Hakuna Ulazima wa Kushinda Kila Majadiliano
PICHA: Elly Prior |
Chukulia mnajadiliana jambo na
rafiki yako. Inaweza ikawa ni mtandaoni, nyumbani, ofisini au mahali kwingineko.
Katika mazungumzo yenu unabaini hamuelewani. Kile unachoona ni sahihi, sivyo anavyoona
mwenzako. Kila mmoja wenu anajaribu kutetea upande wake kuliko anavyoelewa mtazamo
wa mwenzake.
Unadhani kipi ni sahihi kufanya
katika mazingira hayo? Je, ni busara kuendelea kuthibitisha ulivyo sahihi hata
kama ni dhahiri mwenzako hayuko tayari kukuelewa? Unajisikiaje mwenzako
akikuonesha haukuwa sahihi?
Mara nyingi tunafikiri kushindwa na
kutokuwa sahihi ni udhaifu. Tunapambana na wasiotuelewa kwa mabishano na majibizana
kwa lengo tu la kuonesha tulivyo kwenye upande sahihi.
Unazungumza ili kushinda?
Nakumbuka siku moja nilishiriki
mjadala mmoja kwenye mitandao ya kijamii. Katika mjadala huo, kulikuwepo na
pande mbili zinazotofautiana kimtazamo. Kadri mjadala ulivyoendelea, niligundua
hapakuwa na jitihada za pande mbili hizo kuelewana. Kila upande ulisimamia hoja
zake kwa lengo la kushinda ‘mdahalo’ badala ya kupata mtazamo mbadala.
Ndivyo tunavyofanya hata
nyumbani. Tunapoongea na wenzi wetu, wakati mwingine, ndani yetu tunatafuta
kushinda. Tunafikiri kushinda ndio alama ya uimara na msimamo. Mume anajenga hoja
kutafuta ushindi na mke naye anajitetea kutafuta kusikika. Kila mmoja
anazungumza ili ashinde. Hakuna anayetafuta kumweelewa mwenzake.
Kushinda kunabomoa
Mazungumzo ya kutafuta mshindi
hayaleti uwezekano wowote wa maelewano. Mara nyingi mazungumzo ya namna hii huenda
sambamba na hisia. Katika mjadala nilioutaja hapo awali, mwisho wa mjadala ule
wa mtandaoni washiriki waliishia kuzodoana, kusemana na kuitana majina. Hakuna
aliyekuwa tayari kushindwa kwa sababu lengo lilikuwa ni kushinda.
Kwa kawaida, mtu anayetafuta
ushindi anapogundua anashindwa ni rahisi kukasirika. Hasira ni silaha ya
kujihami na fedheha ya kushindwa. Bahati mbaya, watafiti wanasema, unapokuwa na
hasira huwezi kujishughulisha kuelewa mwenzako anafikiri nini.
Pia, kushinda kunaweza kuwa
chanzo cha maumivu makubwa ya kihisia kwa anayeshindwa. Kwa kawaida, anayetaka kushinda hawezi kujali hisia za
mwenzake. Lengo lake ni kumdhibiti mwenzake kwa gharama yoyote hata ikibidi kwa
kejeli na dharau dhidi ya hoja na utu wa mwenzake.
Ushindi unaopatikana katika
mazingira kama haya haujengi. Wakati aliyeshinda akifurahia kuwa sahihi,
aliyeshindwa anabaki na majeraha moyoni. Kwa kuwa kushindwa ni adhabu kwa wengi
wetu, ushindi unaishia kutengeneza kiambaza cha kihisia kati ya aliyeshinda na
aliyeshindwa.
Tujiulize, je kuna ulazima
kushinda kila unapojadiliana jambo na mtu mnayetofautiana? Kama ni lazima,
haiwezekani nyote wawili kushinda? Kama wote kushinda haiwezekani, hamwezi kujadiliana
bila kutafuta mshindi?
Ushindi ni kusikiliza
Najaribu kufikiri uwezekano wa
mtu kusema kile anachofikiri ni sahihi bila kumlazimisha mwenzake afikiri kama
yeye. Naamini hili linawezekana. Lakini ili iwezekane, ni muhimu mtu huyu awe
tayari kusikiliza kile kinachosemwa na mwenzake akifahamu kuwa na mwenzake naye
anaweza kuwa sahihi kwa namna yake.
Najua yapo mazingira watu
hulazimika kuwashawishi wengine kufuata upande wanaofikiri ni sahihi zaidi.
Lakini ushawishi huu unakuwa na tija ikiwa unafanyika katika mazingira ya
kirafiki. Ushawishi unaofanywa bila kutumia nguvu, bila kupuuza mtazamo wa anayeshawishiwa,
una nafasi ya kujenga zaidi kuliko ushindi unaopatikana kwa mabavu na ujuaji.
Kuna nyakati ushawishi mzuri zaidi
ni kushindwa. Kama unayeshindana naye haonekani kuelewa, mwache ashinde. Unapomwacha
mwenzako unayefikiri hayuko sahihi ashinde, unampa nafasi ya kujiona
anaheshimiwa. Mtu akishakukuheshimu, anaweza kukusikiliza vizuri wakati mwingine
mtakapozungumza.
Maoni
Chapisha Maoni