Shirikiana na Mtoto, Usishindane Nae
Tunaendelea kujibu swali
linaloulizwa na wazazi wengi, ‘kwa nini watoto hukosa adabu?’ ‘Kwa nini wakati
mwingine watoto hawasikii hata pale wanapoadhibiwa?’ ‘Inakuwaje mtoto anakuwa
na nidhamu mbele ya mzazi lakini akiwa mbali na mzazi anakuwa na tabia
nyingine?’
Jibu la maswali haya ni mjadala
mrefu. Hata hivyo, tumejaribu kuonyesha kwamba mtoto kukosa adabu haitokei kwa bahati
mbaya. Kwanza, hazaliwi na msukumo wa kushindana wala kumkosea adabu mzazi. Badala
yake, huzaliwa na fahari ya kumpendeza na kushirikiana na mzazi. Kwa mfano, mtoto
hufurahia mzazi anapocheza nae, anapomkumbatia, anapomrusha rusha kwa furaha na
hata anapomtania.
PICHA: Atum Azzahir |
Matendo yanayoimarisha ukaribu huu
na mzazi, kwa kawaida, humsaidia mtoto kujisikia salama. Anakuwa hana sababu ya
kuwa na wasiwasi na usalama wake akiamini wanaomzunguka ni watu wanaoaminika.
Utulivu wa namna hii hujenga ari ya kushirikiana na mzazi inayomfanya kuwa
msikivu.
Lakini kadri mtoto anavyokua
kimwili, mara nyingi mzazi hupunguza jitihada za kushirikiana nae. Kama alizoea
kucheza nae, anaanza kusita kufanya hivyo. Wakati mwingine, mtoto mwingine huzaliwa.
Mzazi huyu hujikuta akitumia muda mwingi kumpa ushirikiano mtoto mchanga
aliyeongezeka kwenye familia. Jitihada hizo za kumfurahia mtoto mchanga hufanyika
katika mazingira ambayo mtoto ‘mkubwa’ anayeanza kujisikia umbali na wazazi
wake, akishuhudia.
Hali kama hizi, zinamjengea
uhitaji mkubwa wa ndani kwa ndani. Mtoto anakuwa na shauku ya ukaribu usiopatikana.
Ukaribu unapokosekana huchochea jitihada za kuziba pengo. Moja wapo ya jitihada
hizi ni kufanya vituko ambavyo mzazi anaweza kuvitafsiri kama kukosa nidhamu.
Ni vizuri kutambua kuwa mtoto anapofanya
hivyo, nia yake hasa si kumuudhi mzazi. Hapana. Hawezi kutaka kumuudhi mzazi
kwa sababu, kwa asili, ana shauku ya kushirikiana nae.
Usipuuze hisia za mwanao
Kama tulivyoona, mara nyingi mtoto
hutafsiri yale anayotendewa kwa namna inayoweza kuwa na upotofu. Unaweza
kufanya kitu kidogo pasipo nia mbaya. Labda umeahidi zawadi na hujatekeleza.
Labda umemkejeli mbele ya wenzake. Labda umemwambia mtoto mwingine maneno
mazuri na hujamwambia yeye. Kwako uliye mtu mzima, huoni tatizo. Kwa kujua
hukuwa na nia mbaya, unaweza ukaamua kupuuza vile anavyojisikia mtoto kwa
sababu unajua hayo anayoyafikiri hayana ukweli wowote.
Jambo la kuzingatia ni kuwa hisia
hata kama zimejengwa kwenye dhana potofu zinaathiri kwa kiasi kikubwa mtazamo
wa mtoto. Mtazamo potofu huongoza maamuzi potofu anayoyafanya mtoto. Mathalani,
mtoto anayeamini hapendwi hata kama kiukweli anapendwa atakuwa tayari
kushindana na mzazi. Kushindana na mtoto mwenye mtazamo potofu kunaweza kuchangia
kukuza tabia mbovu.
Makala haya yanalenga kusisitiza
umuhimu wa kuvaa viatu vya mtoto na kuelewa hisia zake, anafikiri nini, anaamua
nini na kwa sababu gani. Hata hivyo, katika kufanya hivyo, ni muhimu kuchukua
tahadhari tatu kubwa. Kuepuka kumdekeza mno mtoto, kumdhibiti na kumwadhibu
kupita kiasi.
Kumdekeza mtoto
Kudekeza ni kumlinda mtoto kupita kiasi
kwa lengo la kumfanya ajione mtu mwenye umaalum usio wa kawaida. Wazazi wenye
mtoto mmoja, mathalani, wanakuwa na uwezekano mkubwa wa kumchukulia mtoto kwa
umaalum. Mtoto anayedekezwa hufikia kujiona bora kuliko watu wengine.
Unapomdekeza mwanao kumbuka kuwa
unatengeneza hatari ya kumfanya aamini usalama wake unategemea kiasi gani anajidekeza
kwako. Pia, anaweza kujiona mtawala anayeweza kuwaendesha wengine atakavyo
yeye.
Kwa upande mwingine, mtoto huyu
ana uwezekano mkubwa wa kushindwa kufanya vitu vingi bila msaada wa mtu
mwingine, upungufu unaoweza kufanya maisha yake yawe magumu pindi atakapoondoka
nyumbani.
Ili kuepuka kumdekeza mtoto, punguza
kumwonea huruma. Mpe nafasi ya kukabiliana na magumu na hata ikibidi kuumia kidogo
kwa lengo la kujifunza maisha halisi. Usimnyime mwanao maumivu, lakini pia
usimwumize bila sababu.
Kumdhibiti kupita kiasi
Kumdhibiti mtoto ni kumwongoza
kupita kiasi na kutompa nafasi ya kushiriki kufanya maamuzi. Kila anachofanya
mtoto ni matokeo ya amri zisizotoa nafasi ya majadiliano. Atakwenda wapi, asoma
nini, atapenda nini, yote hayo ni juu ya mzazi.
Mtoto anayedhibitiwa namna hii
anaweza kuonekana ni mtu mwenye nidhamu kwa nje. Lakini kama mwanadamu
mwingine, ndani yake kunakuwa na kiu ya kujiona ni mtu mwenye maamuzi na maisha
yake. Mtoto huyu anapopata nafasi ya kufanya vitu vyake mara nyingi hufanya
makosa mengi.
Papara ya maamuzi ambayo mara
nyingi huwa kinyume na matakwa ya wazazi, inatokana na ukweli kuwa hajiamini.
Hajajengewa kuuamini uwezo wake ingawa ndani kunawaka shauku ya kuthibitisha
kuwa anaweza kufanya maamuzi.
Ili kukabiliana na athari za
kumdhibiti mno mwanao, jitahidi kumpa uhuru wenye mipaka kulingana na umri
wake. Mpe nafasi ya kufanya maamuzi yanayolingana na umri wake. Nafasi yako
kama mzazi ibaki kuwa kumhakikisha usalama wake na kuhakiki maamuzi yake.
Unavyomwadhibu
Mtoto anapoanza kushindwa
kushirikiana na wazazi, ni kawaida kwa mzazi kutumia adhabu. Mfano, kumkemea,
kumfokea, kumchapa, kumfinya na hata kumnyima vile anavyovihitaji.
Lakini unapomwadhibu hususani kwa
adhabu kali, mtoto hujenga dhana potofu. Kwake, adhabu maana yake ni ‘naonewa,
sieleweki.’ Hisia hizi mara nyingi huambatana na woga wa kuogopa adhabu, hali
inayoweza kumfanya alazimike kufanya vitu anavyojua vinahitajika hata kama havianzii
ndani yake.
Mtoto anayeadhibiwa mara kwa mara,
hujenga sura isiyo yake kwa lengo la kumridhisha mzazi. Sura hii inaweza
kupotea atakapokuwa mtu mzima, au atakapoondoka nyumbani na kuanza kujitegemea.
Upande mwingine wa adhabu ni mtoto
huanza kujenga hisia za kisasi ndani yake. Anaweza kufanya vitu kwa lengo la
kushindana na matokeo yake kuathiri ukaribu wake na mzazi.
Ni vyema kutumia adhabu kama njia
ya mwisho ya kumsaidia mwanao. Mwadhibu mtoto kwa upendo, na rudisha uhusiano
baada ya adhabu. Kadhalika, usijenge mazoea ya kumwadhibu mwanao ukiwa na
hasira.
Maoni
Chapisha Maoni