Mbinu za Kutafuta Ajira Mtandaoni
Changamoto
kubwa inayoweza kukukabili unapotafuta kazi, ni taarifa zitakazokusaidia kujua
uelekeze wapi maombi ya kazi. Zamani, ili kupata taarifa za kazi, watu
walitegemea radio, magazeti, televisheni na taarifa za marafiki wanaofahamiana
nao. Mambo yanazidi kubadilika kwa kasi. Sasa hivi, kwa mfano, matumizi ya
mtandao yamerahisisha namna tunavyoweza kupata taarifa hizi.
Hata
hivyo, pamoja na uwepo wa mtandao, bado kuna changamoto ya wapi hasa waweza kupata
taarifa sahihi. Mbinu zifuatazo ni matokeo ya uchambuzi wa tafiti mbalimbali na
zinaweza kukupunguzia changamoto ya kupoteza muda na nguvu nyingi kutafuta kazi
mtandaoni.
Picha: Makala hii kwenye gazeti la Mwananchi
|
Hakikisha unaonekana mtandaoni
Kuna
faida kubwa ya kuonekana mtandaoni. Kwanza, inakuwa rahisi kwa waajiri kukuona
wanapotafuta ‘kimya kimya’ mtu mwenye sifa wanazozihitaji. Aidha, inakusaidia
kufuatwa na taarifa za nafasi za kazi pale zinapopatikana bila wewe kutumia
nguvu kubwa kuzitafuta.
Ili
kupatikana mtandaoni, kw a mfano, waweza kujiunga na mtandao maarufu wa LinkedIn
unaotumika kama wasifu huru wa mtandaoni kwa watu wanaotengeneza mitandao ya
kikazi. Fikiria kujiunga na mtandao huu.
Unapokuwa
kwenye mtandao huu wa LinkedIn ni vyema kuweka taarifa zinazokusaidia
kukukutanisha na watu unaowalenga na jitahidi kushiriki mijadala inayoendana na
malengo yako. Kufanya hivi kutakusaidia
kufahamika na watu wanaoweza kukuunganisha na nafsi za kazi pale zinapotokea.
Kadhalika,
upo mtandao mzuri wa kijamii uitwao Twitter. Faida ya mtandao huu ni utamaduni
wa watumiaji wake kuufanya kuwa wa kikazi zaidi na hivyo unatumiwa na wataalam
wa kada mbalimbali. Unapoweza kuutumia vizuri kujadili masuala unayoyaelewa
vyema na uliyo na utaalam nayo, itakuwa rahisi kuonekana na watu ambao katika
hali ya kawaida usingeweza kukutana nao.
Tafuta tovuti zinazoaminika
Si
kila tovuti zinazotoa taarifa za kazi mtandaoni zinaweza kuaminika. Kama ilivyo kwenye maisha halisi, mitandaoni pia wamo
watu wenye nia ya kutumia shida za watu kujitafutia kipato. Utakumbuka hivi majuzi
zilienezwa taarifa potofu kuwa serikali ilikuwa imetangaza nafasi nyingi za
kazi. Ilibidi mamlaka zinazohusika kukanusha taarifa hizi.
Mambo
kadhaa yanayoweza kukusaidia kufahamu ikiwa taarifa za kazi unazozipata
mtandaoni ni sahihi ama la. Kwa mfano, hakikisha tovuti ya taasisi au kampuni
inayodaiwa kutangaza nafasi za kazi kweli inapatikana mtandaoni na inalo
tangazo hilo.
Haiwezekani idara au taasisi makini itoe tangazo la kazi na
ifanye kosa la kutokuweka taarifa hizo kwenye tovuti yake. Matangazo ya kazi
yenye kuweka tovuti za waajiri zisizopatikana, mara nyingi huwekwa mtandaoni na
watu wenye nia mbaya.
Hakikisha
taarifa unazotaka kuzifanyia kazi ni rasmi kabla kujaamua kuchukua hatua yoyote
ya kuomba kazi husika. Usifanye haraka kuamini na kufanyia kazi taarifa
zinazopatikana kwenye tovuti/blogu zisizothibitishwa. Kazi zinazotangazwa na
idara na mashirika ya umma, kwa mfano, ni lazima zipatikane katika tovuti rasmi
za serikali.
Jambo
la pili, hakuna taasisi inaweza kutangaza nafasi za kazi mtandaoni na zikudai
fedha ili uitwe kwenye usaili. Unapokutana na madai yoyote ya ada, elewa
kinachoendelea. Aidha, wakati mwingine, si tu waweza kuombwa kiasi cha fedha,
lakini pia waweza kuombwa taarifa zako binafsi na nyeti kwa madai ya kuwezesha
mchakato wa kuomba kazi.
Vile
vile, ni lazima tangazo la kazi lioneshe mawasiliano yanayoeleweka kama vile
barua pepe rasmi zenye ‘domain’ zinazofanana na majina ya taasisi husika.
Unapokutana na taarifa muhimu zisizoambatana na mawasiliano yasiyo rasmi, mfano
barua pepe ya ‘gmail’, ‘yahoo’, ‘hotmail’ na nyinginezo, fikiria mara mbili.
Ingawa
ni kweli katika mazingira yetu taasisi na idara nyingi zinaweza kutumia barua
pepe zisizorasmi, ni muhimu, hata hivyo, kuhakiki mambo mengine muhimu kama
namba za simu, nukushi na anuani ya posta. Hayo yote ni kujaribu kujiridhisha
kabla hujawekeza nguvu zako kuomba kazi isiyokuwepo.
Fahamu unataka nini
Mtandao
wa intaneti una kila aina ya taarifa. Unapotafuta kitu usichokuwa na uhakika
nacho mtandaoni ni rahisi kuchanganyikiwa na hivyo unaweza usifikie malengo
yako. Ni muhimu kuamua unatafuta kazi gani kutoka kwa waajiri gani na wapi ili
uweze kuelekeza nguvu zako kwenye lengo mahsusi.
Kwa
mfano, kama unatafuta kazi ya Uhasibu, usitumie muda wako kutafuta taarifa
zisizohusiana na Uhasibu. Jikite kutafuta taarifa zinazohusiana na wasifu (ujuzi)
wako.
Kadhalika,
unapojua unahitaji kazi gani, itakuwa rahisi kwako kutafuta taarifa za taasisi
au idara zinazoweza kukuajiri. Tembelea tovuti za waajiri unaowafikiria kujua
ikiwa wameweka tangazo la kazi.
Kwa
mfano, kama una lengo la kupata kazi katika kampuni za habari, unahitaji kuwa
na tabia ya kufuatilia tovuti zao mara kwa mara. Maana, huko kwenye tovuti zao
ndiko zinakopatikana taarifa rasmi.
Chukua tahadhari
Unahitaji
kuwa makini na taarifa unazoweka mtandaoni. Fahamu kuwa mara unapoweka taarifa
zako mtandaoni, unapoteza udhibiti wake na watu usiowafikiria wanaweza
kuzitumia kwa malengo yoyote.
Kadhalika,
taarifa zinazojenga taswira isiyokubalika katika jamii zinaweza kukuathiri
katika safari yako ya kupata kazi itakayotimiza ndoto zako. Wapo waajiri wengi,
kwa mfano, huchunguza taarifa za waomba kazi mtandaoni ili kufanya
maamuzi. Tafiti zinaonesha zaidi ya nusu
ya waajiri hujaribu kupekua wasifu wako mtandaoni kabla hawajakuita kwenye
usaili. Ndio kusema, ni bora usipatikane mtandaoni kuliko kujenga taswira itakayokuletea
hasara.
Fuatilia Jarida la Kazi na Ajira ndani ya gazeti la Mwananchi kwa makala kama hizi.
Mimi
JibuFutaDaud
FutaHabar naitwa eddy Thomas natafuta ajila ya udereva ni mzowef sana hii kazi napatikana tabata atakyonihitaji namba zangu za simu number ni 0748657118 makubaliano yako nipigie mda wowote
JibuFuta