Umuhimu wa Mwajiriwa Kuwa na Mkataba wa AjiraWaajiriwa wengi, hususani kwenye sekta binafsi, wanafanya kazi bila kuwa na mikataba. Utendaji na usalama wa wafanyakazi hawa, kwa kiasi kikubwa, unategemea hisani na uaminifu wa mwajiri.

 Kufanya kazi bila mkataba kuna hatari kadhaa. Kwanza, panakosekana ushahidi wa kisheria kuwa umeajiriwa. Katika mazingira haya, inapotokea unapata matatizo kazini, itakuwa rahisi zaidi kupoteza kazi yako. Vile vile, kutokuwa na mkataba kunakuweka kwenye hatari ya kupoteza haki zako za msingi kama mfanyakazi anayelindwa na sheria za nchi.

Hata hivyo, si kila mkataba unaweza kukulinda wewe kama mfanyakazi. Katika makala haya tunaangazia masuala muhimu ya msingi yanayofanya mkataba wako wa ajira uwe na sifa za kukulinda.

Maana ya mkataba

Mkataba wa ajira ni makubaliano yanayofanywa na mtu au taasisi inayoitwa mwajiri kwa upande mmoja, na mtu anayefahamika kama mwajiriwa kwa upande mwingine kwa lengo la kuainisha haki na wajibu wa pande hizi mbili.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, namba 6 ya 2004, mwajiri ni mtu au taasisi inayomlipa mtu mwingine ujira kwa ajili ya kutoa huduma, ujuzi au nguvu kazi inayofanikisha shughuli zake. Mwajiriwa, kwa upande mwingine, ni mtu mwenye sifa na uzoefu anayefanya kazi chini ya mamlaka ya mtu mwingine au taasisi akilipwa kwa minajili ya kutumia uzoefu na sifa zake kutoa huduma.

Aina ya mikataba
Aina ya kwanza ya mkataba, ni mkataba wa kudumu. Mkataba huu hauainishi ukomo wa ajira na hauelezi ajira itachukua muda gani.
Aina ya pili, ni mkataba wa muda maalum unaofafanua ukomo wa ajira husika. Ukomo unaweza kuwa mwezi mmoja, mwaka mmoja, miwili, mitatu au vinginevyo. Kwa kutumia mkataba huu, muda ulioelezwa kwenye mkataba huo utakapokwisha, huo ndio unakuwa ukomo wa ajira.
Tatu, ni mkataba wa jukumu/shughuli maalum. Hapa mwajiriwa anapewa mkataba wa kukamilisha kazi mahususi. Kazi hiyo inapokamilika, huo ndio unakuwa ukomo wa mkataba. Kwa mfano, mtu anaweza kupewa mkataba wa kuandika mradi. Kazi hiyo ya kuandika mradi itakapokamilika, mkataba huo unakuwa umefikia mwisho.

Mambo muhimu kwenye mkataba

Bila kujali mfumo wake, mkataba hutaja upande unaotoa kazi na upande unaokubali kazi hiyo; kuitaja kazi husika bayana; kuainisha vigezo na masharti ya kazi husika na kiwango cha mshahara atakacholipwa mwajiriwa.

Aidha, mkataba lazima uzingatie uhuru wa pande zote kufanya makubaliano bila shinikizo. Kwa mfano, lazima mwajiriwa akubali kufanya makubaliano hayo kwa hiari yake mwenyewe. Lakini pia mkataba lazima uzingatie sheria za nchi. Mfano, mkataba unapokuwa umeandikwa kwa namna inayomwezesha mwajiri au mwajiriwa kukwepa kodi stahiki basi mkataba huo unaweza kukosa sifa.

Ingawa ni kweli mkataba wa ajira unaweza kuwa makubaliano yasiyoandikwa, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya 2004 inaainisha masuala muhimu kuwekwa kwenye maandishi.

Masuala hayo ni kama jina la mwajiri na mwajiriwa; tarehe ya ajira kuanza; kiwango cha mshahara; nafasi ya kazi na majukumu yake; mahali pa kazi; mahali mwajiriwa alikopatikana; mfumo wa kukokotoa malipo; namna malipo hayo yatakavyofanyika (kwa siku, wiki au mwezi); saa za kazi; utaratibu wa likizo; mwongozo nyakati za ugonjwa na kukosa uwezo wa kufanya kazi na utaratibu wa kufuata wakati wa kuvunja mkataba.

Mkataba unaweza kurejea kanuni za utumishi na sera za maadili na nidhamu kwa mujibu wa mwajiri. Jambo la msingi kuzingatia ni kuwa mkataba lazima uheshimu sheria za nchi, kanuni na miongozo mingine ya kazi.


Wajibu wa mwajiriwa

Kwa mujibu wa sheria hii, mfanyakazi ana majukumu kadhaa. Mosi, kuhudhuria kazini kwa muda na mahali kama ilivyoainishwa kwenye mkataba. Muda na mahali pa kazi vinaweza kubalika ikiwa shughuli husika itabadilika. Pili, mwajiriwa ana wajibu wa kutii amri halali za mwajiri wake bila kuathiri utendaji wake wala kuvunja sheria za nchi.

Tatu, mwajiriwa ana wajibu wa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa akiutumia ujuzi na uzoefu wake kutekeleza majukumu aliyopewa. Nne, mwajiriwa anawajibika kuwa na mwenendo mwema, kufanya kazi kwa uaminifu na kuheshimu misingi ya maadili. Maadili ni pamoja na kutunza siri za kazi na kuhakikisha kuwa siri za kazi hazifahamiki kwa mtu asiyehusika.

Pia, mwajiriwa ana wajibu wa kutoa taarifa (notisi) pale anapofanya maamuzi ya kusitisha ajira. Kuondoka kazini kienyeji bila kuheshimu mkataba wake na mwajiri ni kinyume cha sheria.


Wajibu wa mwajiri

Wajibu mkuu alionao mwajiri ni kumlipa mwajiriwa ujira wake kwa mujibu wa mkataba. Kama tulivyoainisha awali, mkataba lazima utaje kiwango cha mshahara kilichokubaliwa na pande zote mbili. Kadhalika, endapo mwajiriwa atafanya kazi nje ya muda wa kawaida, mwajiri anawajibika kumlipa kwa kufanya kazi kwa muda wa ziada.

Mwajiri pia ana wajibu wa kufidia hasara au gharama anazoingia mwajiriwa katika kutekeleza majukumu yake kwa niaba ya mwajiri. Hata hivyo, si kila gharama anazoingia mwajiriwa zinaweza kuwa halali.

Kadhalika, mwajiri anawajibika kuhakikisha kuwa mwajiriwa anafanya kazi katika mazingira salama yasiyohatarisha afya yake. Katika kufanya hivyo, mwajiri atachukua tahadhara za kuhakikisha kuwa mahali pake pa kazi panamwezesha mfanyakazi kutekeleza majukumu yake bila kupata madhara.

Ndio kusema, mwajiri atakayeshindwa kutoa vifaa vilivyo kwenye hali ya usalama; au atakayetoa vifaa vyenye hitilafu zinazoweza kuhatarisha usalama wa mwajiriwa au atakayeshindwa kurekebisha hitilafu ya vifaa aliyopewa taarifa, atakuwa anafanya kosa linaloweza kuhalalisha mfanyakazi kuacha kazi kwa kulazimika.

Makala haya yameandaliwa kwa msaada mkubwa wa Janeth Urio ambaye ni Mhadhiri wa Sheria, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge na Wakili wa Mahakama Kuu. 

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?