Kwenda mbele kunahitaji kugeuka nyuma?
Ningependa leo tuone ikiwa inatulazimu kuikumbuka jana ili kuweza kuendea kesho. Maana yapo mawazo kwamba ili tuweze kwenda mbele kwa ufanisi, ni vyema kugeuka nyuma kutathmini tulikotoka. Kwamba ni kwa kutumia historia twaweza kubashiri mwelekeo wetu. Tunaambiwa historia hutuelimisha kuhusu mwenendo wetu na namna mwenendo huo ulivyoweza kutufikisha hapa tulipo. Ni kwa kutumia historia hiyo, inasemwa, twaweza kupata maarifa yatakayotusaidia kujikosoa ama kujizatiti kwa faida ya kesho na kuendelea. Wenye mtazamo huu, wanaamini katika nguvu ya historia katika maisha ya mwanadamu. Kwamba maisha yajayo, hayana miujiza. Ni mwendelezo wa mambo yale yale kwa namna isiyotofautiana sana na haya tunayoyajua. Kwamba maisha yatarajiwayo ni kama mwendelezo wa tamthilia ndefu yenye vipande vingi. Vipande hivi vinategemeana. Tukio la kipande kimoja cha tamthlia, hutupa bashiri ya simulizi za vipande vinavyofuata –pamoja na kwamba badiliko dogo laweza kutokea. Katika kujaribu kutanabaisha hiki ...