Mafanikio Hayamfanyi Mwanamke Anayejitambua Kuacha Wajibu Wake
PICHA: RealClearPolitics |
USAWA
wa kijinsia katika dunia ya leo si suala linalohitaji mjadala. Tunakubaliana
kimsingi kuwa hakuna jinsia bora kuliko nyingine na pia hakuna jinsia
inayohitaji kulipa gharama ya kulinda hadhi ya jinsia nyingine. Mwanamke, anayo
haki ya kupata elimu kulingana na uwezo wake, kufanya kazi anayoiweza, kumiliki
na hata kurithi mali sawa na mwanaume.
Hata
hivyo, mabadiliko haya kimsingi yanakuja na gharama zake. Kwa mfano, mwanaume aliyezoea
kutumia udhaifu wa mwanamke kama ngazi ya kujihakikishia mamlaka yake katika
familia lazima akubali kubadilika. Badala ya kutegemea uduni na unyonge wa
mwanamke, lazima aanze kuchukua hatua za kujitambua.
Kama
tulivyodokeza kwenye makala iliyopita, mwanaume anapojitambua hawezi kutishwa
na mabadiliko yanayomruhusu mwanamke kuwa na haki ambazo hapo awali hakuwa
nazo. Hiyo hata hivyo, haimaanishi kuwa mwanamke hana gharama anayohitaji
kuilipa. Hapana. Mwanamke naye anahitaji kujitambua kwa kuelewa kuwa mafanikio
ya kielimu, kiuchumi na kijamii hayamfanyi asahau wajibu wake kama mwanamke. Nitaeleza.
Tofauti ya majukumu
kijinsia
Mila
na desturi zetu ziligawa majukumu fulani fulani kwa kigezo cha jinsia. Ingawa
ni kweli mgawanyo huu wa kimajukumu wakati mwingine uliigharimu jinsia moja kwa
faida ya jinsia nyingine, bado ulisaidia
kuondoa mgongano wa kimajukumu usio wa lazima.
Tofauti
hii, hata hivyo, ilikuwa na msingi wa kimaumbile. Kwa mfano, maumbile ya mwanaume
yanamruhusu kufanya kazi ngumu kuliko mwanamke. Kwa sababu ya maumbile yake, mwanaume
alifanya kazi za suluba kuhakikisha chakula cha familia kinapatikana. Ndiye
aliyewinda wanyama pori kuiletea familia yake kitoweo. Maumbile yake, kadhalika
yalimpa wajibu wa kumlinda mke na familia yake kwa ujumla. Huo, kwa hakika,
haukuwa upendeleo bali wajibu wa mwanaume kimaumbile.
Sambamba
na shughuli nzito, mwanaume alikuzwa kuwa kiongozi wa familia. Uongozi wa familia
haikuwa suala la kimadaraka bali majukumu mazito ya kuelewa familia yake
inaelekea wapi na nini kifanyike kuelekea huko.
Mwanamke,
kwa upande wake, hakuwa na haja ya kujipatia majukumu haya ambayo kimsingi alijua
si yake. Mwanamke, tofauti na mwanaume, alikuzwa kuamini kuwa yeye ndiye
msaidizi wa mume wake. Kuwa msaidizi maana yake ni kukubali kuwa chini ya
mamlaka ya mwanaume. Mwanamke aliheshimu nafasi ya mume wake kama kiongozi wa
familia.
Kazi
yake kubwa ilikuwa ni kuelea watoto na kutunza familia. Hatuwezi kudhihaki
jukumu hili nyeti. Kazi ya kulea haikuwa ‘shughuli’ ndogo. Ilihitaji moyo wa upendo
na kujituma kwa hali ya juu kuhakikisha kuwa watoto wanapata malezi
yanayostahili.
Kuyasema
hayo hatupendekezi mwanamke asifanye kazi nje ya familia. Hapana. Hoja
tunayoijenga ni kwamba mwanaume na mwanamke walikuwa na majukumu
yasiyoingiliana. Mume alijua kazi yake na mke naye alifahamu kazi yake katika
familia. Hapakuwa na mgongano wa kimajukumu kama ilivyo leo.
Tofauti ya mahitaji
kijinsia
Mahitaji ya mwanamke kimsingi ni tofauti na mahitaji aliyonayo mwanaume kisaikolojia. Tuliwahi
kuzungumzia suala hili. Kwa ufupi, mamlaka na heshima ni hitaji la kisaikolojia
la kila mwanaume. Ndani ya kila mwanaume kuna kiu ya kuheshimiwa kama kiongozi
wa taasisi ya familia.
Mwanamke
wa asili hana hitaji hili. Kwake, kilichomuhimu ni kupendwa. Mwanamke wa
kawaida anahitaji mtu atakayemhakikisha mapenzi ya dhati. Hata kama anaweza
kuwa na kila kitu, bado mwanamke anauhitaji wa mwanaume atakayempenda kwa dhati.
Tofauti
hizi zinafanya uhusiano wa mwanamke na mwanaume kuwa wa nipe nikupe. Wakati
mwanaume anafanya kazi ya kumpenda mke wake, mwanamke naye anafanya kazi ya
kumpa mwanaume heshima anayoihitaji. Utegemeano huu wa kijinsia ndio unaoimarisha
uhusiano wa mwanamke na mwanaume.
Usawa wa jinsia si
kufanana
Dhana
ya usawa wa kijinsia, kwa bahati mbaya, inachukuliwa na wengi kama kufanana
kijinsia. Tunafikiri kwa sababu mwanamke ana haki ya kufanya kazi ambazo hapo
awali zilifanywa na mwanaume basi maana yake ni kuwa kihisia, kiufahamu,
kimatamanio, mwanamke ni sawa na mwanaume. Mtazamo huu unaoendelea kupata umaarifu
katika jamii za kileo unaathiri namna mwanaume na mwanamke wanavyohusiana.
Inapotokea,
kwa mfano, mwanamke anapata mafanikio ni rahisi kwake kujichukulia kama mtu
anayeweza kufikiri na kutenda kama mwanaume. Mafanikio yanampa nguvu ya kuanza
kuhoji uhalali wa mamlaka ya mwanaume. Hufanya hivyo akiamini mafanikio ya
kielimu, kiuchumi na kijamii yanampa uhuru wa kujinasua na ‘utumwa’ wa kuwa
chini ya mwanaume.
Changamoto
ni kwamba mwanaume aliyelelewa katika mila na desturi zinazomtambua kama kichwa
cha familia, hutishika anapoona mamlaka yake yanapinduliwa. Kuhoji uhalali wa
yeye kuwa kichwa ni tishio la wazi wazi la ‘mapinduzi.’ Ni sawa na mkuu wa
ofisi anayeshuhudia wafanyakazi waliochini yake wakipanga kumng’oa. Hawezi kuwa
na amani.
Ndivyo
inavyokuwa kwa mwanaume anapoona mwanamke anataka kuwa na mamlaka kama alivyo
yeye. Inapofikia hapa, uhusiano kati ya mume na mke huanza kuingia dosari
zinazoweza kuzaa misuguano isiyo ya lazima.
Nguvu ya mwanamke
Kunusuru
dosari hii katika mahusiano ni muhimu (soma lazima) mwanamke uliye na mafanikio
ufahamu iliko nguvu yako. Kuwa na fedha, elimu, madaraka havikupi nguvu kwa
mwanaume. Hivyo vyote, kama tulivyoona, vinakupunguzia ushawishi wako kwa
mwanaume. Nguvu uliyonayo inayoweza kumkamata mwanaume ni kujitambua kwa maana
ya kuelewa mahitaji halisi ya mwanaume.
Kujitambua
ni kuelewa kuwa mafanikio yako kielimu, kifedha na kijamii hayapaswi kukushawishi
kujiondoa chini ya mwanaume. Kujitambua ni kumhakikishia mume wako –bila kujali
elimu yake, uwezo wake wa kiuchumi wala hadhi yake– kuwa hana sababu ya kuwa na
wasiwasi na mamlaka yake katika familia.
Pamoja
na uwezo ulionao, jifunze kuwa mnyenyekevu kwa mwanaume unayempenda. Rekebisha
tafsiri yako ya usawa wa kijinsia na usitamani kuwa ‘mwanaume’ kwa sababu ya mafanikio.
Vitendo na kauli zako zioneshe kuwa wewe bado ni mwanamke anayejua mipaka ya
majukumu yake kwa kuwa anatambua nafasi ya mwanaume katika familia.
ni somo zuri sana
JibuFuta