Namna ya Kujenga Uhusiano Mzuri na Wafanyakazi Wenzako -1
PICHA: tovoy.se |
Moja ya sababu zinazowafanya wafanyakazi wengi wakose ari ya kazi ni mahusiano mabaya na watu kazini. Kimsingi, tafiti nyingi zinabainisha kuwa, mbali na kutokuridhishwa na maslahi ya kazi zao, wafanyakazi wengi hufikia huacha kazi kwa sababu ya kutokuelewana na watu kazini.
Unapokuwa
na watu wengi ofisini kwako wasiofurahia kukuona; watu wanaokerwa na kazi nzuri
unazozifanya; watu wanaokuonea wivu; watu wanaojenga uadui na wewe, ni rahisi
kukosa amani na mazingira ya kazi unayoifanya. Kukosa amani kazini kunakuondolea
ujasiri na uchangamfu wa kuchangamana na wenzako. Hali hii, kwa kiasi kikubwa,
inaweza kupunguza ufanisi wako kazini.
Kama
ilivyo mitaani, wapo watu kazini huwezi kuwaridhisha. Unaweza kufanya jitihada
za kuwatendea yaliyo mema lakini bado wakakuchukulia kama adui. Pamoja na hayo, ni vizuri kuelewa kuwa si mara
zote watu hujenga chuki na wewe kwa sababu tu hawakupendi. Wakati mwingine,
tabia ulizonazo zinaweza kuchochea hisia za wivu, uadui na hata mashindano yanayoweza
kuathiri mahusiano yako na watu.
Katika
makala haya, tunajifunza tabia mbili zitakazokusaidia kuwa na uhusiano mzuri na
wafanyakazi wenzako. Ukizisoma kwa haraka unaweza kuzichukulia kama mbinu za
kucheza na akili za watu.
Hata hivyo, ukiweza kuzifanya zikawa sehemu ya maisha
yako ya kila siku, zitakujengea tabia ya unyenyekevu unaoanzia ndani na
zitakupunguzia misuguano isiyo na msingi katika mazingira yako ya kazi.
Wafanye watu wajione wanakuzidi
Kwa
kawaida tunapenda kujisikia tunawazidi watu. Kupenda kuwazidi wengine ni moja
wapo ya misikumo iliyojificha nyuma ya mengi tunayoyafanya. Tunapojiona tuna
hadhi ya juu kuliko wengine, hiyo peke yake inatosha kutupa namna fulani ya
utoshelevu wa nafsi.
Katika
mazingira ya kazi hisia hizi za kuzidiana hazikosekani. Watu huweza kushindana
kimya kimya kwa viwango vya elimu; utendaji wa kazi; tija waliyoiletea taasisi
na mambo mengine kama hayo.
Unapoingia
kwenye mfumo wa kazi, unajikuta bila wewe kujua, ukiwa sehemu ya mfumo huu wa
mashindano yasiyo rasmi. Msisimko wa kuanza kazi mpya unaweza, mathalani,
kukusukuma kutaka kuthibitisha kuwa wewe ni mtu mwenye uwezo pengine kuliko wengine.
Vyeti ulivyonavyo vinaweza kukupa kiburi cha kujiona kuwa wewe ni mtu bora na
mweledi kuliko wengine wote uliowakuta kazini.
Wakati
mwingine, hutokea ukalazimika kuwajibika kwa mtu asiye na sifa kama ulizonazo. Kwa
kuwa unataka kuonekana bora, unajisikia kufedheheka nafsi. Unatamani
kuwaonyesha watu hapo ofisini kuwa unamzidi mkuu wako wa kazi.
Ukikubali
hali hiyo ya kujiona unawazidi watu, utajitengenezea mazingira ya kupishana na
watu bila sababu. Utajikuta ukiongea kama mtu anayejua kila kitu. Utashauri
mahali ambapo ushauri wako haujaombwa. Utafanya mambo kwa papara ili tu uonekane
unaweza. Hutakuwa tayari kujifunza kwa wengine. Haya yote yatakutengenezea ufa wa
kimahusiano kati yako na wenzako na utajiweka kwenye hatari ya kutengwa kimya kimya.
Unahitaji
kubadilisha mtazamo. Mosi, sahau imani uliyonayo kuwa ‘najua…hawa wengine
hawajui.’ Mengi uliyojifunza shuleni ni nadharia tu zinazoweza kushindwa kukidhi
matakwa ya uhalisia wa kazi. Kimsingi, mazingira ya kazi ni darasa jipya
linalokulazimu kuwa mwanafunzi endelevu.
Ukishaelewa
hivyo, utafanya jitihada za kujenga taswira ya mtu asiye na ujuaji. Fanya kazi kwa ushirikiano na wenzako. Weka mazingira ya makusudi kuomba msaada kwa watu wanaokuzidi uzoefu. Lakini fanya hivyo kwa
uangalifu bila kuwafanya watu waanze kuwa na wasiwasi na uwezo wako.
Sambamba na hilo, usiwe mwepesi wa kushauri kama
ushauri wako haujahitajika. Unapomshauri mtu ambaye hajakuomba ushauri, anakuona mjuaji. Akikukuona hivyo, hutaweza kufanya nae kazi kwa ufanisi. Badala ya kupenda kushauri, jenga weledi utakaowafanya watu
wakufuate wenyewe kwa ushauri.
Ukiweza
kufanya hivyo, watu hawatakuwa na sababu ya kukuonea wivu, kushindana na wewe
kwa sababu huonyeshi mashindano yasiyo ya lazima. Badala yake watakuchukulia
kama rafiki asiye mshindani. Utajipunguzia
maadui na mapambano yasiyo ya lazima.
Wasaidie watu kufikia malengo yao
Ni
dhahiri nafasi uliyopewa kazini inakutarajia kufikia malengo fulani. Labda ni
kuongeza uzalishaji wa kampuni. Labda ni kupunguza malalamiko ya wateja au hata
kuongeza siha ya bidhaa mnazozalisha. Hayo, kwa hakika, yanakuwa ni malengo
yako rasmi kikazi. Ndiyo dira ya shughuli unazotarajiwa kuzifanya kama
mfanyakazi wa taasisi iliyokuajiri.
Vile
vile, unaweza kuwa na malengo yako binafsi. Mfano, unatamani kupanda cheo baada
ya muda mfupi; kujenga heshima kazini kwako ili ufikie malengo yako binafsi. Si
jambo baya kuwa na malengo yako kama mfanyakazi anayejitambua.
Unapofanya
hivyo, hata hivyo, ni vizuri kuelewa kuwa kila mfanyakazi naye ana malengo
yake. Wakati mwingine malengo yako yanaweza kuingilia na malengo ya mwingine. Kwa
kuwa watu wana tabia ya kujipenda, unapoonekana unatishia malengo yao, unaweza
kujikuta kwenye mgogoro usio rasmi.
Ukifanya
kosa la kuonyesha wazi wazi kuwa unajijali wewe na malengo yako, tena wakati
mwingine ukiwatumia wao, utapoteza watu wengi. Watu, kwa kawaida, hawapendi mtu
anayejifikiria yeye muda wote. Wakigundua unafikiria maslahi yako mwenyewe,
watajitenga na wewe kimya kimya. Mazingira ya namna hii yatakuletea matatizo
mbeleni.
Badala
yake, jaribu kudhibiti ubinafsi wako. Fikiria namna unavyoweza kuwasaidia wenzako
kufikia malengo yao. Unapowasaidia kufikia malengo yako, unawajengea hali ya
kukuhitaji.
Chukulia,
kwa mfano, umebaini kuna mwenzako anapata shida kuandaa ripoti na wewe ujuzi
huo unao. Jitolee kumsaidia afanikiwe. Ujisikie vibaya kuwa atafanikiwa. Kufanikiwa
kwake, kutakuwa akiba kwako. Siku nyingine mtu huyo huyo atajisikia kudaiwa
fadhila kwa kukusaidia na wewe.
Jambo
la kukumbuka ni kuwa katika kuwasaidia wengine kufikia malengo yao, unaweza
kujikuta wakati mwingine watu wakijipatia sifa kwa mgongo wako. Usiumie wala
kujiona umetumika. Huo ni uwekezaji unaolipa. Kwanza, watu hao watadaiwa
kukulipa fadhila siku ukihitaji msaada wao. Lakini pili, kwa kuwasaidia,
unawafanya wasiwe na sababu ya kushindana na wewe.
Makala haya yalichapishwa kwanza kwenye Jarida la
Ajira na Kazi, linaloandaliwa na gazeti la MWANANCHI. Itaendelea Ijumaa ijayo.
nikweli kabisa
JibuFuta