Mwalimu Anavyoweza Kukuza Udadisi kwa Wanafunzi -2

PICHA: The East African

MWALIMU anabeba wajibu muhimu wa kuhakikisha mwanafunzi anajenga ari ya kujifunza maudhui kama yaliyoainishwa kwenye mtalaa. Mwalimu aliyeandaliwa vyema na kufuzu kazi ya kutafsiri mtalaa katika maisha ya mwanafunzi, anaweza kuibua na kuchochea udadisi kwa mwanafunzi. 

Katika makala ya kwanza tulitumia mfano wa mradi wa Next Generation Leaning (NGL) unaoendeshwa na Shirika la Opportunity Education kujifunza namna mwalimu anavyoweza kuifanya kazi hii kwa ufanisi.

Tuliona kanuni mbili. Kwanza, mwalimu anahitaji kumfanya mwanafunzi aone namna gani kile anachofundishwa darasani kinagusa maisha yake ya kawaida. Kujua uhusiano uliopo kati ya maudhui anayojifunza na maisha yake, kunamfanya athamini maudhui husika na hivyo kuwa na ari ya kujifunza. Pili, mwalimu anahitaji kumjengea mwanafunzi uwezo wa kujiuliza maswali ya msingi kuhusu maudhui anayojifunza. Kanuni hii inamsaidia mwanafunzi kupunguza utegemezi kwa mwalimu na hivyo kujenga hali ya kujiamini kuwa anaweza kushiriki kwenye mchakato wa ujifunzaji. Kujiamini ni msingi muhimu wa udadisi wa mtoto.

Kanuni ya tatu ni kujenga ujuzi. Mwanafunzi wa NGL anatarajiwa kutumia maarifa anayojifunza kuzalisha. Tunafahamu walimu wengi katika shule zetu huwatarajia wanafunzi kukusanya na kukariri maarifa. Kipimo cha ujifunzaji siku zote kimekuwa ni kwa kiwango gani mwanafunzi anajua maelezo sahihi ya nadharia. Mwanafunzi anayesoma mada ya Uchafuzi wa Mazingira, kwa mfano, anatarajiwa kukusanya, kukariri na kuelewa maelezo mengi kuhusu uchafuzi wa mazingira.

Mwanafunzi huyu aliyeelewa mambo mengi kuhusu uchafuzi wa mazingira anaweza kuvumilia kuishi na takataka zilizo karibu na makazi yake bila wasiwasi. Uelewa wa uchafuzi wa mazingira, haumsaidii kuona tatizo. Kwa mwanafunzi huyu uchafuzi wa mazingira ni ‘mambo ya shule’ yasiyohusiana na maisha yake halisi. Upungufu huu unachangia kuwafanya wanafunzi wetu wasijue namna gani wanaweza kutumia kile wanachokifahamu katika maisha halisi.

Katika zama hizi za ukuaji wa mawasiliano, maarifa ya kila namna yanaweza kupatikana. Mtu yeyote mwenye ujuzi wa namna ya kutumia mtandao wa intaneti anaweza kutafuta na kupata chochote anachotaka kujifunza. Kuendelea kusisitiza kwenye kumbukumbu ya maarifa kimsingi si kumtendea haki mwanafunzi. Maarifa hayapaswi kuwa lengo la elimu. Tunahitaji kuongeza thamani kwa kwenda mbele ya maarifa.

Badala ya mwalimu kumjazia mwanafunzi maelezo mengi, anahitaji  kulenga katika kukuza uwezo wa mwanafunzi kutumia maarifa anayoyapata katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto halisi zinazomkabili. Uwezo huu unaitwa ujuzi. Mtu mwenye ujuzi anaweza kufanya vitu vinavyoonekana kama ushahidi kuwa amejifunza maudhui fulani.

Kwa mfano, katika kufundisha mada ya Uchafuzi wa Mazingira, mwalimu asiishie kumjaza mwanafunzi nadharia na maelezo mengi yanayohusiana na uchafuzi. Badala yake, aende hatua moja mbele kwa kumjengea mwanafunzi uwezo wa kuona matatizo yanayofanana na kile anachojifunza na kujaribu kutafuta majibu yanayolingana na kiwango chake cha uelewa. Huko ndiko kutumia maarifa kujipatia ujuzi.

Hiki ndicho kinachofanywa na mradi wa NGL. Tunajifunza kwamba mwalimu aliyeandaliwa vizuri anaweza kumjengea mwanafunzi uwezo wa kuja na majibu yanayolingana na uwezo wake. Mwalimu wa NGL, kwa mfano,  mbali na kuhakikisha mwanafunzi anahusianisha kile anachojifunza na maisha yake, anatarajiwa kukuza ujuzi wa mwanafunzi kwa kufundisha katika namna inayochochea utafutaji wa majibu. Ufanisi wa somo unapimwa kwa namna mwanafunzi anavyoweza kutazama nje ya darasa na kubaini matatizo yanayoweza kutatuliwa kwa kutumia maarifa aliyonayo.

Kanuni ya nne ni kumwezesha mwanafunzi kujifunza kwa ushirikiano na wenzake. Tunafahamu kuwa wanafunzi hutofautiana uwezo. Wapo wanafunzi wenye uelewa mkubwa wa mambo kuliko wengine. Kadhalika, kila mwanafunzi anaweza kuwa na eneo analoliweza zaidi kuliko maeneo mengine.

Mradi wa NGL unamfanya mwalimu afikiri namna gani mwanafunzi atashirikiana na wenzake darasani katika mchakato wa kujifunza. Mwalimu anahitajika kuweka mazingira yanayomlazimu mwanafunzi kujadiliana na wenzake, kusikiliza mawazo ya wenzake na kutafuta majibu akiwa na wenzake. Kufanya hivi kunamwezesha mwanafunzi kufurahia kile anachokisoma kwa sababu ujifunzaji unafanyika katika mazungumzo ya kawaida.

Ingawa walimu wetu wamekuwa wakifundishwa mbinu hii ya kuwashirikisha wanafunzi katika ujifunzaji, mara nyingi utekelezaji wake umekuwa na changamoto nyingi. Walimu wengi, kwa mfano, hupata shida kujua ni wakati upi mwanafunzi ashirikiane na wenzake na anaposhirikiana na wenzake afanye nini. Matokeo yake walimu huendelea kutumia mbinu za kimazoea zinazowanyima wanafunzi fursa ya kushiriki kwenye mchakato wa ujifunzaji.

Inaendelea


Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?