Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini
Ufanisi kazini, kwa kiasi kikubwa, unategemea uwezo alionao
kiongozi. Huyu ni mtu mwenye mamlaka yanayompa sauti ya kuhamasisha watu
kujiwekea dira na utaratibu wa kuifikia dira hiyo. Kiongozi anatambulishwa na
uwezo wake wa kuwavuta na kuwashawishi watu makini kutumia vipawa , ujuzi na
uzoefu walionao katika kuwezesha kufikia malengo mapana ya kampuni, taasisi au
kikundi husika.
Tunaweza kusema mengi yanayohusu wajibu wa mfanyakazi lakini
bila kiongozi makini itakuwa vigumu kupata ufanisi unaotakikana. Haiwezekani,
kwa mfano, kuwa na wafanyakazi waliohamasika bila kuwa kiongozi anayejua kuibua
hamasa hiyo kwa watu. Utendaji wa watu unategemea aina ya sauti inayowaongoza
kufanya kazi.
Kama wewe ni kiongozi wa idara, ofisi, kampuni au taasisi yoyote
ikiwemo familia, makala haya yanakuhusu. Ingawa ni kweli tunaweza kuzaliwa na
siha ya uongozi, kiongozi makini hachoki kujifunza namna bora ya
kuwaongoza waliochini yake. Tuangalie sifa nne muhimu kuwa nazo wewe kama
kiongozi.
Kujenga hamasa
Kiongozi mzuri ana tabia ya kuwafanya watu wakajisikia
fahari kufanya kitu bila kusukumwa. Hapa tunazungumzia kuwa na sauti
inayosikika mioyoni mwa wale unaowaongoza. Kinyume chake ni kuwatawala watu kwa
maana ya kuwalazimisha kufanya kitu wasichojisikia kukifanya.
Unaweza kujenga hamasa kwa namna kadhaa. Kwanza, kuwafahamu
waliochini yako kwa majina yao. Kama kiongozi unapokuwa na desturi ya kuongea na
kuwasiliana na watu kwa kuwaita majina yao unawafanya waone unawathamini.
Kuthaminiwa kunaongeza hamasa.
Pili, kutambua kazi na jitihada zinazofanywa na waliochini
yako. Kuna ukweli kuwa zaidi ya mshahara mzuri watu wanatamani kuona kazi
wanazofanya zinatambuliwa na kiongozi wao. Ukijifunza kutambua jitihada za watu
wako utawajengea hamasa ya kujituma zaidi. Kuwa na utaratibu wa
kuwaita wale wanaofanya vizuri zaidi utambue kazi zao. Itisha vikao si kwa lengo
la kuwagombeza watu kwa makosa yao bali kusikiliza maoni yao na kuwapa
mrejesho wa kazi nzuri ulizoziona. Utawaongeza hamasa.
Kujali ndoto za unaowaongoza
Moja wapo ya sifa mbaya zinazotajwa kwa viongozi wengi ni tabia
ya kupuuza maslahi na mustakabali wa watu wanaowaongoza. Kuwachukulia watu wako
kama mashine zisizo na hisia wala malengo ni namna moja wapo ya kuonyesha
unavyowapuuza.
Jambo moja la kuzingatia ni kwamba mafanikio ya taasisi au
kampuni unayoiongoza yanachangiwa na bidii ya watu unaofanya nao kazi.
Ukishindwa kulitambua hilo utakuwa huna sifa za kiongozi anayeweza kuhamasisha
watu kufikia malengo ya kampuni au taasisi unayoiongoza.
Katika mazingira hayo hutafikiria mahitaji ya watu wako kama
binadamu badala yake utatumia muda mwingi kujifikiria wewe na utakuwa mwepesi
kufurahia kuona unaowaongoza wakitaabika na kulalamika.
Ukitaka kufanikiwa kama kiongozi, jifunze kujali utu wa watu
unaowaongoza. Jali maslahi yao badala ya kuwakamua kutumikia maslahi yako
binafsi. Tengeneza mipango ya wazi ya kuwaendeleza kadri ya uwezo wao. Fikiria
unavyoweza kuwasaidia kufikia ndoto zao.
Ukiweza kuwathamini watu wako kwa kauli na matendo, wataheshimu
kazi. Ari na motisha ya wafanyakazi kufikia malengo ya kampuni au taasisi yako,
kwa kiasi kikubwa inategemea kiwango cha imani waliyonayo kuwa unawajali.
Kujiamini na kujifunza
Kiongozi anayejiamini hana wasiwasi na kile anachokifanya.
Kujiamini kunamfanya awe na uhakika kwamba anaiweza kazi yake. Kipimo cha
kujiamini kwako kama kiongozi ni uvumilivu unaposikia mawazo mbadala. Kiongozi
unayejiamini huwezi kuchukulia mawazo tofauti na yako kama uadui. Hutishwi na
uhuru wa waliochini yako kushauri jambo kwa nia ya kuboresha.
Kadhalika, kujiamini kunakwenda sambamba na tabia ya kusema
ukweli. Kiongozi anayejiamini hadanganyi. Inahitaji kujiamini ili uweze
kuwaambia wale unaowaongoza vile mambo yalivyo hasa katika mazingira ambayo
kuficha ukweli kuna madhara kwao.
Kiongozi asiyejiamini, kwa upande mwingine, hujilinda kwa kuwa
mkali bila sababu ya msingi. Hufikiri ubabe na kufoka ndio ujasiri kumbe ni
kuficha udhaifu anaousikia ndani yake.
Pia, kutokujiamini kunamfanya asiruhusu waliochini yake kusema
tofauti na vile anavyofikiri. Kiongozi anapokosa hali ya kujiamini huwa na
shughuli ya kutengeneza makundi ya kimaslahi kazini kwa lengo la kuwa na
vibaraka wanaomsaidia kujua wabaya wake wanafikiri nini.
Ili uweze kujiamini kama kiongozi lazima kweli uwe na uwezo.
Ingawa si lazima uwazidi unaowaongoza, lakini ni muhimu kwako kama kiongozi
kuwekeza kwenye weledi na maarifa. Kuwa kiongozi haimaanishi unajua kuliko
unaowaongoza. Hiyo ikupe unyenyekevu wa kujifunza na kuwa msikivu kwa
wanaokuzidi.
Jiulize ni lini ulijiongezea maarifa kwenye eneo lako la
utaalamu kama kiongozi? Unapata muda wa kusoma vitabu na kuhudhuria semina za
kujinoa kiweledi? Unapokuwa mwanafunzi wa kudumu unajiongeza hali ya kujiamini.
Ujasiri wa maamuzi
Unapokuwa kiongozi maana yake unaijua njia. Waliochini yako
wanategemea maongozi yako uwaonyeshe wapi pa kupita. Hapa tunazungumzia uwezo
wako wa kuona mbali. Kiongozi lazima uwe na maono mapana. Unapokuwa na maono
yanayoakisi malengo na dira ya taasisi au kampuni unayoiongoza, utakuwa na
ujasiri wa kuwashawishi waliochini yako kukufuata. Huwezi kuwa kipofu na ukawa
na ujasiri.
Ujasiri ni uwezo wa kuthubutu kufanya maamuzi yenye maslahi ya
wengi. Kama kiongozi, lazima ujitokeze kuwa mtu wa kwanza kugundua viashiria
vya tatizo na kuwaalika wale unaongoza katika kutafuta ufumbuzi. Unaowaongoza
wanakuwa na ujasiri wanapoona na wewe kama kiongozi wao unao ujasiri huo.
Hulazimiki kuongea ili watu waone kuwa wewe ni jasiri bali namna unavyoongea,
unavyoonekana, unavyowasiliana na watu.
Kinyume cha ujasiri ni kiongozi anayejificha nyakati za matatizo
akisubiri wengine watangulie. Kiongozi dhaifu huogopa kufanya maamuzi mara
nyingi kwa sababu hana hakika na kile anachokisimamia. Kinachompa wasiwasi ni
namna anavyoweza kuonyesha njia ambayo yeye mwenyewe hana hakika nayo. Usiwe
kiongozi wa namna hii.
Asante kwa somo zuri sana
JibuFutaNa hii ni changamoto kubwa sana kwa viongozi Mungubakubariki
Kiongozi bora anasiniliza mawazo ya wenzake nakuyachakata
JibuFutaUmenifunza,mung akubariki
JibuFutaMtazamo wako somo la kuwa kiongozi bora nimeuelewa
JibuFutaBarikiwa sana.