Mwalimu Anavyoweza Kukuza Udadisi kwa Wanafunzi
PICHA: OBrown & Associates Education Consulting |
Mara nyingi tumesikia watu wakilaumu mtalaa wetu
kwamba unafunga fahamu za wanafunzi wetu. Wenye madai haya wanafikiri bila
mtalaa kufanyiwa marekebisho makubwa, haiwezekani elimu yetu ikamnufaisha
mwanafunzi. Hata hivyo, tulisema wiki iliyopita, kazi ya mtalaa ni kutoa diraya jumla ya aina ya raia wanaotarajiwa kufundwa kupitia mtalaa husika.
Mwalimu ndiye mwenye kazi kubwa kuhakikisha kuwa
wanafunzi wanaelewa kile kinachokusudiwa kufikiwa na mtalaa. Katika makala haya
ninalenga kuonesha namna gani mwalimu aliyefuzu anaweza kutumia mtalaa huu
unaolalamikiwa kujenga tabia ya udadisi kwa wanafunzi wake.
Ningependa nitumie mfano wa Shirika lisilo la
Kiserikali liitwalo Opportunity Education. Shirika hili linaendesha mradi
unaoitwa Next Generation Learning (NGL) ambao kimsingi unajaribu kutafsiri
maudhui ya mtalaa katika mazingira halisi ya mwanafunzi. Kazi hii inafanywa na
walimu wa shule zetu waliopata mafunzo maalum kuandaa mfululizo wa masomo
yanayoandaliwa kutokana na mtalaa wetu.
Sambamba na kutafsiri maudhui ya mtalaa wetu, NGL
wametengeneza mfumo wa ufundishaji na ujifunzaji wanaousimamia wao wenyewe kwenye
shule teule. Mradi huu ambao tayari umeshaonesha mafanikio, unatumia kanuni kuu
tano ambazo naamini mwalimu yeyote anaweza kuzitumia.
Kwanza, kuhakikisha kuwa mwanafunzi anaelewa kwa
nini anahitaji kujifunza kile anachojifunza. Hili kwa hakika limekuwa
changamoto ya ufundishaji wa kimazoea.
Tumekuwa tukifundishwa maudhui ambayo kwa kweli
hatuelewi tutayatumia wapi. Nakumbuka kwa mfano, nikiwa kidato cha V kwenye
somo la Fizikia tulifundishwa hesabu ndefu za namna ya kutafuta muda
utakaotumiwa na tone la mwisho kudondoka kwenye bomba la maji linalofungwa.
Hatukuelewa kwa nini ilikuwa ni lazima kusumbua
akili kufanya hesabu hizi ngumu zisizotatua tatizo lolote kwenye maisha yetu. Ufundishaji
wa namna hii, kwa hakika, unamkatisha tamaa mwanafunzi. Mwanafunzi asiyeelewa
kwa nini anasoma kitu hawezi kuwa na udadisi. NGL wameonesha mfano wa namna
tunavyoweza kuondoa hitilafu hii.
Kupitia mfumo wao wa ujifunzaji, NGL wanajaribu
kufikiri namna gani kile kinachofundishwa kinagusa maisha ya kawaida ya
mwanafunzi. Kujua uhusiano wa maudhui na maisha yake kunamwongezea mwanafunzi
ari ya kujifunza kwa sababu anaelewa thamani ya kile anachotarajiwa kujifunza.
Mwalimu anapata somo muhimu hapa. Kwamba ni
muhimu atafute namna ya kuhusianisha somo lake na maisha ya mwanafunzi. Kwa
mfano, mwalimu wa Kemia anapofundisha somo la Mada (matter) anahitaji kufanya
kazi ya ziada kumsisimua mwanafunzi kuona namna maarifa ya mada yanavyoweza
kumsaidia katika maisha yake ya kila siku. Kazi hii haifanywi na mtalaa bali
mwalimu.
Kanuni
ya pili inayotumiwa na NGL, ni kuhakikisha mwanafunzi anajenga uwezo wa
kujiuliza maswali ya msingi kuhusu hicho anachojifunza badala ya kutegemea
majibu yaliyopikwa na mwalimu anayeonekana kuwa mjuzi na mmiliki wa maarifa.
Kwa
hakika madarasa yetu yanafanya kinyume. Kazi ya walimu imekuwa ni ‘kuhubiri’
maarifa kwa mwanafunzi. Mwanafunzi anachukuliwa kama mtu anayesubiri kupikiwa
kila kitu na kazi yake ni ‘kumeza’ kile anachoambiwa. Hana fursa ya kuuliza
wala kuhoji.
Shule
zetu ‘zinazofaulisha sana’ kimsingi zinajitahidi kuhakikisha mwanafunzi
anafahamu kwa hakika nini cha kukariri. Walimu wa shule hizi wanafanya bidii
kubwa kuwaimbisha wanafunzi kile wanachojua kitaulizwa kwenye mtihani.
Somo
tunalopewa na Opportunity Education ni kwamba mwanafunzi anayewekewa mazingira
ya kujiuliza maswali na kushiriki moja kwa moja katika kutafuta majibu, anakuwa
na uwezo wa kudadisi kuliko mwenzake anayeshiriki ‘kumeza’ maarifa.
Mwalimu
lazima afanye kazi kubwa ya kuibua maswali yanayohusiana na kile
anachokifundisha ili wanafunzi waweze kujifunza kwa mfumo wa kutafuta majibu
wao wenyewe. Mradi wa NGL unatuthibitishia kuwa mwalimu akiwezeshwa anaweza
kutafsiri mtalaa huu unaodaiwa kuwa haufai kuibua kiu ya kutafuta majibu.
Kanuni
ya tatu ni kumtarajia mwanafunzi kutumia maarifa yake kutengeneza ujuzi.
Mwanafunzi wa NGL si tu anahitajika kujibu maswali ya kufikirisha, bali
kuonesha ujuzi mahususi. Mathalani, baada ya mwanafunzi kujifunza namna mimea
inavyotengeneza sukari kwa kutumia mwanga wa jua, lazima aoneshe anavyoweza
kutumia maarifa hayo kutatua matatizo katika mazingira yake.
Inaendelea
Chapisho hili limeondolewa na msimamizi wa blogu.
JibuFutaNi kweli Mwalimu, lazima tuwashirikishe wanafunzi nao ktk kufikiri na Kutafiti na si kuwamezesha tuu .
JibuFuta