Mzazi Ufanyeje Unapompeleka Mwanao Shule ya Bweni?
PICHA: Paul Jeffrey |
PAMOJA na
changamoto za malezi ya shule za bweni tulizoziona, bado mzazi anaweza
kulazimika kumpeleka mwanae kwenye shule hizi. Kwanza, kuna suala la kazi.
Wazazi wanaofanya kazi mbali na familia zao wanaweza kuamua kuwapeleka watoto
kwenye shule ya bweni ili wasiwe na wasiwasi na uangalizi wao.
Pili, hutokea
familia zikawa na misuguano ya kimahusiano. Wazazi wanaofarakana wanaweza
kuamua kumlinda mtoto kwa kumpeleka shule ya bweni. Lakini pia kuna suala la
watoto yatima wanaoachwa na wazazi, au watoto wanaozaliwa kwenye mazingira
yanayowanyima uhusiano wa kifamilia.
Sambamba
na hilo, kuna imani imejengeka kwa wazazi –wenye uwezo wa kiuchumi– kuwa
mazingira ya shule ya bweni yanamwezesha mtoto kujifunza vizuri zaidi kuliko
anapokuwa nyumbani.
Ndio
kusema yapo mazingira yanayoweza kufanya shule ya bweni isikwepeke. Makala haya
yanajaribu kuangazia mambo ya msingi kuzingatiwa mzazi anapoamua kumpeleka
mwanae kwenye shule za bweni.
Malezi yenye ubora
Kama
tulivyokwisha kuona, suala la ubora wa malezi kwenye shule hizi linaonekana
kuwa na changamoto nyingi. Ni kawaida kukuta shule nzima ikitegemea huduma ya
mlezi mmoja. Hali hii, kama tulivyoona, huathiri uwezekano wa mtoto kupata
msaada unaokidhi mahitaji yake ya pekee.
Jiridhishe
kuwa shule unayompelekea mtoto ina walezi wa kutosha. Idadi ya walezi iwiane na
idadi ya watoto wanaolelewa na mlezi mmoja. Lengo ni kuhakikisha kuwa watoto wanaishi
katika makundi madogo madogo yanayowawezesha kufahamiana na kushirikiana kwa
karibu.
Kwa
mfano, idadi ya walezi wanaowatazama watoto wadogo wa darasa la kwanza inabidi
iwe kubwa kuliko idadi ya walezi wanaowatazama watoto wa darasa la nne au la
saba. Mantiki ya utaratibu huu ni ukweli
kuwa watoto wadogo wana mahitaji mengi zaidi ya wenzao wenye umri mkubwa zaidi.
Kadhalika,
watoto wa umri mdogo hawana uwezo mzuri wa kusema mambo yanayowasibu hivyo
wanahitaji mtu wanayeweza kumwamini wamwambie mambo yao. Ni kwa msingi huo, epuka
shule inayokuwa na uwiano mdogo wa mlezi na watoto.
Vile
vile, kwa kuwa unampeleka mtoto mdogo kiumri mbali na wewe, jiridhishe kuwa
shule inatumia walezi wanaoweza kufanya wajibu wa mama. Hapa tunamaanisha kuwa
mlezi anayehudumia watoto anapaswa kuwa na utulivu, upendo na uelewa wa
mahitaji ya watoto pasipo kujisikia kukerwa na madai mengi ya watoto.
Ubora wa huduma
Katika
mipaka ya makala haya, ubora wa huduma ni kupatikana kwa malazi safi, chakula
bora, usalama na utaratibu mzuri wa usafi kwa watoto. Kadhalika, ubora unaweza
kumaanisha namna mazingira ya shule yanayolinda faragha na hadhi ya mtoto.
Tunapozungumzia
faragha tunaaminisha haki ya mtoto kuishi katika mazingira yasiyoruhusu
mwingiliano usio na mipaka kati ya mtoto na watu wengine wakiwemo watoto
wenzake. Mwingiliano huu ni pamoja na watoto kuchangia vitanda, watoto wengi
kulala chumba kimoja, kuchangia mahali pa kuweka vifaa vyao kwa namna ambayo
mtoto anapoteza umiliki wa vitu vyake.
Muhimu kujiridhisha
kuwa shule inawalaza watoto katika mazingira yanayoheshimu faragha ya mtoto
mmoja mmoja. Watoto wadogo wasichanganywe na watoto wakubwa wala kuishi. Mchanganyiko
wa watoto usiozingatia umri unaweza kufanya iwe rahisi kwa watoto wakubwa
kuwaambukiza wadogo zao tabia walizotoka nazo nyumbani.
Inaendelea
Maoni
Chapisha Maoni