Mwalimu Anavyoweza Kukuza Udadisi kwa Wanafunzi -2
PICHA: The East African |
MWALIMU anabeba wajibu muhimu wa kuhakikisha
mwanafunzi anajenga ari ya kujifunza maudhui kama yaliyoainishwa kwenye mtalaa.
Mwalimu aliyeandaliwa vyema na kufuzu kazi ya kutafsiri mtalaa katika maisha ya
mwanafunzi, anaweza kuibua na kuchochea udadisi kwa mwanafunzi.
Katika makala ya kwanza tulitumia mfano
wa mradi wa Next Generation Leaning (NGL) unaoendeshwa na Shirika la Opportunity
Education kujifunza namna mwalimu anavyoweza kuifanya kazi hii kwa ufanisi.
Tuliona kanuni mbili. Kwanza, mwalimu anahitaji kumfanya
mwanafunzi aone namna gani kile anachofundishwa darasani kinagusa maisha yake
ya kawaida. Kujua uhusiano uliopo kati ya maudhui anayojifunza na maisha yake,
kunamfanya athamini maudhui husika na hivyo kuwa na ari ya kujifunza. Pili, mwalimu
anahitaji kumjengea mwanafunzi uwezo wa kujiuliza maswali ya msingi kuhusu maudhui
anayojifunza. Kanuni hii inamsaidia mwanafunzi kupunguza utegemezi kwa mwalimu na
hivyo kujenga hali ya kujiamini kuwa anaweza kushiriki kwenye mchakato wa
ujifunzaji. Kujiamini ni msingi muhimu wa udadisi wa mtoto.
Kanuni
ya tatu ni kujenga ujuzi. Mwanafunzi wa NGL anatarajiwa kutumia maarifa anayojifunza
kuzalisha. Tunafahamu walimu wengi katika shule zetu huwatarajia wanafunzi
kukusanya na kukariri maarifa. Kipimo cha ujifunzaji siku zote kimekuwa ni kwa
kiwango gani mwanafunzi anajua maelezo sahihi ya nadharia. Mwanafunzi anayesoma
mada ya Uchafuzi wa Mazingira, kwa mfano, anatarajiwa kukusanya, kukariri na
kuelewa maelezo mengi kuhusu uchafuzi wa mazingira.
Mwanafunzi
huyu aliyeelewa mambo mengi kuhusu uchafuzi wa mazingira anaweza kuvumilia kuishi
na takataka zilizo karibu na makazi yake bila wasiwasi. Uelewa wa uchafuzi wa
mazingira, haumsaidii kuona tatizo. Kwa mwanafunzi huyu uchafuzi wa mazingira
ni ‘mambo ya shule’ yasiyohusiana na maisha yake halisi. Upungufu huu
unachangia kuwafanya wanafunzi wetu wasijue namna gani wanaweza kutumia kile
wanachokifahamu katika maisha halisi.
Katika
zama hizi za ukuaji wa mawasiliano, maarifa ya kila namna yanaweza kupatikana.
Mtu yeyote mwenye ujuzi wa namna ya kutumia mtandao wa intaneti anaweza kutafuta
na kupata chochote anachotaka kujifunza. Kuendelea kusisitiza kwenye kumbukumbu
ya maarifa kimsingi si kumtendea haki mwanafunzi. Maarifa hayapaswi kuwa lengo
la elimu. Tunahitaji kuongeza thamani kwa kwenda mbele ya maarifa.
Badala
ya mwalimu kumjazia mwanafunzi maelezo mengi, anahitaji kulenga katika kukuza uwezo wa mwanafunzi
kutumia maarifa anayoyapata katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto halisi zinazomkabili.
Uwezo huu unaitwa ujuzi. Mtu mwenye ujuzi anaweza kufanya vitu vinavyoonekana
kama ushahidi kuwa amejifunza maudhui fulani.
Kwa
mfano, katika kufundisha mada ya Uchafuzi wa Mazingira, mwalimu asiishie
kumjaza mwanafunzi nadharia na maelezo mengi yanayohusiana na uchafuzi. Badala
yake, aende hatua moja mbele kwa kumjengea mwanafunzi uwezo wa kuona matatizo
yanayofanana na kile anachojifunza na kujaribu kutafuta majibu yanayolingana na
kiwango chake cha uelewa. Huko ndiko kutumia maarifa kujipatia ujuzi.
Hiki
ndicho kinachofanywa na mradi wa NGL. Tunajifunza kwamba mwalimu aliyeandaliwa
vizuri anaweza kumjengea mwanafunzi uwezo wa kuja na majibu yanayolingana na
uwezo wake. Mwalimu wa NGL, kwa mfano, mbali
na kuhakikisha mwanafunzi anahusianisha kile anachojifunza na maisha yake, anatarajiwa
kukuza ujuzi wa mwanafunzi kwa kufundisha katika namna inayochochea utafutaji
wa majibu. Ufanisi wa somo unapimwa kwa namna mwanafunzi anavyoweza kutazama
nje ya darasa na kubaini matatizo yanayoweza kutatuliwa kwa kutumia maarifa
aliyonayo.
Kanuni
ya nne ni kumwezesha mwanafunzi kujifunza kwa ushirikiano na wenzake.
Tunafahamu kuwa wanafunzi hutofautiana uwezo. Wapo wanafunzi wenye uelewa
mkubwa wa mambo kuliko wengine. Kadhalika, kila mwanafunzi anaweza kuwa na eneo
analoliweza zaidi kuliko maeneo mengine.
Mradi
wa NGL unamfanya mwalimu afikiri namna gani mwanafunzi atashirikiana na wenzake
darasani katika mchakato wa kujifunza. Mwalimu anahitajika kuweka mazingira
yanayomlazimu mwanafunzi kujadiliana na wenzake, kusikiliza mawazo ya wenzake
na kutafuta majibu akiwa na wenzake. Kufanya hivi kunamwezesha mwanafunzi
kufurahia kile anachokisoma kwa sababu ujifunzaji unafanyika katika mazungumzo
ya kawaida.
Ingawa
walimu wetu wamekuwa wakifundishwa mbinu hii ya kuwashirikisha wanafunzi katika
ujifunzaji, mara nyingi utekelezaji wake umekuwa na changamoto nyingi. Walimu
wengi, kwa mfano, hupata shida kujua ni wakati upi mwanafunzi ashirikiane na
wenzake na anaposhirikiana na wenzake afanye nini. Matokeo yake walimu huendelea
kutumia mbinu za kimazoea zinazowanyima wanafunzi fursa ya kushiriki kwenye
mchakato wa ujifunzaji.
Inaendelea
Nzuriiii hiyooooo
JibuFuta