Kanuni Nne za Kufurahia Kazi Yako
Kwa
nini unaamka asubuhi kwenda kazini? Kitu gani kinakupa sababu ya msingi ya
kwenda kazini? Ni dhahiri vigezo
tunavyovitumia kufurahia kazi haviwezi kufanana.
Wapo wanaofurahia kiwango kikubwa
cha mshahara. Thamani ya kazi inategemea na ukubwa wa kipato. Wengine
wanaridhika na kazi inayowajengea hadhi katika jamii. Kazi inayowaongezea hadhi
inawapa kuridhika.
PICHA: Dreamstime.com |
Pia,
wapo wanaoridhika na kazi inayowapa utulivu. Hawa hata kama kazi yenyewe
hailipi, wala haiwapi heshima kubwa katika jamii, ikiwa tu inaweza kuwapa
uhakika wa kuishi bila kuwa na wasiwasi wa kukosa kazi kesho, wanatulia.
Ingawa
kila mmoja ana sababu zake, kwa ujumla, namna gani mwajiri wako amekuwekea
mazingira yanayokuwezesha kutekeleza majukumu yako, kwa kukulipa kiwango
kinacholingana na thamani yako, kukutambua, kukupa uhakika wa kazi ni baadhi ya
mambo yanayoweza kukuongezea furaha ya kazi.
Hata
hivyo, tafiti za ajira na kazi zinaonyesha kuwa mtazamo binafsi wa mfanyakazi
una nafasi kubwa ya kumwongezea furaha ya kazi anayoifanya. Makala haya
yanaangazia kanuni nne unazoweza kuzitumia kufurahia kazi unayofanya na hivyo
kuongeza tija yako kazini.
Fahamu kinachokuridhisha
Kuelewa
kitu gani kinakufanya uone thamani ya kazi unayoifanya kunaweza kukuongezea
furaha ya kazi. Watu wasio na hakika ya kitu mahususi kinachowapa furaha
maishani mwao, ni vigumu kuridhika na kazi.
Jiulize,
kitu gani kilikuhamasisha kuomba kazi uliyonayo leo? Je, msukumo gani hasa
unakufanya uendelee kwenda kazini? Je, usingekuwa na kazi uliyonayo, ungekuwa
na furaha zaidi?
Majibu
ya maswali haya yanaweza kukusaidia kutathmini kiwango chako cha kuridhika na
kazi uliyonayo. Ni dhahiri pia kuwa ari na msisimko wa kazi hupungua kadri mtu
anavyoizoea kazi yake. Kadhalika, mahitaji yetu ya kisaikolojia, kiuchumi na
kijamii hubadilika kadri miaka inavyokwenda.
Hata
hivyo, unapotambua kiwango chako cha kuridhika na kazi, unaweza kuchukua hatua
stahiki. Si mara zote unapokosa msisimko wa kazi maana yake uache kazi. Wakati
mwingine kubadili namna unavyoitazama kazi yako kunaweza kukusaidia. Kazi
unayoona haina maana leo, wapo watu maelfu ambao pengine wanaota siku moja
wangeipata. Labda huipendi kwa sababu ya namna unavyoitazama.
Jitambulishe na kazi yako
Ujasiri
wa kujitambulisha na kazi yako ya sasa unakusaidia kuipenda zaidi kazi yako. Kufurahia
kazi yako ya sasa haimaanishi usiwe na ndoto za kufanya kazi nyingine. Si watu
wengi wanafanya kazi walizotamani kuzifanya.
Hata
hivyo, kutokuridhika na kazi uliyonayo tayari, kwa kiasi kikubwa, kunaathiri
ufanisi wako. Unapokosa furaha na kazi yako, inakuwa rahisi kwako kukosa hamasa
ya kuwa mbunifu; hutajituma na inaweza kuwa vigumu kwako kuleta matokeo
yanayoweza kukupeleka kule unakotaka kwenda.
Jizoeshe
kujitambulisha na kampuni yako. Jione kama sehemu muhimu ya kampuni au taasisi unayoifanyia
kazi badala ya kujichukulia kama mpitaji. Kuwa tayari kuitetea kampuni au
taasisi yako mbele ya macho ya umma.
Kutokujisikia
fahari na kazi unayoifanya kunakuondolea furaha ya kazi. Kadri unavyoendelea
kudanganya mahali unakofanya kazi, kwa sababu ya imani kuwa ikifahamika
itakupunguzia heshima unayopata kwa kutokufahamika, ndivyo unayokuwa kwenye
mazingira ya kukosa amani na hapo ulipo. Fanya kinyume. Jitambulishe wazi wazi
hata kama unajua wapo watu wenye mtazamo hasi na aina ya kazi unayoifanya.
Kujiamini kutakuongezea furaha.
Kuwa na bidii na ushirikiano
Heshima
inayotokana na kazi ya mtu, kwa kawaida, inaongeza furaha ya kazi. Kule
kujisikia kuwa mchango wako unatambuliwa, uwepo wako unahitajika, inakupa heshima.
Lakini ili uweze kuheshimiwa kazini, unahitaji kujituma. Fanya kazi kwa bidii.
Ione kazi yako kama njia halali ya kukusaidia kupata heshima unayohitaji kuwa
nayo.
Ni
kweli kuwa wakati mwingine unaweza usijikie kujituma kwa sababu labda mazingira
ya kazi sio rafiki. Hakuna kazi inaweza kukujengea mazingira yasiyo na kasoro
yoyote. Pengine hujioni ukitumia vipaji vyako ipasavyo. Hakuna kazi yoyote
unayoweza kuifanya na ikatumia vipaji ulivyonavyo kikamilifu.
Vipaji
vyako vinaweza kutumiwa na karibu kila kazi unayoifanya. Labda hujajituma vya
kutosha. Ukiweza kujituma kikamilifu kwenye kazi hiyo unayoifanya, unaweza
kushangaa namna utakavyotumia vipaji usivyovutumia hivi sasa. Kadri
unavyovitumia vipaji vyako, ndivyo utakavyojisikia kuridhika zaidi.
Kadhalika,
jenga uhusiano mzuri na wenzako. Mahusiano mabaya kazini yanachangia kuondoa
furaha ya kazi. Huwezi kuridhika na kazi inayokukutanisha na watu msioelewana. Shirikiana
na wenzako badala ya kushindana nao. Wape msaada wanaouhitaji kukamilisha kazi
zao. Kwa kufanya hivyo, utashangaa namna wanavyofurahia kufanya kazi na wewe na
hiyo itakuongezea furaha ya kazi.
Rekebisha namna unavyoyachukulia
maisha
Mtu
asiye na furaha na maisha yake ya kawaida, anakuwa na uwezekano mdogo wa
kufurahia kazi yake. Unapokuwa na utulivu na mtazamo chanya na maisha, inakuwa
rahisi kwako kuipenda kazi yako. Kinyume chake pia ni kweli. Usipokuwa na furaha
na maisha, hutafurahia kazi yoyote utakayopewa.
Tafsiri
yake ni kuwa unahitaji kurekebisha mtazamo wako wa jumla na maisha ili uweze
kuona thamani ya kazi unayoifanya. Pengine unashindana na watu. Kila
unachokifanya unakiweka kwenye mizani ya kile unachofikiri watu wengine
wanakifanya.
Pengine
unajifikiria mwenyewe kuliko mchango unaoutoa kwa watu wengine. Labda ni wakati
wa kufikiri upya. Je, maisha ni kujifikiria mwenyewe? Je, fedha na mali ndilo
lengo kuu la maisha? Hakuna kusudi jingine kubwa zaidi ya kupata mahitaji yako
ya kila siku?
Pengine
vile unavyoyachukulia maisha ndiyo tatizo. Ukibadili mtazamo wako wa jumla wa
maisha, unaweza kugundua namna kazi yako ilivyo na thamani kubwa kuliko
unavyofikiri.
Maoni
Chapisha Maoni