Utamaduni wa Demokrasia Uanzie Ngazi ya Familia

PICHA: Dennis Louis
Tumesikia madai kuwa baadhi ya watawala wetu wa ki-Afrika ni madikteta. Watawala hawa wanashutumiwa kupuuza haki ya raia kueleza mawazo yao wazi wazi bila hofu ya ‘kushughulikiwa.’

Inavyoonekana wananchi wana matamanio ya kushiriki moja kwa moja katika shughuli za kudhibiti serikali wanazokuwa wameziweka madarakani. Bahati mbaya watawala wanapopata madaraka huziba masikio yao sambamba na kuhakikisha vivywa vya wananchi haviwezi kusema kinyume na maoni waliyonayo watawala.


Kutokufikiwa kwa matamanio haya ya wananchi katika kuamua aina ya utaratibu utakaotumika kujitawala kunawafanya wajisikie kuminywa na hata kunyang’anywa haki muhimu ya raia kujieleza.  

Hata hivyo, ni dhahiri kuwa watawala wa nchi hutokana na jamii inayowachagua kuwasaidia kufikia malengo yao. Haiba, hulka na mienendo ya watawala haiwezi kuwa tofauti na hali halisi ya wananchi wao.  Wanayoyafanya –kwa kujua au kutokujua– ni  sura halisi ya utamaduni wa wananchi.

Tutumie mfano. Wananchi wanaothamini elimu, hutafuta na kuchagua miongoni mwao viongozi wanaothamini elimu. Kinyume chake, wananchi wasiothamini elimu huweza, na kwa kweli hufurahia, kuchagua wajinga wenzao kuwa watawala wao.

Vivyo hivyo, wananchi wanaopenda njia za mkato kujipatia kipato, huthamini na kuwachagua wagombea ‘wajanja wajanga’ ambao baadae kuja kufahamika kama mafisadi. Haiwezekani viongozi kuwa tofauti na wananchi.


Tukizitazama nchi zinazosifika kwa demokrasia tunabaini kuwa demokrasia [katika nchi hizo] ni utamaduni wa wananchi. Demokrasia ni maisha yanayoanzia kwenye utawala wa familia. Kila mwanafamilia anajengewa mazingira ya kujisikia kuwa na uhuru wa kuchagia maoni yake.

Mtoto hupewa nafasi ya kufanya maamuzi kwa mwongozo wa mzazi. Mke naye anakuwa na fursa ya kushiriki katika maamuzi anayoyafanya mumewe kwa sababu demokrasia katika jamii hizo ni utamaduni unaoanzia kwenye familia na sio matamanio bandia ya kisiasa.

Ninapotafakari madai ya raia katika nchi zetu kutaka watawala wetu wawe wanademokrasia, maswali kadhaa yanajitokeza. Ninajiuliza, kwa mfano, tunaweza kweli kudai kuwa sisi ni jamii inayoamini katika demokrasia kuanzia ngazi ya familia? Je, demokrasia ni utamaduni wetu? 

Sisi wanaume wa ki-Afrika, mathalani hatutishwi na kukua kwa demokrasia kwenye ngazi ya familia zetu? Tunawashirikisha kweli wake zetu katika maamuzi bila kuwawekea mipaka? Tunaheshimu maoni ya watoto wetu kama tunavyotaka watawala wetu waheshimu maoni yetu?

Kwamba tunahitaji demokrasia kwenye vyama nyetu vya siasa na serikalini hili halina mjadala. Lakini je, tunaweza kuwalaumu watawala/viongozi wanaoonesha hulka za kidikteta kama sisi wenyewe ni madikteta wa familia zetu?

 Je, sisi madikteta wa familia zetu (tusiowapa wake/waume/watoto wetu uhuru wa maoni kwa kuogopa kukosa mamlaka yetu kama wazazi/wanaume) tunaweza kuwa na uhalali kwa kudai hatupendezwi na viongozi wa ki-Afrika wanaoonesha hulka na tabia za madikteta?

Tunayo mapendekezo mawili. Kwanza, ili tuweze kujenga taifa linaloamini uhuru wa mawazo kweli kweli, tuanze kujenga demokrasia ya kweli ndani ya familia zetu. Tuanze kuzishirikisha familia zetu katika maamuzi bila  hofu ya kupokonywa madaraka yetu. Tuanze kuthamini na kuheshimu maoni/mahitaji ya watoto wetu na kuyasikiliza. Tujenge taifa la kweli la watu wanaoamini demokrasia.


Tukishindwa pendekezo la kwanza, basi, tuamue kuwa wakweli wa dhamira zetu kuwa sisi ni madikteta kwa asili. Tuunge mkono udikteta wa ngazi ya taifa ambao kwa hakika utakuwa unaakisi utamaduni wa udikteta tuliouzoea katika familia zetu. 

Makala haya yalichapishwa awali kwenye gazeti la Mtanzania. Unaweza kufuatilia safu ya Uwanja wa Wazazi kwenye gazeti hilo kila Alhamisi kwa makala kama hizi.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?