Unaweza Kumfundisha Mtoto Adabu Bila Kumchapa

Mjadala wa fimbo na malezi una historia ya mjadala mkali. Fimbo, kwa hakika, zimekuwa kama sehemu ya maisha yetu. Takwimu zinathibitisha hali hii. Kwa mfano, asilimia zaidi ya 80 ya wazazi wa nchi zinazoendelea wanatumia fimbo angalau mara moja kwa mwezi. Ndio kusema, vipigo kwa watoto vimekuwa sehemu ya malezi katika nchi zetu hizi.

Matumizi haya makubwa ya fimbo kwa kiasi fulani yanatokana na imani waliyonayo wazazi kuwa bila mtoto kusikia maumivu hawezi kurekebisha tabia wala kuwa msikivu. Ingawa hakuna ushahidi wowote kuwa viboko vinasaidia kujenga nidhamu kwa watoto, bado wazazi wengi wanaamini adhabu ya fimbo ndiyo jibu la kumnyoosha mtoto.

PICHA: Awo Aidam Amenyah

Hebu tutazame kwa ufupi sababu zinazochangia kukuza utamaduni huu, athari za kuamini fimbo ndiyo suluhu ya matatizo ya kinidhamu na mwishoni tuone ikiwa tunaweza kupata mbadala wake.

Sababu za kutumia fimbo

Zipo sababu nyingi zinazohusianishwa na matumizi ya fimbo ambayo mara nyingine yanazidi kiasi.

1.      Hasira za mzazi

Huwezi kutenganisha fimbo na hasira. Hiyo ni kwa mujibu wa tafiti za kisayansi. Kuchapa ni kulipiza kisasi kwa kile mzazi anachoona hakijafanywa sawa sawa na mwanae.

Tunafahamu, kwa mfano, unapokuwa na hasira ni rahisi kufoka, kupiga kelele zisizo na sababu na wakati mwingine matusi. Haya yote hayalengi kurekebisha tabia ya mtoto bali namna fulani ya kulipiza kisasi. Na kadri hasira inavyoongezeka, ndivyo uwezekano wa fimbo kugeuka kuwa shambulizi unavyozidi kuwa mkubwa.

2.      Hali ngumu ya kiuchumi

Ndio ukweli wenyewe. Ugumu wa maisha unahusianishwa kwa karibu sana na matumizi ya viboko. Zipo tafiti zilizohusianisha umasikini wa kipato na ongezeko la hasira kwa wazazi. Ilivyo ni kwamba umasikini huchangia sana hali ya kukosa uwezo wa kudhibiti hasira.

Katika kuthibitisha haya, tafiti zinaonesha kadri hali ya uchumi wa familia inavyozidi kuimarika, ndivyo matumizi ya fimbo yanavyokuwa na uwezekano wa kupungua. Maana yake, wakati mwingine wazazi hujikuta wakitumia fimbo kama namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo.

3.      Kudumisha mila/imani

Wakati mwingine ni ukweli kuwa watu huamini vibokoni njia sahihi zaidi ya kumwadabisha mtoto kwa sababu tu wao wenyewe walichapwa na wazazi wao. Kwamba ulichapwa na ukanyooka basi unaamini fimbo ni muafaka kumwadabisha mwanao. Hata hivyo, imani hii yaweza kuwa mwendelezo wa mila uliyokulia wewe hata kama huenda, kihalisia, ungeweza kunyooka bila fimbo.

Wengine wanatumia vitabu vya dini kuhalalisha fimbo. Lakini ukweli wa mambo ni kwamba mara nyingi tunachapa kwa mazoea tu ya mila tunayoamini ni sahihi na dini ni namna tu ya kuhalalisha mazoea yetu. Hata kama tunaamini kuchapa kunasaidia kumwadabisha mtoto, kisayansi, tunachapa kupunguza hasira zetu zaidi. Na kwa sababu hatutaki kukubali kuwa kuchapa ni kujiridhisha wenyewe, basi tunatumia mafundisho ya dini kama mwamvuli.

4.      Jinsia na umri wa mtoto

Unaweza kushangaa lakini ndio ukweli wenyewe wa kisayansi. Takwimu zinasema mtoto wa kiume ana uwezekano mkubwa wa kuchapwa zaidi kuliko mtoto wa kike. Ipo imani isiyowazi kuwa adhabu kwa mtoto wa kiume ni lazima iwe nzito na yenye kuleta maumivu zaidi zaidi kuliko kwa msichana. Ni aina fulani ya mfumo dume unaojenga fikra za ubabe na mabavu kwa watoto wa kiume.

Kadhalika, kuna ukweli pia kuwa umri wa mtoto unahusianishwa kwa karibu sana na matumizi ya fimbo kwa wazazi wenye kuamini katika fimbo. Kwa mfano, katika umri wa kati ya miaka mitano na kumi na mitano, takwimu zinaonesha hapa ndiko fimbo zinakotumika zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Sababu kubwa ni kwamba katika umri huu mtoto ndio kwanza anajaribu kufanya vitu vingi katika mazingira yake na hivyo kujikuta katika mgogoro wa mara kwa mara na wazazi. Anapokuwa na wazazi ‘wasiopenda ujinga’ ni rahisi sana kujikuta matatani mara kwa mara.

Madhara ya fimbo kwa mtoto

Viboko vimethibika kuwa na madhara makubwa katika makuzi ya mtoto. Ukiacha madhara ya kimwili yanayoweza kutokana na majeraha ya viboko, tutazame matatizo makubwa matatu ya kisaikolojia.

1.      Huathiri uhusiano

Fimbo, kama tulivyoona, huenda sambamba na hasira na matumizi mabaya ya maneno. Matokeo yake ni kudhuru uhusiano wa mzazi na mtoto iwe kwa muda mfupi au kwa muda mrefu. Mtoto anayechapwa hujiona kama mtu asiye maana kwa mzazi wake hasa kama mzazi hana tabia ya kukarabati mahusiano upya na mwanae baada ya kumchapa. Vile vile, wakati mwingine wazazi huwachapa watoto wao bila staha (mbele ya wenzao, hadharani). Hii huweza kutafsirika kwa mtoto mwenyewe kama kumkosea adabu.

Pia wazazi wengi wanaochapa huwa hawakumbuki kukaa na watoto kufafanua sababu ya kuwachapa na kuonesha mbadala. Mara nyingi hili haliwezekani kwa sababu mzazi mwenye uwezo wa kufanya mazungumzo ya namna hii baada ya fimbo, maana yake angeweza kabisa kuachana na mpango wa fimbo. Kukosekana kwa ukaratabi huu baada ya adhabu ya fimbo watoto huachwa na majeraha moyoni ambayo, pasipo hatua kuchukuliwa, huathiri mitazamo ya watoto bila wao wenyewe kujua.

2.      Husababisha usugu

Fimbo zina tatizo la kuzoeleka. Kadri inavyotumika kumsababisha maumivu mtoto, ndivyo inavyobidi iwe kali zaidi ili iendelee kumfanya mtoto apate maumivu yanayotarajiwa. Na kadri inavyoendelea kuwa kali zaidi, ndivyo inavyozidi kugeuka kuwa ugomvi wa kibinafsi na hivyo kujenga usuguwa kitabia ikiwa tahadhari stahiki hazitachukuliwa.

Watoto waliokulia kwenye mazingira ya vipigo, ni watu sugu hata katika mahusiano yao na watu wengine. Wengi huwa hawana uwezo wa kujua hisia za wengine kwa sababu wamekulia kwenye mazingira yaliyowazoeza kupuuza hisia zao wenyewe.

3.      Hufundisha ubabe

Fimbo humfundisha mtoto kutumia nguvu katika kutatua migogoro anayokutana nayo. Watoto wanaochapwa, mara nyingi huwa ni wagomvi katika maisha halisi. Sababu ni kwamba mtoto hujikuta  haoni njia nyingine mbadala wanayoweza kuitumia kutatua matatizo yake. Matokeo yake huongeza uwezekano wa kuwa mtu wa mabavu, mchokozi kwa wenzake, asiyeweza kuelewa hisia za wengine na mwisho wake na yeye wenyewe hugeuka kuwa mtu anayeunga mkono fimbo kwa watoto wake. Ni namna fulani ya duara ya fimbo.

Tunaweza kubadilika

Najua watetezi wa fimbo wanasema huwezi kuheshimiwa na mtoto bila kumfanya ajisikie uchungu. Imani hii si kweli. Maumivu hayawezi kukupa heshima yako kama mzazi. Huhitaji kuumiza hisia za mtoto wako ili umfundishe maadili. Kama unataka kuheshimiwa na mwanao, mheshimu yeye pia.

Wengine wanasema huwezi kumfundisha mtoto kujidhibiti wala kuwajibika bila kumchapa. Kwamba watoto hawezi kabisa kusikiliza bila kutengenezewa mazingira ya hofu na maumivu. Imani hii si ya kweli. Unaweza kumfundisha mwanao kujidhibiti, na kuwajibika bila kumwuumiza.

Fimbo ya kweli ni kumwelewa mwanao. Kujua anafikiri nini, kwa nini anafanya anayoyafanya, na kumpenda. Upendo husitiri wingi wa dhambi. Ukimpenda mtu, hutatamani kumsababishia maumivu. Na ukimwonesha mtu kuwa yeye ni wa thamani, mara nyingi atafanya bidii ya kuthibitisha kuwa ni kweli yeye ni wa thamani. Mfanye mwanao ajione ni mtu wa thamani. Hutalazimika kutumia njia ya mkato kwa kumchapa. 

Wengine watasema, 'Kutokuchapa ni kuiga uzungu bwana!'. Zamani watu waliamini kumchapa mwanamke ni lazima. Siku hizi hakuna anayejisifia kumchapa mkewe. Unaona? Kuchapa ni mazoea tu yanayoweza kuachwa. Kama tumeweza kuacha kuchapa wake zetu, tunaweza kuacha kuchapa watoto. Ni suala la kubadili mtazamo tu.


Fuatilia safu ya Uwanja wa Wazazi, katika Gazeti la Mtanzania kila Alhamisi kwa mada kama hizi. 

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?