yupo kama babangu naye mwaka jana alinishangaza kweli pale alipoingia ndani na kutoka na vitabu ambabyo mimi nilivisoma nilipokuwa darasa la kwanza kwa mfano juma na Roza, Bwana matata hajui kusoma sikui kilisoma darasa gani? Akawakabidhi wajukuu zake kwa hiyo na sisi hapo tunameanzisha maktaba yaani kiswahi. Ahsante.

    JibuFuta
  3. KUMBE KWENYE UFISADI WA VITABU TUPO WENGIIIIIIIIIIIII

    JibuFuta
  4. Mimi nakumbuka nilikuwa nafanya vibiashara uchwara enzi zile na nikipata vihela, mbali na kununua vitumbua na pipi, nilikuwa natafuta kitabu kizuri na kukinunua.

    Wakati ule riwaya pendwa zikitamba, nilikuwa nafanya kila njia ili kuhakikisha kwamba nina vitabu vyote vya akina James Bond wetu - Willy Gamba wa riwaya za Musiba na Joram Kiango wa riwaya za Marehemu Ben Mtobwa; pamoja na Sherlock Holmes(Bwana MUSA wa riwaya za Muhammed Said Abdulla - na hasa Siri ya Sifuri) na wengineo. Na kila ilipowezekana kudokoa basi hakukuwa na kizuizi.

    Kwa bahati mbaya maktaba yangu yote ililiwa na mchwa kule kijijini kutokana na uzembe wa niliyekuwa nimemkabidhi. Ndiyo maana nilipopata nafasi kidogo nilikasirika na kuamua kujenga kibanda ambacho hakitashambuliwa na mchwa kirahisi...

    Dada Yasinta, nitakutafuta ili nione uwezekano wa jinsi ya kuvipata hivyo vitabu vya darasa la kwanza....

    JibuFuta
  5. Makala hii nimeiona kuwa nzuri sana, na imeandikwa namna ya kusisimua. Imenifurahisha sana. Namheshimu sana Mzee Bwaya kwa busara zake za kuhakikisha watoto wake wanakua katika utamaduni wa kusoma vitabu. Katika blogu zangu, nimelalamika miaka yote kuhusu suala kufifia utamaduni wa kusoma nchini mwetu, na taarifa hii inaleta faraja.

    JibuFuta
  6. Hivi ulikuwa wapi na uko wapi siku hizi wewe!
    Unajua hata sie nyumbani baba anayo maktaba yake ambayo ndiyo inayoniwezesha kuandika ujinga wangu pale Vukani...LOL

    Umenifurahisha sana kaka.

    lakini ninalo swali...
    Mbona hayo magazeti na vitabu vyaonekana bado ni vipya?

    maan makataba yetu vitabu ba magazeti yamebadilika rangi na kupoteza ule muoenakano wake halisi, na hata hata vitabu navyo mwe!
    habu nijuze umetumia teknolojia ganikuhifadhi?....LOL

    JibuFuta
  7. Nimevutiwa na swala hili la 'wizi wa vitabu' na najiuliza hadi sasa ni wangapi wanaofanya hivi kwenye maktaba za mikoa,maktaba za shule na hata za watu binafsi na ni wangapi wakosao vitabu hivi viibwavyo na ambavyo vingewaongezea na hari ya kuzidi kusoma vitabu. Ni dhahiri kuwa wizi wa vitabu unakwamisha sana hari ya usomaji hususani kwa wale ambao vitabu muhimu vinapopelekwa mbali na upeo wa macho yao.


    Si wote wenye uwezo wa kununua vitabu na pia suluhisho si kuiba na wizi wa vitabu usihalalishwe kuwa ni wa kawaida kwa sababu aibae ni msomaji mzuri.


    Ndugu Bwaya na wengine,kuelezea tu kuwa mlikuwa "mnadokoa vitabu" haitoshi. Hamna budi panapo uwezo mzuri,mpate kuendeleza maktaba za shule,mikoa na nyinginezo kwa kuziwezesha kwa kuzipatia vitabu vinavyokwenda na wakati na mzidi kukemea hali hii kwani wapo wengi wanaoumia kwa kukosa vitabu muhimu na wavipendavyo.


    Kibaya zaidi,vitabu ambavyo huwa vinaibiwa ni vile vilivyo vichache,venye kupendwa na upatikanaji wake huwa ni mgumu.


    Ni hayo tu.

    JibuFuta
  8. Asanteni nyote kwa maoni yenu yanayosisimua.

    Niwe mahususi kwa

    Koero, sehemu niliyoipiga ilikuwa na magazeti ya si zaidi ya mwaka jana. Angalia vipisi vya magazeti vya makala za mwaka 2006 uone vilivyochakaa.

    Kisima, umesema jambo la msingi. Wezi wa zamani, tunalo jukumu la kuhimiza zaidi usomaji. Kwa kuwa tuliiba kwa kutokuweza kununua, basi tuna wajibu zaidi pale tulipopunguza kwa nia ya kukidhi kiu ya kusoma.

    JibuFuta
  9. Nakumbuka nikiwa shule ya msingi nilikuwa na vitabu vingi vya ZIADA kuliko vya KIADA. Nilikuwa mwanachama mzuri wa maktaba ya mkoa. Na nilipenda zaidi kusoma habari nyingi nje ya shule. Nilikuwa ninafuatilia sana jinsi dunia inavyokwenda. ILA HALI HIYO ILIKUWA INAKWENDA HUKU IKIPUNGUA. Galfa nikawa mfuatiliaji tu wa vitabu vya shule(KIADA) kuliko vingine. Na hali ilizidi kubadilika nikiwa high school. MITIHANI ILITUNGWA KUPIMA UWEZO WA KUKARIRI ZAIDI KULIKO KUJUA MAMBO, hapa ndipo nilianza kusoma "past papers" na nikapoteza kabisa "HOBI" ya ku "update" Library yangu.
    NINAHISI PIA MFUMO WETU WA ELIMU UNACHANGIA SANA KUPOTEZA MSINGI WA WATU KUPENDA KUJISOMEA. sioni mantiki ya mtoto wa kidato cha kwanza mapka cha nne kukaririshwa masomo zaidi ya tisa. NA WALIMU WANATUNGA MITIHANI INAYOMSUKUMA MTU KUKARIRI. na ukijaribu kujibu kwa kuelewa na kunukuu vitabu vingine mwalimu asivyovijua ELEWA KUWA UTAFELI SOMO HILO.
    Kama mwalimu mwenyewe hana utamaduni wa kujisomea unadhani mwanafunzi ataupata.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia

Uislamu ulianza lini?