Madikteta wa Familia Tunaweza Kudai Demokrasia?

Madai kuwa baadhi ya watawala wetu wa ki-Afrika ni madikteta hayashangazi. Inasemekana watawala hawa  hawasikilizi maoni ya watu wanaowaongoza, hawashauriki wakati mwingine na watu walioteuliwa kuwashauri, wanaminya uhuru wa maoni/kujieleza na kadhalika. Madai haya yanaonekana kuwa ni matamanio ya wananchi kuwa na serikali zinazoheshimu demokrasia -nguvu ya wananchi kushiriki katika uongozi/utawala wa taifa lao kwa kuamua utaratibu gani utatumika kujitawala na nani anaweza kupewa jukumu la kuwaongoza. Haya yote yanadai ushirikishwaji wa wananchi kwa kukuza uhuru wa kila raia kusema/kutoa maoni na kadhalika.


Naomba kujenga hoja kwamba ili tuweze kujenga uhalali wa kudai demokrasia ni muhimu sisi wenyewe tuoneshe mfano wa kuwa wanademokrasia kweli.  Ninatumia dhana kwamba, mara zote, utawala wa nchi ni sura halisi ya utamaduni wa wananchi wake. Kwamba viongozi/watawala wa nchi hubeba tabia/ na hulka za jamii wanazoziongoza. 

Haiwezekani kutarajia watawala wawe tofauti na wananchi wanaowaongoza kwa sababu utawala wa nchi huzaliwa na wananchi. Ndio maana, kwa mfano, wananchi wanaothamini elimu, hutafuta na kuchagua miongoni mwao viongozi wanaothamini elimu kama wao. Kinyume chake, wananchi wasiothamini elimu (wajinga) huweza, na kwa kweli hufurahia, kuchagua wajinga wenzao kuwa watawala wao. Kadhalika, wananchi wanaopenda njia za mkato kujipatia kipato, huthamini wenzao wajanja wenye kujua kutafuta fedha kirahisi na hatima yake wananchi hawa hujichagulia viongozi wanaokuja baadae kufahamika kama mafisadi. Ndio kusema viongozi hawawezi kuwa tofauti na wananchi.


Tukizitazama nchi zinazosifika kwa demokrasia tunabaini kuwa demokrasia katika nchi hizo ni utamaduni wa wananchi. Demokrasia ni maisha/mila inayoanza kwenye utawala wa familia. Kila mwanafamilia kwa kiasi kikubwa anajengewa mazingira ya kujisikia kuwa na uhuru wa maoni. Mtoto hupewa nafasi ya kufanya maamuzi kwa mwongozo wa mzazi. Mke hupewa fursa ya kushiriki katika maamuzi anayoyafanya mumewe kwa sababu demokrasia katika jamii hizo ni utamaduni unaoanzia kwenye familia na sio matamanio hewa ya kisiasa.


Ninapofikiria madai yetu haya ya kutaka watawala wetu wawe wana-demokrasia, maswali kadhaa yanajitokeza. Ninajiuliza, kwa mfano, tunaweza kweli kudai kuwa sisi ni jamii inayoamini katika demokrasia kuanzia ngazi ya familia? Je, demokrasia ni utamaduni wetu? 

Je, sisi wanaume wa ki-Afrika hatutishwi na kukua kwa demokrasia kwenye ngazi ya familia zetu? Tunawashirikisha kweli wake zetu katika maamuzi bila kuwawekea mipaka? Tunaheshimu maoni ya watoto wetu kama tunavyotaka watawala wetu waheshimu maoni yetu? Ni lini kwa mfano wazazi hukaa na watoto wao kujadili bajeti ya familia?
Familia ikishirikiana kazi. Picha: globalfarmernetwork.org
Pengine ni kweli tunaihitaji demokrasia kwenye vyama nyetu vya siasa na serikalini. Lakini je, tunaweza kuwalaumu watawala/viongozi wanaoonesha hulka za kidikteta kama sisi wenyewe ni madikteta wa familia zetu? Je, sisi madikteta uchwara  wa familia zetu (tusiowapa wake/waume/watoto wetu uhuru wa maoni kwa kuogopa kukosa mamlaka yetu kama wazazi/wanaume) tunaweza kuwa na uhalali kwa kudai hatupendezwi na viongozi wa ki-Afrika wanaoonekana kuwa ni madikteta?

Pengine unauliza, sasa tufanyeje? Tuache kudai demokrasia? Nina mapendekeza njia moja wapo kati ya mbili. Ya kwanza, ili tuweze kujenga taifa linaloamini uhuru wa mawazo kweli kweli, tuanze kujenga demokrasia ya kweli ndani ya familia zetu. Tuanze kuwashirikisha wake zetu katika maamuzi bila kuogopa kuonekana 'tumeshikiliwa'. Tuanze kuthamini na kuheshimu maoni/mahitaji ya watoto wetu na kuyasikiliza. Tujenge taifa la kweli la watu wanaoamini demokrasia.

Tukishindwa pendekezo la kwanza, basi, tuamue kuwa wakweli wa dhamira zetu kuwa sisi ni madikteta uchwara kwa asili. Tuunge mkono udikteta uchwara  wa ngazi ya taifa ambao kwa hakika utakuwa unaakisi utamaduni wa udikteta tuliouzoea katika familia zetu. Taifa ni sura ya familia. Right? Right. 
Twitter: @bwaya

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia

Uislamu ulianza lini?