Namna ya Kujenga Uhusiano Mzuri na Wafanyakazi Wenzako -2


PICHA: gainrecruitment.com


Katika makala yaliyopita, tuliona tabia mbili unazozihitaji ili kujenga uhusiano mzuri na wafanyakazi wenzako. Tabia ya kwanza ni kuwafanya wenzako wajione wana hadhi ya juu kuliko wewe. Unapowafanya watu waamini wanakuzidi, kwa kawaida unawaondolea sababu ya kupambana na wewe.

Tabia ya pili ni kuwasaidia wenzako kufikia malengo yao. Tulisema, kila mtu anajipenda. Sisi binadamu ni wabinafsi kwa asili. Ni nadra kumpenda mtu asiyetupenda. Tumia hulka hiyo kunyoosha mambo yako. Wasaidie wenzako kufanikisha malengo yao. Ukifanya hivyo, unatengeneza mtandao wa watu watakaojisikia kuwajibika kukusaidia na wewe.

Katika makala ya leo, tunaangazia tabia nyingine nne zinazoweza kukusaidia kujenga mahusiano mazuri ya kikazi na wenzako.


Kubali kuanzia chini

Wanafunzi huwa na matumaini makubwa wanapokuwa masomoni. Wanafikiri mafanikio hutokea kwa njia ya mkato. Wengine huwa na ndoto za kulipwa mishahara minono itakayobadilisha maisha yao ndani ya muda mfupi.

Ukiacha kipato, kuna mambo ya vyeo. Wafanyakazi wapya hufikiri ni rahisi kukwea ngazi na kupewa  madaraka makubwa kirahisi. Wasichojua ni kuwa viongozi wanaowaona sasa kazini, wamefanya kazi kwa muda mrefu kufikia hapo walipo.

Fikra kuwa unaweza kuanzia juu zinaweza kukuingiza kwenye matatizo kazini. Kwanza, utakosa uvumilivu wa kufanya kazi chini ya watu wengine kwa kujiona una sifa za kutosha kukupandisha juu kimamlaka. Fikra hizi zinaweza kuzaa misuguano isiyo ya lazima na wenzako kazini.

Unahitaji kuwa mtu wa subira. Jizuie kujipatia sifa za haraka haraka. Ukweli ni kwamba mafanikio yoyote kazini ni matokeo ya jitihada na bidii zinazoweza kuchukua muda kulipa. Kila aliyefanikiwa leo, alianza chini. Ili ufanikiwe unahitaji kuwa na subira.

Jitambulishe kwa matokeo

Moja wapo ya makosa tunayoyafanya kazini ni kutamani kutambulika.  Shauku ya kutambulika inaweza kukusukuma kuwa mtu wa maneno mengi. Unapofanikisha jambo unatamani kila mtu alifahamu. Unafikiri kwa kuwaambia watu namna ulivyofanikiwa watakuheshimu. Mara nyingi ni kinyume chake. Mafanikio yako yanapofahamika yanajenga hisia za wivu kwa wenzako. Unapowaambia watu mambo yako unajijengea maadui wa hiari.

Pia, wakati mwingine tunafikiri ili tutambulike, ni muhimu kuwapandishia watu matarajio waliyonayo kwetu. Ili kufanya hivyo, tunakuwa watu wa kutoa ahadi zinazofanya watu wawe na imani kubwa na sisi. Hatari, hata hivyo, ni pale unaposhindwa kuishi maneno yako. Matokeo yake, mara nyingi, ni kujishushia hadhi uliyojaribu kuijenga kabla ya wakati wake.

Badili mbinu. Punguza matarajio ya watu kwako na fanya bidii ya kuzidi matarajio hayo. Sema maneno chanya wakati ukifanya jitihada za kuongeza ubunifu katika kazi zako. Wafanye watu wakutambue kwa kazi zako. Fanya kazi zako zipige kelele bila kusaidiwa na maneno mengi.
Unapofanya hivyo, jitahidi kuongeza ubunifu na juhudi kufanya kazi zako. Utajijengea heshima kazini na watu wataona thamani yako bila wewe kulazimika kuwatangazia.

Linda heshima ya wenzako

Mazingira ya kazi hayakosi watu wanaopenda kueneza maneno ya watu. Utakaa na mtu unayemheshimu wakati wa chai kisha ataanzisha mazungumzo yanayomhusu mtu asiyekuwepo kwenye mazungumzo hayo. Nani anatoka nani. Nani hawezi kazi. Nani ni swahiba wa bosi na mambo kama hayo. Mazungumzo kama haya yanaitwa majungu. Lengo, mara nyingi, ni kubomoa hadhi za watu wengine. Wakati mwingine mambo haya hulenga kuimarisha makundi ya kimaslahi kazini.

Kwa kawaida, majungu ni kazi ya watu wasio na kazi; watu wasiojiamini au watu wanaolinda maslahi binafsi kwa kubomoa heshima za wengine. Unapokubali kuyasikiliza mazungumzo ya namna hii, tayari unakuwa sehemu ya mzunguko wa majungu kazini. Unajipotezea heshima yako mwenyewe.

Unahitaji ukomavu kufanya kinyume. Jenga utaratibu wa kulinda heshima ya wenzako hata wanapokuwa hawapo kwenye mazungumzo. Unaposikia habari mbaya za mfanyakazi mwenzako, usiwe mwepesi kushabikia. Habari mbaya zilizobomoa heshima ya mwenzako hazikusaidii kuongeza ufanisi wako.

Badala ya kushabikia mazungumzo yanayomharibia mwenzako asiyekuwepo, tafuta jambo jema na liseme kwa ujasiri. Ukijenga tabia ya kuwatetea wenzako, unajijengea heshima yako. Watu watakuheshimu. Unapokwepa kuwa sehemu ya makundi yanayofuga ‘siasa’ za maslahi kazini, utajenga kuaminika kazini. Mbinu chafu zinaposukwa dhidi yako, utakuwa na watu watakaokuwa tayari kukutetea.

Ruhusu watu wakukosee

Binadamu tunapenda heshima. Ni hulka yetu kujihesabu kuwa watu maalum tusiotakiwa kukosewa na mtu yeyote. Hata katika mazingira ambayo tunawakosea wengine, hatupendi wale tuliowakosea watukosee. Haturuhusu watu kutukosea.

Hulka hii inatufanya tuwe wepesi kukasirika pale tunapogundua kuna mtu hana nia njema na mustakabali wetu. Tunakuwa wepesi kulipiza kisasi kwa sababu tunajichukulia kama watu tusiotakiwa kutendewa hila.

Hata hivyo, ni vizuri kuelewa kuwa makazini wapo watu ambao kwa vyovyote vile wanaweza kuwa kinyume na wewe. Unaweza kujitahidi kuishi vizuri na watu, kwa kusimamia haki lakini bado wakawepo watu watakaochukulia wema huo kama sababu ya kukosana na wewe.

Hali hii isikuvunje moyo. Jichukulie kama binadamu anayeweza kuchukiwa bila sababu na mtu yeyote. Jichukulie kama mtu anayeweza kufanyiwa visa na watu wenye kutumia mbinu chafu kufikia malengo yao. Ukielewa hivyo, hutapata shida unapogundua kuna watu wanakuzunguka.

Kufanya hivyo, hata hivyo, haimaanishi kukubali kuonewa bila sababu. Hapana. Ni ule ukomavu wa kikazi unaokufanya uwe tayari kufanya kazi na watu wasiokupenda bila kuathiri kazi zako. 

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Pay $900? I quit blogging

Uislamu ulianza lini?