Unajengaje Uhusiano Mzuri na Viongozi Kazini?


Moja ya mambo yanayoweza kukusaidia kufanikiwa kazini ni namna unavyohusiana na mkubwa wako wa kazi. Huyu ni mtu anayekuongoza, anayetoa maelekezo ya nini kifanyike na wakati mwingine ndiye mwenye kauli ya mwisho kwenye taasisi, idara au ofisi unayofanya kazi.

Kwa nafasi yake, kiongozi wa kazi ni mtu mwenye mamlaka ya kufanya maamuzi yanayohusu kazi yako hata kama anaweza asiwe mwajiri wako moja kwa moja. Huyu ni mkuu wa ofisi, idara, kitengo, kampuni au taasisi unayofanyia kazi. Ndiye mtu anayekusimamia na kupokea taarifa za utendaji wako na labda kuzipeleka kwenye mamlaka za juu.

Usipoelewa namna gani unaweza kuishi na mtu mwenye mamlaka juu yako, unaweza kujiingiza kwenye matatizo makubwa yanayoweza kukugharimu. Nawafahamu watu kadhaa wenye weledi, uzoefu na ujuzi mkubwa kazini, lakini wakijikuta wakipoteza kazi zao kwa sababu ya kutokujua namna ya kufanya kazi na wakubwa wao kazini.

Ingawa ni kweli wapo viongozi wanaokosa sifa za uongozi na hivyo kuwa sababu ya misuguano kazini, bado unaweza kujifunza namna ya kupunguza migogoro isiyo na ulazima katika mazingira ya kazi. 

Sambamba na bidii na ufanisi wako wa kazi ambao si sehemu ya makala haya, makala haya yanaangazia masuala matatu makubwa: heshima kwa anayekuongoza, kujua namna ya kumshauri na kuepuka mashindano yasiyo na sababu.

Mpe heshimu anayostahili

Kinachokutofautisha wewe na kiongozi wako ni mamlaka ya kikazi aliyonayo. Mnaweza kuwa na umri unaofanana; inawezekana mmesoma darasa moja; alikuwa rafiki yako wa karibu; una elimu na uzoefu kuliko yeye na mambo mengine kama hayo; Lakini anapokuwa na mamlaka ya kukuongoza, hiyo peke yake ni sababu inayotosha kumpa heshima anayostahili.

Heshima ina mambo mengi. Mosi, ni kujua mipaka yako kwake kwa urafiki, mazungumzo na namna ya kuhusiana naye kila siku. Wakubwa wengi wa kazi wanajisikia salama zaidi wanapokuwa hawafikiki kirahisi. Wengi wao hulinda ushawishi wao kwa kujenga ukuta unaowatenganisha na wafanyakazi wao. Hawapendi kuzoeleka. Unapokuwa karibu nao, ni rahisi kutafsiri kama kuwakosea heshima.  

Pili, mtambue kwa nafasi yake. Wakubwa wengi wanapenda kutambuliwa kwa vyeo walivyonavyo. Katika taaluma, kwa mfano, watu hutambuana kwa viwango vya elimu, ‘Dokta’, ‘Profesa.’ Vivyo hivyo, jeshini. Watu wanathamini vyeo vya kazi, ‘Kapteni’, ‘Luteni’, ‘Meja.’ Fanya hivyo kwa mkubwa wako wa kazi. Tambua nafasi yake bila unafiki. Kumpa mtu hadhi anayostahili si kujidhalilisha wala kujikomba. Ni utaratibu wa kawaida wa kazi.


Kadhalika, mheshimu mkubwa wako kwa kufuata taratibu za kazi hata nyakati za dharura. Wakubwa wengi wa kazi hupenda kupewa taarifa. Epuka kuwa mtu asiye na utaratibu kazini. Heshimu urasimu wa ofisi kwa kupeleka taarifa zinazohitajika mahali panapohusika. Usijione kama mtu mwenye haki ya kufanya lolote.

Jifunze namna ya kutoa ushauri

Kiongozi wa kazi si mtu anayefahamu mambo yote. Inawezekana unamzidi uelewa na pengine maamuzi yake ni kinyume na uhalisia unaoujua wewe. Hata katika mazingira hayo, unahitaji kufikiri namna unavyowasilisha mawazo yako.

Jambo la kwanza, usitoe ushauri usiohitajika. Kama hakuna mtu ameomba mawazo yako, usijipe kazi isiyokuhusu. Unaposhauri jambo lisilohitajiwa na huyo unayemshauri, maana yake unachokifanya ni kujitafutia sifa nyepesi. Huu unaweza kuwa mwanzo wa matatizo kuliko faida.

Pili, mkubwa wa kazi hakosolewi hadharani isipokuwa kama ni lazima. Wafanyakazi wengi wanapenda kukosoa watu wenye mamlaka. Wanafanya hivyo mbele za watu. Wanafikiri kwa kumshambulia mkubwa kikaoni au mkutanoni, basi wataonekana ni wajuzi, wanaharakati na watafuta haki.

Tabia hii ya kupenda kuwakosoa wakubwa mbele za watu mara nyingi inasukumwa na kupenda umaarufu. Kama ni lazima, basi busara ni kumfuata mkubwa wako ofisini kwake au mahali penye faragha na kumpa mawazo unayofikiri yana tija kwa taasisi au kampuni. Unapofanya hivi unamfanya ajisikie kuheshimiwa.

Tatu, unapolazimika kutoa ushauri, tumia lugha chanya yenye kuheshimu haki za wengine. Jenga ushauri wako kwenye kile unachojua kinakubalika. Tumia lugha yenye utulivu, isiyomshambulia wala kumshinikiza mkubwa wako wa kazi kufanya maamuzi unayofikiri ni sahihi. Tumia hoja na takwimu badala ya mihemko, tetesi na hisia.

Usijaribu kumzidi mkubwa

Kumzidi mkubwa wako ni kutaka kupata sifa binafsi zinazokufanya uonekane ni bora kuliko yeye. Tamaa ya kupenda kuwa zaidi ya mkubwa wako wakati mwingine inaweza kukusukuma kufanya kazi kwa bidii na maarifa. Kilichojificha nyuma ya bidii hiyo mara nyingi ni sifa binafsi.

Katika mazingira ya kazi, ni kosa la kiufundi kuonekana unashindania heshima na mkubwa wako wa kazi. Si wakubwa wengi wanaweza kuvumilia mashindano ya namna hii. Kushindania heshima na mamlaka kunachochea chuki na uadui usio na sababu. Mwathirika wa mashindano hayo ya ‘nani anaweza kuliko mwenzake’ mara nyingi ni mfanyakazi.

Siku zote mfanye mkubwa wako wa kazi aonekane juu yako. Kubali achukue sifa kwa kazi nzuri uliyofanya. Kama una mawazo mazuri, mpekee hata kama atayaleta hadharani kama vile ni ya kwake. Unapomwuuzia sifa zako, kimsingi unamtengenezea deni kwako. Mazingira kama haya yanakuongezea ushawishi wako kwake bila yeye kung’amua.

Kadhalika, epuka kuwa na makundi kazini. Kinachoimarisha makundi kazini, mara nyingi, ni mashindano ya madaraka. Mashindano haya yanaweza kuwa sababu ya majungu na fitina kwa lengo la kulinda maslahi ya watu fulani.


Wakati mwingine, waasisi wa makundi haya ni wakubwa wa kazi wenyewe. Usikubali kuchukua upande kwenye makundi hata kama kufanya hivyo kutakuweka ni karibu na mkubwa. Faida ya muda mfupi leo, inaweza kuwa na gharama za muda mrefu. 

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?