Kumsaidia Mtoto Asiyejiamini, 'Anayeogopa' Watu
PICHA: Blend Images |
KUTOKUJIAMINI
ni kutokuwa na ujasiri, kutokuwa na imani na uwezo wako mwenyewe. Mtu
asiyejiamini anaweza kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya vitu. Tatizo lake ni
kujishuku. Vijana wa mjini wanaita ‘kujistukia.’
Huenda
umewahi kukutana na mtu anayefanya kitu kwa umahiri mkubwa lakini ana wasiwasi.
Pengine na wewe ni mmoja wapo. Unafanya kitu vizuri tu lakini bado unahisi
hujafanya ipasavyo. Wanaokuona wanaweza kukupongeza kwa kazi nzuri lakini ndani
yako bado unahisi wanakudanganya. Huamini unachoambiwa. Hii ndio hali ya
kutokujiamini.
Unapokosa
imani na uwezo wako mwenyewe unajiweka kwenye hatari ya kushindwa katika maisha.
Huwezi kufanikiwa kama huna hakika na uwezo wako mwenyewe. Maisha yanakuhitaji
ujiamini. Watu huwa na mashaka na mtu ambaye yeye mwenyewe haonekani kujiamini.
Aidha,
unaweza usiwe na uwezo mkubwa lakini kujiamini kukakubeba. Ukijiamini, watu
watakuamini. Kujiamini kunaongeza uwezekano wa watu wengine kuwa na imani na wewe.
Kwa hakika kuaminiwa ni jambo la muhimu katika maisha. Wapo watu wanakosa kazi
kwa sababu tu wameshindwa kuonyesha kujiamini kwenye usaili. Wapenzi, hali
kadhalika, wanaweza kufarakana kirahisi kwa sababu tu kuna mmoja wao hajiamini.
Mtu asiyejiamini hujaa wivu usio na sababu na humchosha mwenzake. Kujiamini,
kwa kweli, ni tunu muhimu kwenye maisha.
Jambo
la kuzingatia ni kwamba hatuzaliwi na hali ya kutokujiamini. Kujiamini
kunajengwa. Kila mtu anaweza kujenga hali ya kujiamini ndani yake. Wazazi wanaweza
kujifunza kuwajengea watoto kujiamini. Ili uweze kufanikiwa kumjengea mtoto
imani na uwezo wake mwenyewe, ni muhimu kuelewa viashiria vya mtoto
asiyejiamini na chanzo chake.
Viashiria vya
kutokujiamini
Unaweza
kumfahamu mtoto asiyejiamini tangu akiwa mdogo. Kwanza, ana tabia ya ‘kumganda’
mzazi/mlezi kupita kiasi. Anapohisi dalili za kuachwa, hali ya hewa hubadilika.
Kwa mfano, katika umri wa miezi kadhaa tu, hapendi kabisa kuachwa. Ingawa mtoto
anayejiamini naye atalia kama huyu, tofauti yao ni kwamba itamchukua muda huyu asiyejiamini
kunyamaza.
Pili,
ni mdekaji na muda mwingi analia lia bila sababu ingawa si mgomvi wala mkaidi. Wakati
mwingine huwa ni mtoto mwenye mashitaka mengi dhidi ya wenzake. Kinachomsumbua
ni haja ya kusikilizwa.
Pia
katika umri wa kuanzia miaka sita na kuendelea, mtoto asiyejiamini anaweza kuwa
mkimya. Ingawa si kila mtoto mkimya hajiamini, mara nyingi, ukimya unaashiria
woga na wasiwasi wa kutokueleweka na watu. Mtu mkimya ni nadra kujichanganya na
watu.
Kinachomfanya
ashindwe kujichanganya na wenzake ni kujistukia. Nafsi yake haiamini watu. Ndani yake kuna sauti inayomnong’oneza, 'Walimwengu
hawaaminiki. Usimwamini mtu!'.
Hata hivyo, wapo watoto wasiojiamini wanaokuwa na tabia ya kupenda kuwa na watu. Kinachofanya wapende ‘kujichanganya’ na watu, si upendo walionao kwa watu bali ni ile hali ya kuwaamini wengine kuliko wanavyojiamini wao. Mioyo yao haijisikii utoshelevu bila kuwa na watu wanaowaamini na hivyo wanakuwa na shauku kubwa ya kutaka kuwapendeza na kuwaridhisha wengine. Hali hii huwafanya wawe na ‘umaarufu’ fulani.
Hata hivyo, wapo watoto wasiojiamini wanaokuwa na tabia ya kupenda kuwa na watu. Kinachofanya wapende ‘kujichanganya’ na watu, si upendo walionao kwa watu bali ni ile hali ya kuwaamini wengine kuliko wanavyojiamini wao. Mioyo yao haijisikii utoshelevu bila kuwa na watu wanaowaamini na hivyo wanakuwa na shauku kubwa ya kutaka kuwapendeza na kuwaridhisha wengine. Hali hii huwafanya wawe na ‘umaarufu’ fulani.
Mtoto asiyejiamini anaweza kupatwa na ‘dhoruba’ anapoingia
kwenye kipindi cha balehe. Kwanza, hana imani na kile anachoambiwa na mzazi
wake. Kichwani kwake anaamini mzazi hamtendei haki. Kwa hiyo hata anapoelekezwa
jambo si mwepesi kuzingatia. Katika mazingira haya, kugombana na wazazi ni
jambo la kawaida kwake.
Katika uhusiano wa kimapenzi, mtu asiyejiamini huwa na wivu uliopitiliza. Wivu humfanya awe na matarajio mengi yasiyo halisi na hutamani kumdhibiti mpenzi wake. Ingawa anaweza kuonekana kama mtu anayejua kupenda, ukweli ni kuwa wasiwasi alionao humfanya awe karibu sana na mwenzake kwa lengo la kumlinda.
Chanzo
cha kutokujiamini
Kutokujiamini kunachangiwa na mambo
kadhaa kwa pamoja. Kwanza, ni mchanganyiko wa malezi yaliyojaa upendo yasiyo na
kelele wala mabavu lakini yasiyotabirika. Mtoto huyu kwa hakika anaelewa kuwa
wazazi wake wanamthamini na kumpenda. Ingawa mzazi si mtu mkali mwenye ghasia, changamoto
ni kuwa mtoto anakuwa hana hakika afanya nini kuupata upendo huo unaopatikana
kwa nadra. Sababu ni kuwa mzazi kimsingi ana utoro wa kutokupatikana nyumbani.
Kwa
upande mwingine, inawezekana mzazi huyu mpole anapatikana kimwili, lakini
kihisia ni kama vile hayupo. Muda mwingi anakuwa hajali kile anachojisikia
mtoto au inawezekana ameweka ukuta mnene kati ya yake na mtoto. Mazingira haya
yanamchanganya mtoto asielewe ni wakati upi anaweza kubahatisha ‘urafiki’
usiojulikana utapatikana lini.
Lakini
pia inawezekana mzazi huyu ni mkosoaji kupindukia. Ingawa ni mzazi mwenye utulivu
na asiyetumia nguvu, ana viwango vya juu mno ambavyo humwia mtoto vigumu kuvifikia.
Huyu ni mzazi mgumu kumridhisha kwa sababu usipofikia viwango vyake, ni sawa na
hujafanya kitu.
Sambamba
na hilo, inawezekana pia mzazi anamdekeza mno mtoto na hajampa nafasi kufanya
vitu bila msaada kwa imani kuwa ‘mtoto
hawezi kuteseka wakati mimi nipo.’ Huyu ni mzazi anayeamini mtoto kufanya
vitu fulani ni kumsumbua. Mtoto asiyepewa fursa ya ‘kuhangaika kidogo’ huishia
kukosa imani na uwezo wake.
Msaada
unaohitajika
Kwanza,
hakikisha unapatikana kimwili na kihisia. Hata katika mazingira ambayo umebanwa
na shughuli nyingi, tengeneza utaratibu wa kutabirika wakati upi unakuwepo. Unapopatikana,
hakikisha unapatikana kweli kihisia. Mpe mtoto nafasi ya kukupata kwa
mazungumzo na michezo. Usimfanye mtoto afanye kazi ya ziada ‘kukupata’ wakati
upo.
Lakini
pia usimdekeze mtoto. Mzazi utambue kuwa unapomdekeza mtoto unamnyang’anya
ujasiri wake. Kumdekeza kunamfanya asijiamini. Punguza kumwonea huruma mtoto. Mpe
fursa mtoto kujifunza maisha kwa kumshirikisha kwenye shughuli ndogo ndogo.
Mwache afanye vitu kwa uhuru wake bila kumpa msaada mkubwa.
Pia,
epuka kumkosoa mtoto kupindukia. Punguza matarajio. Mpe mtoto nafasi ya kukosea
na msaidie kujiwekea malengo yanayosadifu uwezo alionao. Hata pale anaposhindwa
kuyafikia, mtie moyo. Anapofanikiwa, hata kwa sehemu, tambua na mpongeze.
Ahsante sana Barikiwa Mr. Christian Bwaya
JibuFutaAhsante sana Barikiwa Mr. Christian Bwaya
JibuFutaAhsante sana bwaya kwa makala nzuri ningependa kujua inakuwaje kwa mtoto wa namna ya kutojiamini akiishi kwenye mazingira ya shida je anaweza kuwa mbunifu na kujiamini au kwake itabaki hivyo muda wote wa changamoto zake?
JibuFutaMtoto wangu mimi anaweza kufanya mambo mengi mazuri lakini hajiamin ,anawoga anapokuwa shuleni, na hata mbele za watu hiyo inampelekea kutokufanya vizur. Naomba ushauri nifanye nini?
JibuFuta