Yatambue Madhara ya Adhabu ya Bakora
INGAWA
wazazi wengi huwachapa watoto wakiamini wanafanya hivyo kwa lengo la kuwaadabisha,
tulibainisha sababu zilizojificha. Kwa ujumla, tunaweza kusema mzazi
aliyelelewa kwa fimbo hujikuta na yeye akiamini fimbo ndio suluhu ya matatizo
ya kinidhamu anayoyaona kwa mwanae.
Aidha, mzazi
mwenye hasira kwa sababu yoyote, anakuwa na uwezekano mkubwa wa kutumia fimbo
anapofikiria kumwadhibu mwanae. Matumizi ya fimbo katika mukhtadha huu, ni
namna ya kujisaidia yeye mwenyewe kukabiliana na hasira na msongo wa mawazo na
sio kumsaidia mtoto kama inavyoaminika.
Ndio
kusema, mzazi anapokuwa na changamoto zinazomkosesha amani, iwe ni hali duni ya
kiuchumi, migogoro ya ndoa, kutokuwa na utulivu wa maisha, anakuwa na uwezekano
mkubwa wa kutumia adhabu kama namna ya kujituliza bila yeye mwenyewe kughamua.
Kuna
jambo muhimu la kuzingatia kabla hatujatazama madhara ya kumwadhibu mtoto.
Ingawa watoto wote bila kujali jinsia ni wahanga wa adhabu ya viboko katika
jamii, watoto wa kiume huwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kuchapwa kuliko wenzao
wa kike.
Imejengeka
imani isiyowazi kuwa adhabu kwa mtoto wa kiume ni lazima iwe nzito na yenye
kuleta maumivu zaidi kuliko ile anayopewa msichana. Kwamba unapomwadhibu mtoto
wa kiume unaweza kutumia mabavu zaidi kuliko unapomwadhibu mtoto wa kike.
Katika
mazingira ya shule, mathalani, watoto wa kike walichapwa viganjani wakati
watoto wa kiume walichapwa kwa namna inayowadhalilisha zaidi.
Tunaweza
kuwa na tafsiri nyingi kuelezea tofauti hii. Lakini mojawapo, jamii inaelewa maumivu
yanayoambatana na mapigo ya fimbo na hutuzitumia kama namna ya kukuza fikra za
ubabe na mabavu kwa watoto wa kiume. Fimbo zinakuwa namna fulani ya kuendelea
mfumo dume kwenye jamii.
Hata
hivyo, viboko vimethibitika kuwaathiri watoto. Tukiachana na madhara ya mwili
yanayoweza kutokana na majeraha, yapo matatizo makubwa matatu ya kisaikolojia.
Huharibu uhusiano
na mtoto
Adhabu
ya fimbo, kama tulivyoona, ina uhusiano mkubwa na hasira anazokuwa nazo mzazi.
Tunafahamu mtu aliyekasirika anaweza kufanya lolote ikiwemo kutumia nguvu
nyingi kupita kiasi kuliko ambazo angetumia kama angesubiri hasira zipungue.
Upo
utafiti mmoja ulioonyesha kuwa mtu mwenye hasira anapopewa nafasi ya kutulia na
kupooza hasira zake anakuwa mwepesi kughairi matumizi ya adhabu. Mtu huyo huyo
anapotoa adhabu akiwa na hasira, adhabu huwa kali zaidi.
Mara
nyingi, mtu anapotumia fimbo hufanya hivyo akiwa na hasira. Kwamba
anayeadhibiwa amefanya kosa linalostahili kichapo, hufanya adhabu iwe ya papo
kwa hapo. Hakuna kusubiri. Na ilivyo, hawezi kuchapa kimya kimya. Hukazia
kichapo anachokitoa kwa maneno ya kushutumu na kulaumu. Lengo ni kuonyesha kuwa
amefanya hivyo kwa nia njema.
Matokeo
yake adhabu kudhuru
uhusiano wa mzazi na mtoto. Mtoto anayechapwa,
kwa mfano, hujiona kama mtu asiye thamani kwa mzazi wake hasa kama mzazi hana
tabia ya kukarabati mahusiano yake upya na mwanae baada ya kumchapa.
PICHA: parentspartner.com |
Pia
wazazi wengine hawakumbuki kukaa na watoto baada ya adhabu kufafanua sababu
iliyowalazimu kuwachapa na kujadili tabia mbadala. Mzazi mwenye uwezo wa
kufanya mazungumzo ya namna hii baada ya fimbo, maana yake angeweza kabisa
kuachana na mpango wa fimbo tangu awali. Kwa hiyo, ni nadra mzazi aliyemchapa
mwanae kufikiria kurudisha mahusiano baada ya adhabu.
Kukosekana
kwa ukaratabu huu baada ya adhabu ya fimbo hufanya watoto waachwe na majeraha
moyoni ambayo, pasipo hatua kuchukuliwa, huathiri mitazamo ya watoto na hata
namna wanavyowachukulia wazazi wao.
Hukuza tabia ya
usugu
Fimbo
zina tatizo la kuzoeleka. Kadri inavyotumika kumsababishia maumivu mtoto,
ndivyo inavyobidi iwe kali zaidi. Isipokuwa kali na nzito haiwezi tena
kuendelea kumfanya mtoto apate maumivu yanayotarajiwa. Kama mtoto alikuwa
akichapwa fimbo mbili ndogo, baada ya muda, fimbo mbili hazitshi kumpa
wasiwasi. Anajua akikosea, atapata fimbo mbili na mambo yataisha.
Kwa
kuwa mzazi hana namna nyingine ya kumrudi mwanae, mtoto hufanya kosa lile lile.
Mzazi naye hutumia mbinu ile ile ya kumsababishia mtoto maumivu akifikiri
anaweza kumjengea hfu ya kutorudia alichokifanya. Kwa mshangao wake, mzazi
anaweza mtoto hufika mahali hatetemeki kama ilivyokuwa awali.
Suluhu inakuwa
ni kuongeza mapigo ili kutengeneza woga unaoonekana kupotea. Kadri mapigo yanavyozidi
kuongezeka na kuwa makali zaidi, ndivyo adhabu inavyoendelea kupoteza maana
yake na kugeuka kuwa ugomvi kati ya mzazi na mtoto.
Watoto
wanaozoea hali ya kupigwa, ni watu sugu hata katika mahusiano yao na watu
wengine. Wengi wanapokuwa watu wazima hukosa uwezo wa kujua hisia za wengine
kwa sababu wamekulia kwenye mazingira yaliyowazoeza kupuuza hisia zao wenyewe.
Hufundisha Ubabe
Fimbo humfundisha
mtoto kutumia nguvu katika
kutatua migogoro anayokutana nayo. Watoto wanaochapwa, mara nyingi huwa ni
wagomvi katika maisha halisi. Hujikuta wakiwa na mazoea ya kupigana na wenzao
na hata watu wengine kama namna ya kutatua matatizo yao.
Tabia
ya ugomvi anakuwa amejifunza kwa wazazi wake mwenyewe. Amemwona baba akishika
fimbo kushughulikia tatizo yanayojitokeza na yeye atamshika shati mtu mwingine anayemkosea.
Hawezi kuona njia nyingine bora zaidi. Mtoto wa nyoka anaendelea kuwa nyoka.
Matokeo
ya mazoea haya ni kumfanya awe mtu wa mabavu, mchokozi kwa wenzake, asiyeweza
kuelewa hisia za wengine na mwisho wake na yeye wenyewe hugeuka kuwa mtu
anayeunga mkono fimbo kwa watoto wake. Ni namna fulani ya kuridhisha utamaduni
wa ubabe.
Maoni
Chapisha Maoni