Kwa Nini Wazazi Tunawachapa Watoto?

PICHA: Mountain TV I Gilgit-Baltistan


‘Nakubaliana na njia unazopendekeza (kumfundisha mtoto tabia njema kwa kushirikiana nae). Lakini hii ya kutokumchapa sikubaliani nayo,’ ananiandikia msomaji mmoja na kuendelea, ‘Nina watoto wakubwa nimewachapa tangu wakiwa wadogo na wanakwenda vizuri tu […] Naelewa hatari ya kutokumwadhibu mtoto. Viboko vinasaidia sana sana kumnyoosha mtoto. Usipompa mapigo mtoto unakaribisha maradhi. Biblia iko wazi katika hili.’


Suala la viboko lina sura ya utamaduni wenye mizizi mirefu. Mjadala wake hauwezi kuwa mwepesi. Viboko, kwa hakika, vimekuwa kama sehemu ya maisha yetu. Takwimu sahihi za matumizi yake hapa nchini hazipatikani. Lakini inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia zaidi ya 80 ya wazazi wanaoishi kwenye nchi zinazoendelea wanawaadhibu watoto wao kwa kuwachapa angalau mara moja kwa mwezi.

Utamaduni wa kuchapa watoto haushii majumbani pekee. Hata walimu mashuleni na wanatumia viboko kuwaadhibu wanafunzi wasio na nidhamu. Mwanafunzi anapokosea atachapwa, wakati mwingine kwa mapigo makali.

Matumizi haya makubwa ya fimbo kwa kiasi fulani yanatokana na imani kwamba ili watoto wasikie tunachowaambia lazima tuwafanye wasikie maumivu. Ingawa hakuna ushahidi wowote kuwa viboko vinasaidia kujenga nidhamu kwa watoto, bado wazazi wengi –wakiwemo walimu– wanaamini adhabu ya fimbo ndiyo jibu muafaka la ‘kumnyoosha’ mtoto.

Jambo hili limefanyiwa utafiti kujua kitu gani kinawatofautisha wazazi wenye kutumia vikobo na wenzao wasiotumia njia hiyo. Makala haya yanajadili masuala matatu makubwa yanayojitokeza ambayo, kwa kiasi kikubwa, yanachangia kukithiri kwa utamaduni huu wa kuwachapa watoto.
 
Hasira

Katika utafiti mmoja, wazazi walitengwa katika makundi mawili kutegemeana na kiwango chao cha hasira kilichotathiminiwa kitaalamu. Walipowekewa mazingira ya kuwaadhibu watoto wao kwa makosa yanayofanana, tofauti ilikuwa bayana. Wazazi wenye hasira walikuwa wepesi kufoka na kutumia lugha ya matusi wakati wenzao wenye kiwango cha chini cha hasira hawakutumia mbinu hizo.

Sambamba na kufoka, wazazi wenye hasira walikuwa wepesi kutumia mabavu kuwarekebisha watoto wao ukilinganisha na kundi la pili ambalo, kwa kiasi kikubwa, lilitumia mbinu za kirafiki kuwarekebisha watoto wao.

Tafsiri ya utafiti huu ni kuwa hasira inaongeza uwezekano wa mzazi kutumia mbinu za kibabe ikiwemo fimbo kuwaadhibu watoto. Hasira, katika mazingira haya, zinakuwa ni kichocheo muhimu cha matumizi ya mabavu kwa mtoto.

Jambo hili linafanyika katika hali ambayo mzazi hawezi kuelewa kinachoendelea. Mara nyingi mzazi anapomchapa mwanae hufikiri anafanya hivyo kwa nia ya kumsaidia. Kwa kuwa mzazi asiye na hasira hawi mwepesi kutumia fimbo katika mazingira yale yale, maana yake lazima iwepo sababu nyingine zaidi ya ‘kumnyoosha mtoto.’ Sababu yenyewe ni kulipiza kisasi.

Mzazi mwenye hasira anapobaini mwanae anatenda kinyume na matarajio yake, hughadhibika. Nafsi yake hujisikia kudhalilika. Katika mazingira haya, mzazi wa namna hii anapomchapa mtoto kimsingi anajisaidia mwenyewe kupunguza hasira zake. Hiki ni kisasi ambacho kikichunguzwa vyema, hakina lengo la kurekebisha tabia ya mtoto bali kupunguza hasira.

Wengi wetu tuliosoma kwenye shule za kawaida ni mashuhuda wa hali hii. Walimu waliokuwa na hasira wengi wao ndio hasa waliopenda kuchapa. Hawakutuchapa kwa nia ya kutusaidia. Wakati mwingine, walifanya hivyo kutuonyesha kuwa hatuwezi kuwachezea. Hasira zao ndizo zilizokuwa msukumo wa kutumia viboko kama adhabu.

Utamaduni na imani

Wazazi waliochapwa, bila kujali kiwango chao cha hasira kama tulivyokwisha kujadili, hutumia mbinu hiyo hiyo kuwaadabisha watoto wao. Ilivyo ni kuwa vile ulivyolelewa wewe huathiri namna unavyowalea watoto wako mwenyewe.

Kwa kuwa ulichapwa na wazazi wako ukiwa mdogo, unajikuta ukiamini fimbo ndiyo njia sahihi ya kumwadabisha mwanao. Unaamini ulichotendewa ndicho sahihi kuliko kile ambacho hujawahi kuona kikitendwa na kikafanya kazi.

Kwamba ulichapwa na ukanyooka basi unaamini fimbo ni muafaka kumwadabisha mwanao. Lakini inawezekana usingechapwa bado ungeendelea kuwa kuwa hivyo ulivyo. Kwa sababu tu umefika hapo ulipofika na ulichapwa, inajengeka dhana tu kuwa kilichokunyoosha ni fimbo. Hakuna ushahidi.

Kama ambavyo wasiochapwa na wakaharibika wapo wengi, waliochapwa na wakaharibika nao pia wapo wengi. Huwezi kuhitimisha tu kuwa kwa kuwa wapo waliofanikiwa na walichapwa basi kilichowafanikisha ni fimbo. Lazima iwepo sababu zaidi ya fimbo.

Kimsingi nafasi ya fimbo kwenye malezi katika mazingira haya inakuwa ni imani tu. Ni mwendelezo wa utamaduni tulioukuta na tunafikiri unatufaa. Na kwa sababu hatufahamu mbadala wake, basi tunajisikia kuwajibika kuuendeleza vile ulivyo.

Wengine wanatumia vitabu vya dini kuhalalisha fimbo. Lakini ukweli wa mambo ni kwamba mara nyingi tunachapa kwa mazoea tu ya mila tunayoamini ni sahihi. Dini ni namna tu ya kuhalalisha mazoea yetu ambayo tungeyaendeleza hata kama hayajazungumzwa kwenye vitabu vya dini. Kwa kuwa hatuwezi kukubali kuwa kuchapa ni kujiridhisha wenyewe, basi tunatumia mafundisho ya dini kama mwamvuli.

Hali ya uchumi

Katika utafiti mwingine, wazazi wenye unafuu wa maisha walilinganishwa na wazazi wenye ukata. Makundi hayo mawili yalilinganishwa kwa mbinu wanazotumia kuwaadabisha watoto wao. Matokeo yalionyesha kuwa wazazi wenye hali ngumu kimaisha walikuwa na uwezekano mkubwa wa kutumia nguvu katika kuwaadabisha watoto wao kuliko wazazi wenye unafuu wa kimaisha.

Tafsiri ya matokeo hayo ni kuwa kadri mzazi anavyokuwa na msongo wa mawazo unaotokana na ugumu wa maisha ndivyo inavyokuwa rahisi kwake kutumia njia za mkato kumwadabisha mtoto. Ugumu wa maisha katika mazingira haya unahusianishwa kwa karibu sana na matumizi ya viboko.

Katika kuthibitisha haya, utafiti huo ulibaini kuwa kadri hali ya uchumi wa familia inavyozidi kuimarika, ndivyo matumizi ya fimbo yanavyozidi kupungua. Maana yake, wakati mwingine wazazi hujikuta wakitumia fimbo kama namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo.

Hiyo, hata hivyo, haimaanishi kuwa wazazi wenye hali nzuri ya kimaisha hawatumii fimbo bali uwezekano wa wazazi hawa kutumia fimbo unapungua.


Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?