Mambo Sita ya Kufanya Unapotafuta Kazi

Kutafuta kazi ni kuingia kwenye soko la ajira ambalo kimsingi ni uwanja unaowakutanisha watu wenye mahitaji makubwa ya aina mbili. Upande mmoja, wapo watu wenye ‘bidhaa’ ya ujuzi na weledi, lakini wenye hitaji la kujipatia kipato kwa kutumia ujuzi na maarifa waliyonayo. Hawa wanaitwa watafuta kazi.

Upande wa pili, wapo watu wenye uhitaji wa ujuzi huo ili uwasaidie kuongeza ufanisi wa huduma wanazotoa kwa kutumia raslimali na fedha za kuulipia ujuzi huo. Hawa wanaitwa waajiri. Pande hizi mbili zinahitajiana na kutegemeana kwa maana ya hitaji la upande mmoja hufanyika jawabu la upande wa pili.

Ili uweze kuajirika, unalazimika kumridhisha mwajiri kuwa unao ujuzi na uwezo wa kutumia maarifa uliyonayo katika kuongeza ufanisi wa huduma anazozitoa. Kutokana na ukweli kwamba waajiriwa hutofautiana ujuzi na uwezo huo, na kwa sababu uwezo wa waajiri kadhalika hutofautiana, na kwa kuwa haiwezekani kila mwenye ujuzi kukidhi mahitaji ya mwajiri, hapa ndipo dhana ya ushindani wa soko la ajira inapojitokeza.

Ndio kusema, ili kuweza kushindana vyema katika soko la ajira ni jukumu la mtafuta kazi kujiandaa ipasavyo kiujuzi na kiweledi. Tuangalie mambo sita muhimu ya kufanya unapoingia kwenye soko la ajira ili kuongeza uwezekano wa kuajirika.
PICHA: reamstime.com

Jenga utambulisho wako

Utambulisho wako ni  kama kutangaza bidhaa uliyonayo sokoni. Kwa wewe unayetafuta kazi, bidhaa yako ni ujuzi ulionao, maarifa na fikra zinazokutambulisha kwa wengine. Ni muhimu sana kutafuta mazingira ya kutangaza bidhaa yako.

Katika dunia ya leo mawasiliano yamerahisishwa sana.  Ingia mitandaoni, jenga taswira yako kwa kujihusisha kwa bidii na maeneo uliyobobea.  Kuna mitandao kama Facebook, Twitter, Blogu, LinkedIn,  ambayo yote hiyo ni bure kabisa. Hulipii chochote zaidi ya kuunganishwa na mtandao wa intaneti.

Badala ya kutumia mitandao hiyo kupiga porojo na kufuatilia habari zisizokusaidia, itumie kuonesha mchango ulionao katika jamii. Kupitia unayoyaandika, watu watakuona na itakusaidia kuongeza ushindani wako katika soko la ajira.

Fahamu zinakopatikana taarifa za ajira

Unalazimika kufuatilia kwa karibu vyanzo mbalimbali vya habari kupata taarifa za ajira. Zipo tovuti maalum zilizoandaliwa na watu na taasisi binafsi kwa minajili ya kusambaza habari za kazi. Serikali nayo, kwa mfano, inao ukurasa maalum uitwao http://portal.ajira.go.tz/  kukusaidia kupata taarifa za nafasi za kazi serikalini kila zinapotolewa.

Vile vile, 
Wizara ya Kazi na Ajira inacho kitengo maalumu kiitwacho Wakala wa Huduma za Ajira (TaESA) ambao pamoja na majukumu mengine hutoa huduma ya ushauri na takwimu kuhusu masuala ya ajira kwa waajiri na watafutaji kazi, kusambaza taarifa za soko la ajira kwa wadau mbalimbali pamoja na kuunganisha watafuta kazi na waajiri ndani na nje ya nchi. Wafuatilie kupitia ukurasa wao http://www.taesa.go.tz/jobs.

Tengeneza mtandao

Mara nyingi tunatarajia kuwa nafasi za kazi hutangazwa.  Lakini wakati mwingine kazi nyingi hasa katika sekta binafsi huwa hazitangazwi wazi wazi. Sababu ni kuwa waajiri wengi wana tabia ya kutafuta watu wanaoaminika, na wakati mwingine kwa kuelekezwa na watu wanaoeleweka.

Ni kwa sababu hiyo ni muhimu kutengeneza mtandao wa watu wanaoaminika wanaoweza kukusaidia kupata taarifa za kazi pale zinapopatikana. Shiriki makongamano, semina na warsha ambazo pamoja na kukukuza kiujuzi, zitakukutanisha na watu mbalimbali wanaoweza kuwa msaada kwako katika safari ya kutafuta ajira.

Jitolee kufanya kazi bila malipo

Utamaduni wa kujitolea haujazoeleka katika jamii yetu. Matarajio ya wahitimu wengi baada ya kumaliza vyuo ni kusubiri ajira zenye malipo na hawako tayari kufanya ‘kazi zisizolipa’. Ikiwa umetafuta kazi kwa muda fulani na hujafanikiwa bado, pengine changamoto ni kukosekana kwa uzoefu unaohitajika na waajiri.

Ili kukabiliana na changamoto hii, tumia muda wako wa mpito kujitengenezea uzoefu unaohitajika bila ajira rasmi. Jitolee kufanya kazi bila malipo. Tafuta taasisi zinazotoa huduma zinazolingana na ujuzi wako. Onesha nia ya kutafuta uzoefu. Kufanya hivyo kutakusaidia kuboresha taarifa zako za uzoefu, na hivyo  kukuongezea sifa za kuajirika.

Andaa nyaraka zako vizuri

Ubora wa taarifa zako binafsi unakuweka katika nafasi kubwa kumshawishi mwajiri kukukubali. Tumia kipindi cha mpito kuweka vizuri taarifa zako binafsi (CV) zikusaidie kuboresha maombi ya kazi utakayoyatuma baadae. Inashauriwa kupitia maelezo yako mara kwa mara ili kuyafanya yakupambanue vizuri wewe ni nani, una ujuzi upi, elimu na uzoefu gani.

Vile vile, ni muhimu kuandaa barua za maombi kwa kila kazi utakayoomba. Kwa kawaida, barua ya kazi hubadilika badilika kuendana na mahitaji mahususi ya tangazo la kazi inayoombwa. Nyaraka zote hizi ni vyema kuandaliwa mapema ili iwe rahisi kuzirekebisha kukidhi mahitaji ya kazi inayombwa.

Punguza matarajio, usikate tamaa

Kuwa na matajirio ya kupata kazi nzuri yenye heshima ni jambo jema. Ndoto ni muhimu. Lakini, wakati mwingine, waweza kuanza na kidogo kinachopatikana kikuwezeshe kupata unachokilenga. Katika mazingira yenye ushindani mkubwa wa ajira, si busara kuchagua sana kazi.

Aidha, kutafuta kazi ni mchakato unaoweza kukuchosha. Wakati mwingine waweza kupata majibu yanayokatisha tamaa. Huna sababu ya kukata tamaa.  Jipe moyo kuwa katika maisha hakuna kizuri kisicho na gharama. Unapokuwa na matumaini, utaweza kufuatilia mambo yako kwa umakini mzuri zaidi.

Fuatilia Jarida la Kazi na Ajira ndani ya gazeti la Mwananchi kila Ijumaa kwa mada kama hizi. Twita: @bwaya, Simu: 0754 870 815

Maoni

  1. Kale Karoho kakuchagua kazi...daah kanapaswa kukemewa kwa nguvu zote..asante kwa ujumbe

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?