Fanana na Unayetaka Asikilize Nasaha Zako
Fikiria mtoto amekuwa na tabia ya
kufanya vibaya darasani. Wewe kama mzazi hupendi hali hiyo. Ungetamani mtoto
afanye vizuri. Kwa shauku hiyo, unaona uongee na mwanao kumhamasisha afanye
juhudi kwenye masomo.
Unamwambia, 'Hebu jitahidi mwanangu. Alama
hizi unazopata hazifai. Mimi sijawahi kupata alama hizi. Nilipokuwa na umri
kama wako, nilikuwa na bidii sana kwenye masomo. Kwa sababu ya kufanya bidii, siku
zote nilishika nafasi kati ya nambari moja na tatu darasani!'
Lengo ni jema kabisa. Unachofikiri hapo
ni kuwa mwanao akisikia simulizi la mafanikio yako, atahamasika na kuanza
kujitahidi. Unafikiri uwezo wako unaweza kumtia hamasa kijana. Inawezekana ikawa
hivyo. Lakini mara nyingi mambo huwa kinyume.
Unapomwambia kijana namna ulivyokuwa
ukifanya vizuri, unaweza kuibua hisia mchanganyiko. Kijana wako anaweza kusikia
ujumbe tofauti na huo. Kichwa chake kinaweza kuchakata taarifa tofauti kabisa. Ujumbe
huo huo ukasikika, 'Mimi baba yako nilikuwa mtu mwenye akili sana. Nashangaa
kwa nini wewe ni mjinga kiasi hiki.'
Tafsiri hiyo inafanya nafsi ya mtoto
ijisikie kudhalilika. Hakuna mtu anapenda kujisikia dhalili. Ili kukabiliana na
udhalili huo, mtoto anafikiri, 'Huyu mzee anajiona kichwa sana. Hapa ameniita
kunizodoa tu. Sasa nitakachofanya ni kuachana nae. Kwanza haelewi mambo yalivyo
magumu shuleni siku hizi.'
Kufanana ni kuvaa viatu vyake
Kwa kawaida, watu wanavutiwa na wale wanaofanana nao; wanaoishi
maisha kama yao; wenye changamoto kama zao. Hujisikia vizuri kuona mtu
anayewashauri, anaelewa maisha yao, yuko kama wao.
Ni vigumu kumvutia mtu unayemwonesha ulivyo tofauti nae.
Unapomfanya ajione tofauti na wewe, labda kwa kuwa na uwezo asionao yeye, anakata
mawasiliano na wewe. Akiisha kukata mawasiliano hayo, anawasha taa
itakayomsaidia kumwulika ujumbe wako kwa kuukosoa; kuubatilisha ili kuhalalisha
kwa nini yeye anapata matokeo tofauti na hayo unayomsimulia. Matokeo yake
hawezi kufurahia kuusikiliza hata kama ujumbe wako ungemsaidia.
Usijitofautishe
Nasaha na ushauri mwingi mzuri hukosa kibali kwa walengwa. Wanaoshauri
hutumia nguvu nyingi kujitofautisha na wanaolengwa. Tofauti hiyo inakaribisha
shughuli ya ujumbe huo kupigwa.
Mfano, mzazi anaongea na vijana wenye changamoto za mahusiano ya
ujana. Pengine kwa kufikiri anaweza kuwahamasisha, anatumia muda mwingi
kusimulia namna yeye alivyokuwa na 'ujana mtakatifu.' Vijana hawa ambao tayari
hawana huo utakatifu, wanajisikia dhalili. Hawatamsikiliza. Fikra zao zitakata
mawasiliano na kuanza kuhoji yasiyolengwa. Watahoji ukweli wa yanayosemwa; tofauti
ya mazingira ya wakati huo na haya waliyonayo wao na kwa kweli uwezekano wa wao
kupokea ujumbe huo ni mdogo.
Kumwelewa
unayemshauri
Vijana hawa ambao tayari wanaishi kwenye changamoto wanahitaji mzazi
mwenye ujasiri wa kwanza, kuelewa mazingira yao na waamini kuwa anaelewa. Pili,
ili wamwamini mzazi huyu anahitaji kuwa na ujasiri wa kuwaambia namna yeye
mwenyewe alivyokuwa kama wao lakini akajifunza kushinda changamoto hizo kama
zao.
Kijana mwenye changamoto anapoyaona maisha yake kwa mzazi huyu,
atafungua moyo wake kujifunza kwa vipi anaweza kuiga mbinu za kufanikiwa. Ndio
kusema, mapungufu, makosa na udhaifu vikisemwa vizuri vinaweza kuwa na nguvu ya
kumbadilisha mtu kuliko masimulizi ya mafanikio.
Kwa wazazi, kama kweli unataka kijana wako ahamasike kuchukua
hatua za kubadilisha tabia yake, huna sababu ya kumsimulia namna ulivyokuwa
bora kuliko yeye. Mfanye ajione kwenye maisha yako. Atahamasika kubadilika.
Maoni
Chapisha Maoni