Desturi Zetu Zilivyosaidia Malezi Bora ya Watoto -2
|
NIMEJARIBU kubainisha baadhi ya desturi zilizosaidia kukuza watoto wanaojitambua. Unaweza kusoma makala ya kwanza hapa. Kwa kuanzia, tuliona namna familia zilivyowajibika kumtunza mama aliyejifungua. Mtoto na mama walipata muda wa kutosha kujenga mahusiano ya karibu.
Ukaribu
huu kati ya mama na mtoto haukuishia kwenye kipindi cha uzazi pekee. Hata baada
ya mama kupata nguvu na kuendelea na shughuli nyingine za kawaida, bado mtoto
aliendelea kuwa na nafasi muhimu kwenye ratiba za mama. Ilipolazimu, mama alifanya
shughuli zake akiwa amembeba mwanae mgongoni. Kumbeba haikuwa na maana ya mama kujichosha
bali kumwangalia mwanae kwa karibu.
Nyakati
za jioni zilikuwa fursa ya wazazi na watoto kukaa pamoja. Watoto walikusanyika
kusikiliza hadithi, methali na vitendawili. Desturi hii ilikuwa darasa muhimu lililokuza
ufahamu wa mtoto na kumfunza kuhusu jamii yake na wajibu alionao kama sehemu ya
jamii.
Sambamba na hayo, michezo ilikuwa
sehemu muhimu ya maisha ya mtoto. Jamii iliheshimu hitaji la mtoto kucheza na
wenzake. Katika michezo, watoto hawakutegemea vifaa vilivyotengenezwa tayari
kwa matumizi kama ilivyo leo. Vifaa vingi vilitengenezwa kwa kutumia vitu vya
kawaida vinavyopatikana kwenye mazingira yao.
Nakumbuka nilipokuwa mtoto, tulitumia
maboksi na gundi za asili kutengeneza magari ya kuchezea. Tulicheza mpira kwa
kutumia mpira uliotengenezwa kwa mchanganyiko wa nguo kuu kuu na makaratasi.
Tuliruka kamba, tulichora kwa kumtumia mikaa na chokaa na bado tulifurahia
michezo.
Watafiti wengi, akiwemo Christine
Tamis-LeMonda, wanatuambia kwamba mtoto anapotengeneza vifaa vyake mwenyewe kwa
ajili ya michezo au shughuli nyingine, anajenga uwezo mkubwa wa kufikiria na
ubunifu.
Katika makala haya, tunaangalia
desturi nyingine nne zinazoweza kutukumbusha wajibu wetu katika ulimwengu wa
sasa.
Kushiriki kazi za mikono
Mtoto wa ki-Afrika alishiriki kazi
za mikono tangu akiwa mdogo. Kazi zilikuwa sehemu ya maisha ya kila mtu katika
familia. Mama, kwa mfano, alihakikisha watoto wanaanza kutumwa kufanya shughuli
ndogo ndogo za nyumbani tangu kungali mapema. Watoto walifagia nyumba, waliosha
vyombo, walikaa na wadogo zao. Baba naye aliwashirikisha watoto wa kiume kwenye
majukumu ya kuchunga au kutafuta majani ya mifugo inayofugwa nyumbani.
Kufanya hivi haikumaanisha wazazi
hawakuwa na uwezo wa kufanya kazi hizo. Hapana. Lengo lilikuwa kuwafundisha
watoto tabia ya uwajibikaji. Kupitia ushiriki wa kazi za mikono tangu wakiwa
wadogo, watoto walijifunza ujuzi mwingi bila kutumia mtalaa rasmi.
Profesa Bame Nsamenang wa Cameroon,
anatuambia utamaduni huu umeanza kufifia katika jamii nyingi za ki-Afrika.
Wazazi wameanza kuwatenga watoto na kazi za ndani na kuwakabidhi watu wengine
shughuli hizo. Matokeo yake watoto wengi wanakosa ujuzi wa maisha ya kawaida.
Familia tandaa
Jamii zetu zilithamini sana uhusiano
na ukoo wa pande zote mbili. Wazazi, wajomba, akina shangazi, mama na baba
wadogo, binamu, wapwa, bibi na babu walikuwa sehemu muhimu katika uhusiano wa
familia. Kufahamiana na kuitambua
familia tandaa lilikuwa ni sharti la msingi kwa kila mtoto.
Wakati mwingine, kulikuwa na
mwingiliano wa kimaisha baina ya familia na familia. Ndugu walisaidiana kwa
shida na raha. Kadhalika, ndugu walitembeleana mara kwa mara. Binamu, kwa
mfano, angeweza kwenda kuishi kwa baba mdogo, shangazi, bibi na babu kwa muda
fulani. Shangazi, naye angeweza kufunga safari kwenda kuwaona ndugu wengine
walioishi sehemu nyingine.
Mwingiliano huu ulisaidia kuimarisha
mahusiano ya karibu katika jamii. Mtoto alishuhudia uhusiano wa namna hii na
kuuchukulia kuwa sehemu ya maisha yake ya kila siku. Pia, ilimsaidia kuuelewa ukoo
wake na hivyo alijitambua mapema.
Kwa bahati mbaya tumeanza kuipa
mkono desturi hii ambayo imekuwa sehemu ya utambulisho wa jamii yetu kwa muda
mrefu. Uhusiano na familia tandaa umeanza kufifia. Watoto wa siku hizi
wananyimwa fursa ya kufahamiana kwa karibu na familia tandaa. Hawaoni wazazi
wakitembeleana na ndugu wengine wa ukoo. Hawaoni mawasiliano ya karibu na ndugu
wengine. Hali hii inawazoeza kuwa mbali na ndugu zao.
Mtoto alikuwa wa kijiji
Mbali na familia tandaa, malezi ya
mtoto hayakuwa jukumu la familia pekee. Mtoto alikuwa mali ya jamii nzima. Kila
mwanajamii alijiona ana wajibu katika malezi. Ushiriki huu wa kijiji chote
katika malezi ulisaidia kurahisisha kazi ya kuchunga mwenendo wa watoto
wanapokuwa mbali na nyumbani.
Mtoto aliyekwenda kutafuta kuni, kwa
mfano, hakuwa na uhuru wa kufanya chochote alichotaka. Macho yaliyomtazama
yalikuwa mengi. Ikiwa mtu angemwona mtoto anakosa nidhamu njiani, hakusubiri
kuomba ruhusa ya wazazi wake kumwonya. Alijua mtoto ni mali ya kijiji kizima na
jukumu la malezi ya watoto kijijini ni la kila mtu.
Imani hii, kwa kiasi kikubwa,
ilisaidia kuwafanya watoto wawajibike kuonesha mwenendo mwema kwa kila
mwanakijiji. Hapakuwa na fursa ya kukwepa adhabu kwa kile alichokifanya hata
kama alikuwa mbali na wazazi wake.
Jando na unyago
Jamii zetu zilikuwa na mfumo rasmi
wa mafundisho maalum kwa ajili ya watoto wanaopevuka kimwili. Balehe haikuachwa
ipite hivi hivi. Watoto wa kiume, kwa mfano, wafanyiwa tohara iliyoambatana na
utaratibu wa kuwafunza kuelewa nafasi yao kama wanaume wanaotegemewa na jamii.
Pia, katika jamii nyingine, kipindi
cha tohara kilikuwa ni fursa ya kuwafundisha watoto wa kiume ujasiri. Mtoto alitakiwa
kuthibitisha kuwa yeye ni mwanaume anayeweza kugemewa katika jamii.
Mtoto wa kike naye hakuachwa nyuma.
Ingawa hatuungi utamaduni wa tohara kwa wanawake, kazi ya kumfundisha binti
majukumu yake kama mwanamke anayejitambua ilikuwa muhimu. Katika kipindi cha
mpito kuelekea utu uzima, msichana alisaidiwa kujua yeye ni nani na jamii ina matarajio gani kwake.
Kwa ujumla destruri kama hii
ilisaidia kuwaandaa vijana timamu, wanaojielewa na kufahamu wajibu walionao
katika jamii.
Ni kweli kabisa mwalimu wangu hili limekuwa tatizo kubwa kwa kizazi chetu ,nakumbuka nikiwa nyumbani kwetu kijijini niliwahi kuadhibiwa barabarani nikiwa darasa LA tatu kwa kutoroka shuleni na kuingia mtaani nikiamini wazazi hawataniona badala yake nilikutana na mwanakijiji mmoja akanihoji kidogo alipoona sina hoja alinitandika viboko na kunirejesha shuleni na kunikabidhi kwa mwalimu .
JibuFutaSitaweza kusahau tukio hilo ambalo nililiona kama LA ajabu kipindi hicho nashukuru umenikumbusha tena Leo .kwa kweli jamii yetu ilikuwa na uwajibikaji sana siuoni tena uwajibikaji kama huo kwa sasa, ubarikiwe sana mwalimu wangu
Ahsante Sana Mr Christian Bwaya Hii Ni dhahiri kweli kutoshirikishwa kwa watoto katika kufanya mambo ya ubunifu kunarudisha Rate na mbinu za kujifunza maarifa Shukrani kwa kuielimisha jamii na Umma
JibuFuta