Unatafuta Kazi? Sifa Sita Unazozihitaji
Katika
makala yaliyopita tuliona takwimu zinazothibitisha kuwa
tatizo la ajira ni zaidi ya kukosekana kwa nafasi za kazi. Ingawa watafuta kazi
wengi hufanya juhudi za kuthibitisha kuwa wanao ujuzi rasmi waliousomea
darasani, si waajiri wengi wanathamini alama za darasani zinazoonekana kwenye
vyeti vya waombaji hao.
Badala yake, mwajiri kwa kawaida hutafuta ujuzi ambao mara
nyingi mtafuta kazi hautegemei. Ujuzi huo, tulioupachika jina la ‘ujuzi mwepesi’,
ni pamoja na ule uwezo wa kutumia maarifa ya jumla ya darasani katika kufumbua
matatizo halisi yanayomkabili mwajiri katika eneo lake la kazi.
Kwamba waajiri wanatafuta ujuzi ambao si mara nyingi
hupatikana darasani, ndio sababu matangazo mengi ya nafasi za kazi hayaweki msisitizo
mkubwa katika sifa za kitaaluma anazohitajika kuwa nazo mwomba kazi bali ‘ujuzi
mwepesi’ tutakaoujadili katika makala haya.
Je, mwajiri hutarajia ujuzi gani kwa mwombaji wa kazi?
Tutazame mifano michache.
Ubunifu
Mwajiri mzuri anategemea kuona namna gani mwajiriwa anaweza
kufikiri nje ya mazoea. Huu ni uwezo wa kufikiria majibu yasiyozoeleka ya
changamoto zilizozopo ili kuongeza ufanisi wa kazi. Ubunifu ni pamoja na namna
mwajiriwa anavyoweza kutumia raslimali chache zizizopo kuleta matokeo
yanayozidi matarajio.
Kwa mfano, unapoweza kutumia Tsh 100 kuleta matokeo yale yale
ambayo yangeweza kuletwa kwa kutumia Tsh 1,000, hapo unakuwa umelazimika
kufikiri nje ya sanduku la mazoea. Kwa kuweza kutumia raslimali kidogo kuleta
matokeo makubwa unakuwa umemnufaisha mwajiri wako, jambo ambalo kwa hakika ni
kipaumbele kikuu cha waajiri wengi.
Uongozi
Uongozi ni uwezo wa kuwaonyesha njia na kuwahamasisha wengine
kufikia malengo mapana ya mwajiri. Kuwa kiongozi maana yake unaweza kujisimamia
mwenyewe na kuwasaidia wengine pia kuelekea kule kunakotarajiwa na mwajiri.
Uongozi si sawa na madaraka. Hizi ni dhana mbili tofauti
lakini zenye uhusiano wa karibu. Waweza kuwa na madaraka rasmi kazini lakini
katika utendaji usiwe na chembechembe zozote za kiongozi.
Uongozi ni uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa ushirikiano na
wengine pasipo kusimamiwa kwa karibu na wakubwa wenye madaraka ya kikazi.
Uongozi ni pamoja na namna unavyoweza kufanya majukumu mengine kwa moyo wa
hiari na kujituma ili kufikia malengo mapana ya mwajiri. Huhitaji kukasimiwa
urasimu wa madaraka kuweza kutekeleza
hilo.
Mahusiano bora na wengine
Kwa kawaida, kazi nyingi zenye kuleta tija zinahitaji
ushirikano wa karibu wa watu mbalimbali. Ili kuleta ufanisi, kunahitaji
uhusiano mzuri wa kikazi baina ya mwajiriwa na watu wengine. Bila mahusiano
mazuri na wengine, pengine kwa sababu ya ile hulka ya kupenda kuwazidi wengine,
ufanisi wa pamoja wa kazi husika unaweza kuwa mashakani.
Namna gani mwajiriwa anaweza kusaidiana na wengine
kufanikisha malengo ya mwajiri pasipo ushindani usio na tija, hayo ndiyo
mahusiano ya kikazi.
Mawasiliano
Hakuna mahusiano na wengine pasipo mawasiliano. Mambo mengi katika kazi yanalazimu wafanyakazi kufanya mawasiliano yasiyo rasmi kwa kutumia maandishi au mazungumzo yam domo. Mfano kuna nyakati mwajiriwa atalazimika kuwasilisha taarifa au maoni yake kwa wakubwa wake wa kazi. Kadhalika, atalazimika kuwasiliana na wale anaofanya nao kazi. Hapa ndipo uwezo mzuri wa kuwasiliana unapohitajika.
Ingawa matumizi ya lugha yanatofautiana baina ya mazingira ya
kazi, bado ni wazi katika mazingira mengi ya kikazi tunalazimika kuelewa namna
nzuri ya kuwasiliana na watu. Uwezo wa lugha una nafasi kubwa katika kazi.
Nidhamu
ya kazi
Ufanisi katika kazi, kwa kiasi kikubwa, unategemea nidhamu.
Namna gani mwajiriwa anaheshimu kazi yake kwa kuwahi kazini, kuwasilisha
mrejesho wa kikazi kwa muda hiyo ndiyo inaitwa nidhamu ya kazi.
Kadhalika, nidhamu ya kazi ni pamoja mpangilio mzuri wa jumla
wa majukumu ya kila siku unaotanguliwa na utunzaji wa muda. Mwajiri mzuri
hatarajii mtu anayeweza kufanya kazi kizembe bila kufuata taratibu za kikazi
zilizowekwa.
Uzoefu
Uzoefu
Namna gani mwajiriwa anaonesha ushahidi kwamba anao uwezo wa kufanya kazi inayokusudiwa, huo ndio uzoefu. Mwajiri yeyote makini angependa kuona uthibitisho dhahiri kwamba mwombaji wa kazi au mwajiriwa anao uwezo wa kumudu majukumu anayoyaomba kwake au yale aliyoyakabidhiwa.
Uzoefu huu unaweza kupatikana kupita kazi ulizopata kuzifanya kabla ya ajira husika iwe kwa ajira rasmi au kwa kujitolea. Kwa mtafuta kazi asiye na historia ya kuajiriwa, anahitajika kujifunza kutafuta fursa za kujitolea kufanya kazi zinazofanana na ajira anayoitamani wakati akiendelea na masomo au katika kipindi cha mpito anaposubiri kuajiriwa.
Tunavyoweza kuyaonesha haya
Ingawa ni kweli kuwa nchi yetu inakabiliwa na ukosefu wa ajira, bado ni wazi waajiriwa wengi hawaajiriki kwa maana ya kukosa weledi na ujuzi unaowawezesha kuajiriwa na kudumu katika ajira zao. Ujuzi huu, kama tulivyoona, si mara zote unaweza kupatikana kupitia mfumo wa mitihani na vyeti. Ni muhimu kufanya jitihada za makusudi kujinoa kwa lengo la kujiongeza kiujuzi.
Katika kufanya maombi ya kazi na hata pale tunapotekeleza majukumu yetu kazini tunawajibika kuthibitisha kuwa ni kweli tunao ujuzi huu mwepesi. Katika makala zijazo, tutazungumzia kile kinachoweza kufanyika katika kuwasaidia watafuta kazi kujiongezea ujuzi huu tulioupitia hapa kwa haraka na, kadhalika, namna ya kuandika barua na maelezo binafsi (wasifu) yanayoonyesha haya tuliyoyajadili kwa kifupi.
Fuatilia Jarida la Ajira na Kazi ndani ya gazeti la Mwananchi kila Ijumaa kwa makala kama hizi.
Maoni
Chapisha Maoni