Umuhimu wa Kiongozi Kuwa Mnyenyekevu -2
PICHA: entrepreneur.com |
JUMA lililopita tuliona kuwa mtu
huhitaji sifa fulani kumwezesha kupanda ngazi za uongozi. Mtu anapokuwa na uwezo
wa kufanya kazi na watu; kuwasiliana vizuri na wakubwa wake wa kazi na hata
walio chini yake na kufuatilia mambo ya msingi kwa makini anakuwa katika nafasi
nzuri ya kupewa madaraka.
Kinachompa madaraka, kwa kawaida, ni
zile sifa za utu na uwezo wa kusukuma mambo yakaenda kwa ushirikiano wa
wengine. Mtu asiye na sifa hizi, kwa hakika, inaweza kumchukua muda mrefu
kuaminiwa na kupewa madaraka isipokuwa kwa njia za mkato.
Hata hivyo, baada ya kupata madaraka
hayo, uwezekano wa mtu kubadilisha hiba yake huwa ni mkubwa. Sifa zote
zilizomwezesha kupanda ngazi hupukutika moja baada ya nyingine na sifa hasi huanza
kuchukua nafasi yake.
Kama, mathalani, mtu alikuwa na
ushirikiano na wengine, anaanza kujenga tabia ya kupambambana na wanaomzunguka.
Majivuno,
kiburi, dharau na uonevu vinaanza kuwa sehemu ya maisha yake ya kiuongozi.
Kinachombadilisha
Kimsingi, kiu ya mamlaka humfanya
muhusika asijue kile anachokifanya. Hufikiri ili sauti yake isikike, maana yake
anahitaji kujikweza awe mbali na wenzake. Mtu wa namna hii ni mwepesi wa
kujenga dharau na kiburi na hivyo huwakaripia wanaomzunguka. Katika hatua hii,
mtu huyu hugeuka kuwa mnyapara muamrishaji asiyeambilika.
Msingi wa mabadiliko haya ya kitabia
ni kule kuona hana sababu tena ya kuwasilikiza waliochini yake. Anaamini kwa
namna yoyote watu wa chini yake hawana athari kwake. Huanza kuamini kuwa umbali
na hata kutokuelewana na wenzake kunamsaidia kupata heshima na mamlaka
yanayostahali nafasi yake mpya.
Hatari ya kubadilika
Ingawa mabadiliko haya yanaweza
kuonekana kwa juu juu kama yanamsaidia, katika hali halisi yanaweza kuwa mwanzo
wa safari ya anguko lake kwa namna mbili.
Mosi, kujitengenezea maadui wa
hiari. Hawa ni watu wanaosikitishwa na vitendo vya kudhalilishwa, kunyanyaswa
na kukandamizwa na mtu mwenye madaraka. Kujisikia kudhalilika hujenga chuki
inayoweza kuamsha sababu za kupambana naye waziwazi ama kwa siri.
Ni vigumu kwa kiongozi kufanya kazi
kwa ufanisi katika mazingira yenye upinzani wa namna hii. Kama kiongozi, anahitaji
ushirikiano wa watu kumwezesha kufanya kazi. Watu hawa wanapohujumu juhudi zake
hawezi kufika mbali.
Pili, kwa kuwa anajikuta yuko mbali
na watu wa kawaida, mtu wa namna hii hujawa woga wa ndani kwa ndani. Hana hakika
wanaompiga wanafikiri nini dhidi yake na hivyo hulazimika kujenga ujasiri
bandia kwa minajili ya kuwatisha anaohisi wako kinyume nae.
Hatapenda kuona watu wakiongea kwa uhuru, wakijadili mawazo yanayoweza kubainisha mapungufu yake. Ndio maana unakuta viongozi kama hawa makazini huwa hawapendi vikao, hawapendi kuona watu wakikaa pamoja kuzungumza kwa uwazi. Sasa ni woga uliojengeka ndani yake kuwa anapingwa.
Hatapenda kuona watu wakiongea kwa uhuru, wakijadili mawazo yanayoweza kubainisha mapungufu yake. Ndio maana unakuta viongozi kama hawa makazini huwa hawapendi vikao, hawapendi kuona watu wakikaa pamoja kuzungumza kwa uwazi. Sasa ni woga uliojengeka ndani yake kuwa anapingwa.
Ingawa ndani yake anakuwa na
wasiwasi, hadharani hujitahidi kuonesha anajiamini. Utamsikia akisema kwa maneno na vitendo kwamba hana haja ya msaada wa
yeyote katika kutekeleza majukumu yake. Matokeo yake ni kujenga sura ya
kutokuambilika, kutengeneza makundi ya kimaslahi, na hata kuimarisha visasi na
chuki dhidi ya wale anaohisi wanampinga.
Hali ya namna hii huendelea
kumsukumizia kwenye maisha ya upweke mbali na watu. Upweke humfanya awe na
hasira na watu, hali inayoweza kukomaza kutokuambilika kwake zaidi. Hakuna la
maana linaloweza kufanyika kwenye mazingira kama haya.
Heshima kwa unaowaongoza
Kwa kuwa ni dhahiri hakuna kiongozi
makini angependa kujikuta kwenye mazingira haya, ni vyema kujifunza kuwa
mnyenyekevu. Unyenyekevu ni kuelewa kuwa madaraka hayakufanyi uwe mtu usiye wa
kawaida.
Unapopewa madaraka, haina maana
unajua kila kitu. Bado unawahitaji watu wa kawaida kukusaidia kufanya kazi yako
bila kutumia nguvu. Unapoendelea kuwaheshimu na kuwasikiliza watu hawa unawafanya
wawe na msukumo wa ndani wa kukuheshimu.
Makala haya yalichapishwa awali na gazeti la Mtanzania.
Fuatilia safu ya Saikolojia kwenye gazeti hilo kila Alhamisi.
Kweli nimejifunza kitu kikubwa mno
JibuFutaDaniel kapuph
Futa