Jinsi ya Kumfundisha Mtoto Kuwa Mwuungwana
Umewahi
kumpa mtu kitu anachokihitaji lakini haoni sababu ya kusema, ‘asante’? Mtu
anakukosea na hawezi kusema, ‘samahani’, ‘nisamehe’? Wapo wengine hata ufanye
vizuri namna gani kusema, ‘hongera umefanya vizuri’ ni kama adhabu na kujishushia
hadhi. Hizi ni baadhi ya tabia zinazoweza kuonesha namna mtu asivyo muungwana
na zinaweza kumpunguzia thamani yake mbele ya jamii.
Uungwana
ni namna mtu anavyoweza kujali hisia za wengine. Kuelewa mwenzako anataka nini,
anajisikiaje unaposema maneno fulani, anachukuliaje unapomfanyia mambo fulani
na mengineyo kama hayo.
Kuna
msemo uliozoeleka kuwa tabia za watoto ni sura ya walivyo wazazi wao. Tafsiri
ya msemo huu ni kuwa kile anachokifanya mtu, kwa kiasi kikubwa, kinatokana na
yale anayojifunza kwa wazazi wake. Ndio kusema uungwana anaojifunza mwanao
unakutegemea namna wewe mzazi unavyojiweka mbele yao, kwa maneno, kwa matendo
na hata kwa tabia.
Uungwana ni tabia tunayojifunza. Hatuzaliwi nayo PICHA: @bwaya |
Hebu
tutazame mambo manne muhimu unayoweza kuyawekea mkazo unapomfundisha mwanao
uungwana.
Kushukuru
Kushukuru
ni kurudisha fadhila unazotendewa na wengine. Unapopewa huduma nzuri dukani,
kwa mfano, ni uungwana kushukuru hata kama ni kweli umeilipia huduma hiyo.
Tabia ya kushukuru tunajifunza na hatuzaliwi nayo. Ikiwa unataka mwanao awe mtu
mwenye uwezo wa kutambua mema anayotendewa na wengine, ni muhimu uitilie mkazo
tabia hata ikibidi kwa kuweka mazingira ya kulazimisha.
Mfano,
jenga utaratibu wa kudumu unaomlazimisha kila aliyeshiriki chakula hapo
nyumbani kusema, ‘asante’. Utamaduni huu wa kushukuru unawezekana ikiwa wewe
mwenyewe utaanza kuonesha mfano. Mshukuru mwezi wako mbele ya watoto wako.
Washukuru watoto wako wanapokutendea kile unachokipenda. Kadhalika, wakumbushe
kushukuru kila wakati.
Kupongeza
Mtu
mwingine anapofanya jambo zuri ni uungwana kumpongeza. Pongezi humfanya
anayepongezwa kujisikia vizuri. Mfundishe mtoto kutambua mazuri yanayofanywa na
wengine na kutamka maneno sahihi.
Kuwa
mfano kwa kutoa pongezi. Tafuta kutambua jitihada zinazooneshwa na wanafamilia
na toa pongezi kwa moyo wa dhati. Kwa mfano, wapongeze watoto kwa jitihada
wanazoonesha katika masomo. Mpongeze mke/mume wako anapofanya vizuri mbele ya
watoto na bila aibu. Wahimize wanao kupongezana ili kujenga tabia ya kupongeza
wengine.
Kuomba msamaha na kusamehe
Kukosea
ni sehemu ya mapungufu yetu kama binadamu. Lakini si kila mtu anaweza kuwa
tayari kuomba msamaha hata pale anapojua amekosea. Wanafikiri kuomba msamaha ni
kujishushia hadhi zao. Ikiwa unataka mwanao awe na tabia ya kuomba msamaha na
kuwasamehe wanaomkosea unawajibika kumfundisha.
Onesha
mfano wewe mwenyewe kwa kuomba msamaha mbele ya wanao. Mwombe msamaha mke/mume
wako hata kwa mambo madogo unayomkosea. Waombe msamaha wanao unapogundua umefanya
kosa.
Walazimishe na wao kuombana msamaha wanajikuta kwenye makosa. Ukweli ni
kwamba mtoto anapokuwa na tabia ya kuomba msamaha, ni rahisi kusamehe wengine pale
anapokosewa.
Kuwajali wengine
Kuthamini
wengine ni kujiona kuwa huwezi kuwa bora kuliko watu wengine. Hiyo haina maana
kuwa hujiamini. Hapana. Kimsingi unapojiamini ni rahisi sana kuwathamini
wengine. Unao wajibu wa kumfundisha mwanao tabia ya kuwathamini watu wengine.
Anza
kwa kuwaonesha watoto wako vile unavyowathamini. Wanapoumia, onesha kujali na
wape pole bila kuchelewa. Watakapojua unawajali, hawatapata tabu kuwajali
wengine. Wakumbushe wajibu wao wa kutoa pole kwa wenye shida na wanaoumia. Kwa
kufanya hivyo utajenga mazoea mazuri ya kuwajali wengine.
Fuatilia safu ya Uwanja wa Wazazi
kila Alhamisi kwenye gazeti la Mtanzania kwa makala kama hizi.
Maoni
Chapisha Maoni