Unavyoweza Kumrekebisha Mtoto Mjuaji Anayejiona Bora
PICHA: Psychology Today |
Kujiona bora ni kujiamini kupindukia. Mtu anayejiamini kupita
kiasi, mara nyingi, anaamini anazo sifa ambazo watu wengine hawana. Unapoamini
unazo sifa za ziada kuliko wengine ni rahisi kuwa na kiburi. Kuamini watu
wengine hawawezi kuwa bora kama wewe kunakufanya uwadharau.
Mtu mwenye kiburi na dharau hupata shida kuishi na watu. Kwa
kawaida, huwaona wengine kama watu wasiojua, wanaopungukiwa kile alichonacho
yeye. Mtazamo wa namna hii humtenga na watu kwa namna mbili.
Kwanza, huwapuuza wengine. Huamini anaweza kufanya mambo yake
mwenyewe bila kupata msaada wa watu. Pili, hana uwezo wa kujua mahitaji ya
wengine. Kutokujua wengine wanajisikiaje inaweza kuathiri namna mtu anavyoishi na
watu.
Kuishi vizuri na watu kunategemea uwiano wa hali ya kujiamini
na kuwaamini wengine. Tunahitaji kujiamini lakini sio kwa kiwango cha kuwa
kiburi. Tunahitaji kujiamini bila kuwapuuza wengine. Ili kujiamini kwetu kuwe
na maana lazima kwende sambamba na kuona thamani ya watu wanaotuzunguka.
Kama ilivyo kwa tabia nyingine nyingi, hatuzaliwi na tabia ya
ujuaji na kujiona bora. Malezi ndiyo yanayotengeneza hali ya kujiona watu bora
kuliko wengine. Namna gani wewe kama
mzazi unamlea mwanao inaweza kuumba kiburi na dharau ndani yake. Katika makala
haya tunaangazia viashiria vya tabia hii, aina ya malezi yanayochangia tabia
hii na hatua za kuchukua kumrekebisha mambo.
Viashiria
Kiashiria cha mwanzo kabisa kwa
mtoto mdogo ni namna mtoto anavyoitikia pale anapoachwa na mzazi wake. Akiwa na
miezi michache pungufu ya mwaka, mtoto wa kundi hili anapoachwa na mzazi wake,
asubuhi kwa mfano, hulia lakini huwa haoneshi msisimko mzazi wake anaporudi
baadae. Tabia hii ikikomaa, mzazi unaweza hata kuondoka na bado mtoto asilie na
ukirudi anaweza asiwe na habari kama umerudi. Maana yake ni kwamba ameamua
kujiondolea ‘presha’ kwa ‘kukupotezea.’
Pili, ni tabia ya kutokuwa tayari kurekebishwa
hasa anapofikia miaka mitatu. Mtoto asiye na kiburi ni mwepesi kukubali makosa
yake. Mtoto wa kundi hili anapoambiwa jambo asilolipenda ni mwepesi ‘kuzira’
kuonesha kuwa hapendi kuambiwa makosa yake. Pia ana imani kuwa anastahili zaidi
ya wengine. Hutarajia upendeleo maalum na hutamani kupata zaidi ya wengine. Ni
mtoto asiyejali wengine kwa sababu kwake kile anachohitaji yeye ndicho chenye
umuhimu.
Katika michezo, mtoto huyu hapendi
kuongozwa. Ingawa si mgomvi kama mtoto mkorofi, lakini hujikuta matatani kwa
sababu anapenda ‘kuwapelekesha’ wenzake. Furaha yake ni kuonekana mjuaji wa karibu
kila kitu na hapendi wenzake wanapojua kuliko yeye. Huamini kile anachokijua
yeye ndicho bora na wengine wana kazi ya kufuata kile anachokijua yeye.
Kadri umri unavyoongezeka, anaweza ‘kujichanganya’
na watu, lakini lazima watu hao waheshimu uwezo na uwezo alionao. Hapendi
kuambatana na watu wanaothubutu kumwambia kile asichotaka kusikia. Kwa hiyo
anapojikuta kwenye mazingira ya ‘wajuaji’ wenzake, huwa ni mtu mkimya
anayependa kufanya ‘shughuli’ zake bila kuingiliwa.
Anapofikia umri wa utu uzima, anakuwa haoni haja ya urafiki
wa karibu na watu. Kwake, rafiki ni yule anayemnufaisha. Kimapenzi, huyu si mtu
mwenye uwezo wa kuelewa hisia zake wala kuthamini hisia za mwenzake. Kukosa
hisia humfanya awe mwepesi kuwaumiza wengine na bado akashangaa inakuwaje mtu
anaumia.
Malezi yanavyochangia
Wapo wazazi wasiopenda ‘kelele’ za
watoto. Tuchukulie mfano mtoto analalamika kuwa amejikwaa na anaugulia maumivu.
Mzazi asiyependa kusumbuliwa anaweza kumnyamazisha mtoto, ‘Hujaumia bwana jikaze!’ ‘Mtoto mzuri haliagi!’ Lengo ni kutuliza
‘kelele’ za mtoto.
Lakini kwa upande wa mtoto, maneno
hayo yanamaanisha kupuuza maumivu yake. Moyoni anajua anaumia lakini anaambiwa,
‘Mtoto mzuri hatakiwi kulia!’ Kwa
kuwa mtoto angependa kuwa ‘mtoto mzuri’ hupata wasiwasi na hisia zake. Anajua
anaumia lakini kukubali ana maumivu aliyonayo maana yake anakuwa mtoto mbaya.
Mzazi akifanya hivi mara nyingi, mtoto
hujifunza kukana hisia zake. Mtoto huanza kuamini kuelezea hisia ni kosa na ni
udhaifu. Hali hii hujenga tabia ya ‘usanii’ wa kuonesha hisia tofauti na vile
wanavyojisikia ndani. Mfano, mtoto anaweza kucheka kwa nje wakati ndani
anaumia. Lengo ni kumfurahisha mzazi.
Lakini kwa asili watoto wanapenda
ukaribu na wazazi. Inaposhindikana kupata ukaribu huo kwa kueleweka hisia zao
wanajifunza ‘kupotezea’ ukaribu na watu. Hali hii inaweza kuwafanya wawe watu
wasiohitaji ukaribu sana na watu. Mtoto anajua kile anachojua ni sahihi
hakieleweki kwa wengine, huanza kujifariji kwa kujidanganya kuwa anajitosheleza
hata akiwa peke yake. Hisia za kujitosheleza zinaanza kujenga ukuta wa kihisia
na watu wengine.
Sambamba na mtoto kuanza kuamini
anajitosheleza jambo la pili linaweza kutokea. Kwa kawaida, wazazi wasiopenda kusumbuka
na kelele ‘huwatuliza’ watoto kwa kuwapa vitu. Mtoto anapolia, kwa mfano, anapewa
midoli na vifaa vya kuchezea badala ya kupewa usikivu. Mtoto hujifunza ‘kuhusiana’
na vitu kuliko watu. Katika mazingira hayo, ili ‘kumpata’ mzazi mtoto
hulazimika kuonyesha alivyo mjuzi. Ujuaji hubaki kuwa fahari pekee ya mtoto
badala ya urafiki wake na mzazi.
Kwa kuwa ni rahisi mzazi kumsifia
mtoto kuliko kushughulika na usumbufu wake, mzazi anaweza kukosa kiasi
anapomsifia mtoto. Ikumbuke kuwa mtoto tayari anaamini hakuna mtu anajali hali
yake. Faraja yake inakuwa kusifiwa kwa kuonesha uwezo na ujuzi. Sifa zinakuwa
ndio utumwa wake.
Taratibu anaanza kuamini thamani ya
mtu ni ujuaji wake. Anapofahamu kitu wasichokijua wengine, hujichukulia kama
mtu wa thamani kuliko wengine. Ujuzi huwa mtaji wa kukubalika kuliko namna
wanavyoishi na watu.
Unachoweza kufanya
Jenga urafiki na mtoto badala ya
kuwekeza kwenye matarajio. Urafiki maana yake ni kuelewa anavyojisikia, kujua
maumivu na hofu alizonazo. Mtoto anayeeleweka hana sababu ya kudharau watu.
Urafiki na mtoto usitegemee kile
anachokiweza. Urafiki na mwanao ni wajibu. Kumpenda mtoto kusiwe ‘mafao’ ya
kufikia matarajio uliyonayo kwake. Mtoto anabaki kuwa mwanao hata kama hajafikia
matarajio fulani.
Tatu, epuka kumsifia mtoto kupita
kiasi. Sifa zinajenga utegemezi zisipotolewa kwa utaratibu. Msifie bila kumfanya
ajione yeye ndiye bora kuliko wengine. Kila inapowezekana hakikisha anasikia
ukiwasifia na wengine. Itamfundisha kuwa wapo wanaoweza pia kama yeye.
asante kwa mafundisho mazuri
JibuFuta