Kuyamudu Mafanikio Yako...
Fikiria
umehitimu masomo kwenye chuo maarufu; umepata alama nyingi kwenye mtihani
mgumu; umepata kazi yenye heshima; umejenga nyumba nzuri; umenunua gari la
ndoto zako; umesafiri kwenda mahali wanakotamani kwenda watu na hawawezi au
basi tu umekutana na mtu fulani maarufu.
Unajisikiaje
kama watu hawatafahamu? Kwa nini watu wakifahamu unajisikia vizuri zaidi?
Kwa wengine
wetu, mafanikio yetu yasipofahamika kwa wengine haturidhiki. Tunapima thamani
ya tulichonacho kwa kuangalia wengine wanavyokikubali. Ndani yetu unakuwepo
msukumo wa kutamani wengine waone mema yanayotutokea. Furaha ya binadamu ni
kufanikiwa. Hakuna asiyependa kufanikiwa na ni vigumu kuficha mafanikio.
Ukifanikiwa watu wataona na wataambiana.
Hata
hivyo, hali hii ya kupenda mafanikio, inaweza kuchukua sura ya mashindano. Mtu
anaweza kushindwa kuvumilia mafanikio yajitangaze yenyewe. Anaweza kujikuta
akitumia nguvu nyingi kutangaza. Anatamani kila anayekutana naye asikie. Bahati
mbaya kufanya hivyo huleta matokeo hasi kama nitakavyofafanua.
Binadamu
(kwa asili yake) ni mtu wa mashindano. Kimya kimya, tunashindana sisi kwa sisi.
Nani ana nini na mimi nina nini. Tunajilinganisha. Ukiwa na kizuri
wasichonacho, unajihesabu umefanikiwa. Ukikosa kizuri walichonacho wengine,
unanyong'onyea. Sehemu kubwa ya maisha yetu ni KUJILINGANISHA. Hulka hiyo ya
kushindana hutufanya tuwaonee wivu (na hata ikibidi kuwachukia) wale
wanaoonekana kutuzidi.
Unapotangaza
mafanikio yako zingatia hilo. Asiye na hicho ulichonacho, hatakuwa mwepesi
kukupa heshima unayoitarajia. Sababu? Anatafsiri heshima yako kama udhaifu
kwake. Hatakubali ajione dhaifu kirahisi. Ndio maana atakusema, atakupinga na
ikibidi kukudhalilisha. Kwa nini? Mashindano.
Ni vizuri
kabla hujawaambia watu mafanikio yako jiulize, 'Hivi ni lazima wajue? Wakijua
watanufaika? Kama ni muhimu wajue, je siwezi kuwaacha wakajua wenyewe? Hadhi
yangu inategemea namna watu wanavyoniona?'
Pengine
tunahitaji kujifunza kumudu mafanikio. Kama si lazima, usiwaumize watu kwa
kuwaonesha kile unachojua hawana. Waache waone wenyewe na ikibidi waambiane
wenyewe. Unapotumia mikakati kuwajulisha, inakuwa kama mtu anayekwenda kula
keki katikati ya watu wenye njaa. Hawataelewa mantiki yake, hata kama wanaweza
kutoa pongezi kwa maumivu. Uzuri ni kwamba anayejitambua, hawaumizi wengine
kihisia.
Ni kweli kabisa hiyo ndio tabia yetu binadamu na kutokana na hii tabia ya kutaka kujionyesha tumempa Markzagart faida ya kuuunda facebook ambapo humo kazi yetu n kuonyesha mafanikio,
JibuFutakwa nn tusiache watu wayaone wenyewe live mpaka tu post mitandaoni...
tubadilike jamani