Ufanye Nini Mtoto Anapokuwa Mkorofi?
PICHA: JGI/Jamie Grill |
Pengine una mtoto unayefikiri ameshindikana.
Unamwita mtundu, mtukutu, asiyeambilika, mbishi, mkaidi na majina mengine.
Kikubwa ni tabia yake ya kupenda kushindana. Katika makala haya tunamwita mtoto
mkorofi. Huyu ni mtoto anayeweza kukukatalia kitu bila kupepesa macho na
ukajikuta ukifedheheka.
Unaweza kumwagiza afanye kitu na akabaki
akikuangalia. Hajigusi. Wakati mwingine ni mtoto mwepesi kurusha rusha mikono
na miguu kama namna ya kupinga unachomwelekeza. Anapoamua jambo, anakuwa na msimamo
imara. Ukimlazimisha kufanya asichokitaka yeye unaambulia vilio na vurugu.
Mtoto wa namna hii pia huwa mgomvi anapokuwa na
wenzake. Tabia yake ya kushindana na kila anayekuwa naye inamfanya ajikute
kwenye migogoro ya mara kwa mara.
Mbali na kusumbuana naye hapo nyumbani, inawezekana
pia ni msumbufu hata shuleni. Pengine umepokea malalamiko kwa walimu wake kuwa
hafanyi kazi anazopewa, hatulii darasani na muda mwingi anautumia kugombana na
wenzake bila sababu za msingi. Inawezekana tabia ya usumbufu imechangia matokeo
yake shuleni yasiwe mazuri.
Pia, ukorofi unakwenda sambamba na tabia ya kupenda
kujiona ni mtawala anapokuwa na wenzake. Anaweza kuwa mwongeaji au mkimya
lakini anafurahia kuona wenzake wakifanya kile anachokitaka yeye. Ni aina
fulani ya hulka ya uongozi iliyochanyikana na kutokuelewa wengine wanataka nini.
Upofu wa hisia.
Athari
za ukorofi
Ni vizuri kuzingatia kuwa si kila ubishi ni ukorofi.
Kila mtoto kwa wakati fulani hujaribu kupigana na maagizo ya mzazi. Ubishi ni
sehemu ya udadisi wa mtoto hasa pale anapofikiri kile anachoambiwa hakiendani
na anachotamani. Usichukulie kuulizwa maswali mengi na mwanao kama ubishi au
ukorofi. Mtoto mwenye akili nzuri mara
nyingi hapokei kirahisi kile anachoambiwa bila kukitafakari.
Ingawa kila mwanadamu anahitaji kiasi fulani cha
ukorofi kwa maana ya msimamo wa kile tunachokiamini, tabia hii ya misimamo
inayoongozwa na upofu ikiachwa imee inaweza kuwa kikwazo kwa mafanikio ya
mwanao.
Ukubwani, ukorofi unahatarisha –na hata kuvunja– uhusiano
baina ya watu. Unapokuwa mtu mkorofi, huwezi kujisikia hatia kumwumiza mwezako.
Tena wakati mwingine furaha yako inaweza kuwa kuona wenzako wanaumia. Hakuna
mzazi anatamani kukuza mtu wa namna hii.
Kinachosababisha
ukorofi
Ukorofi wa mtoto ni ujumbe. Ni muhimu uuelewe ujumbe
huu kabla hujachukua hatua za kuushughulikia. Ukorofi ni lugha ya kusema ndani
anajisikia utupu. Ni sawa na mtu aliyeshinda njaa siku kadhaa. Kwa vyovyote
vile ni dhahiri atakosa utulivu. Mwili wake unahitaji chakula.
Mtoto mkorofi kimsingi anaamini watu wanaomzunguka
hawajatambua nafasi yake ipasavyo. Ndani yake mna sauti inayomwaminisha kuwa hatambuliki.
Imani hiyo potofu huchochea jitihada za kutafuta kutambulika kwa namna
isiyokubalika.
Ubishi na ukaidi anaoufanya –wakati mwingine bila
hata yeye kung’amua– ni namna ya kujirudishia mamlaka anayoamini hana. Anapobishana
na mzazi, anapogombana na wenzake, kimsingi anajaribu kujirejeshea ushawishi
ambao anaamini hana.
Mambo mengi yanaweza kuzaa ukorofi. Wapo baadhi ya
wanataaluma wanaamini mtu huzaliwa na ukorofi. Inawezekana. Lakini kwa sehemu
kubwa tafiti zinaonyesha kuwa ukorofi ni zao la malezi.
Hapa kuna mambo makubwa matatu. Kwanza, inawezekana
kwa sababu ya kutamani mtoto ‘anyooke’ umekuwa na sheria kali mno. Unaamini
mtoto hawezi kufanya kitu bila kuamrishwa. Kwa sababu ya kuamini hivyo,
umejikuta ukijenga mazingira ya mapambano yasiyo na sababu. Mtoto mkorofi ni ama anakuiga vile ulivyo au basi anapambana na wewe.
Lakini pili, inawezekana una ukali uliopitiliza. Huwezi
kuongea bila kufoka na kupaza sauti. Huna sauti ya upole inayoleta taswira ya mtu
mwelewa, anayejali, na mtulivu. Unaamini bila kelele hakuna nidhamu.
Aidha, inawezekana mtoto amekuwa akishuhudia vitendo
vya ukorofi katika mazingira ya familia au jirani. Kwa kawaida, watoto wananasa
kwa haraka sana mambo yanayogusa hisia zao. Wanapoona mtu mzima anafanya jambo
fulani na watu anaowaamini wanalichukulia kawaida, wanakuwa na uwezekano mkubwa
wa kufanya kile kile wakati fulani.
Mbinu za
kumrekebisha
Jambo la kuzingatia ni kuwa ukali na mapambano yanakomaza ukorofi. Badilika na amua kuwekeza katika kujenga urafiki kabla hujatarajia
kusikilizwa. Hatuzungumzii urafiki wa siku mbili au tatu. Hapana. Tunazungumzia
urafiki wa kudumu ambao mtoto hatakuwa na sababu ya kuwa na mashaka nao. Kama
tulivyoona, mtoto mkorofi kimsingi anahitaji uhusiano wa karibu na wewe mzazi.
Hata katikati ya urafiki huo, usishangae mwanzoni
bado mtoto akaendelea kuwa mkaidi vile vile. Usikate tamaa. Mpe nafasi ya
kukuamini kwa kujenga urafiki imara. Sambamba na urafiki, punguza amri na
kelele zisizo za lazima. Kumbuka kuwa amri bila urafiki huchochea uasi.
Badala yake jenga tabia ya mazungumzo ya utulivu unaposhughulika
naye. Badala ya kuagiza, jaribu kushirikiana naye. Mwonyeshe kuwa unajali na
kuthamini kile anachokipenda. Huna sababu ya kushindana naye. Katika
mazungumzo, mpe nafasi ya kusema. Mwache aongee yaliyoujaza moyo wake na usiwe
mwepesi kukosoa hisia zake wala kujitetea. Kumbuka kuwa ukorofi wake unatokana
na kujisikia kutokueleweka.
Mpe uzingativu kwa kuacha shughuli unazofanya kwa
ajili yake. Ushirikiano wa kiwango hiki utamchangamsha. Ukiweza kufanya hivi
bila unafiki, mtoto ataanza kukuamini. Kidogo kidogo atabadilika.
Kadhalika, mheshimu kama mtu mwingine yeyote
unayemheshimu. Heshima ina mambo mengi. Usimdhalilishe mbele ya wenzake kwa
maneno au vitendo. Kama kuna sababu ya kumwadhibu, fanya hivyo kwa staha. Kumheshimu
mtoto hakukuondolei mamlaka yako kama mzazi.
Pia, tengeneza mazingira ya kufanya maamuzi
shirikishi yanayoheshimu matakwa yake. Kwa sababu tayari ana ukorofi, mweke
karibu unapotaka atekeleze jambo. Badala ya kumwambia ‘kafanye,’ badili lugha iwe,
‘tufanye’ hata kama hulazimiki kufanya. Inapobidi, hasa kwenye hatua za mwanzo,
shirikiana nae kufanya hicho unachotaka akifanye.
Vile vile, tambua kizuri kipya anachojifunza. Kama,
kwa mfano, ameweza kuacha kubishana unapomwagiza kufanya kitu, usikae kimya.
Tambua mabadiliko hayo hata kama ni madogo. Fahari ya mtoto ni kuona jitihada
zake zinatambuliwa. Kadri unavyomfanya ajisikie kutambuliwa, ataendelea kufanya
bidii ya kukupendeza na hatimaye ukorofi aliokuwa nao utapungua.
Maoni
Chapisha Maoni